Kocha JKU ashangaa Mlandege kuwafunga mabao machache

By Hawa Abdallah , Nipashe
Published at 07:27 AM Oct 07 2024
 Kocha JKU ashangaa Mlandege kuwafunga mabao machache
Picha:Mtandao
Kocha JKU ashangaa Mlandege kuwafunga mabao machache

KOCHA Mkuu wa JKU SC, Salum Ali Haji, amesema timu yake ilistahili kufungwa katika mchezo wao wa nne dhidi ya Mlandege FC, kutokana na kiwango walichoonesha wachezaji wake.

Mabingwa hao watetezi walikubali kichapo cha mabao 3-1 kutoka kwa Mlandefe FC mchezo uliochezwa juzi, Jumamosi katika dimba la New Amaan Complex majira ya saa kumi alasiri.

Mlandege FC huo unakuwa mchezo wao wa kwanza kupata alama tatu baada ya kutawaliwa na matokeo ya sare wakati JKU SC umekuwa wao wa kwanza kupoteza baada ya kushinda michezo mitatu mfululizo.

Akizungumza baada ya kumalizika mechi hiyo, Kocha Salum alisema walistahili kufungwa mabao mengi zaidi ya hayo waliyofungwa kutokana na mchezo wenyewe ulivyokuwa.

Alisema katika kipindi cha kwanza timu yake ilikuwa bora na ilicheza vizuri dakika zote za kipindi hicho tofauti na kipindi cha pili ambapo wapinzani wao walimiliki mpira zaidi.

Kocha huyo alisema kipindi cha pili walizidiwa katika maeneo yote na kusababisha wapinzani wao kutawala mchezo huo hadi filimbi ya mwisho ya mwamuzi.

“Ni sehemu tu ya mchezo huu haukuwa bahati yetu, tulizidiwa kila eneo, wachezaji walijitajidi kukaa katika nafasi zao, lakini walipoteana kutokana na presha ya mchezo wenyewe na mashambulizi ya mara kwa mara katika lango letu,” alisema.

Hata hivyo, alisema kupoteza mchezo huo haimaanishi kama wamepoteza lengo lake la ubingwa, kwani bado wanayo nafasi katika michezo 11 iliyobaki ya mzunguko huu wa kwanza.