KIKOSI cha Fountain Gate kimeanza mapema maandalizi ya mchezo wao dhidi ya Namungo ili kuepuka kilichowatokea Desemba 17, mwaka huu, kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam kwa kuchapwa mabao 2-0 na Azam FC.
Akuzungumza jana kutoka Babati mkoani Manyara, Ofisa Habari wa Fountain Gate, Issa Mbuzi, alisema mchezo wao dhidi ya Namungo unatarajiwa kupigwa Desemba 25, mwaka huu, ambapo itakuwa ni Sikukuu ya Krisimasi, kwenye Uwanja wa Tanzania Kwaraa, lakini wameanza kujiandaa mapema kwa sababu hawataki kitu kama kile kijirudie tena.
"Hatutaki kile kilichotupata kwenye Uwanja wa Azam Complex cha kufungwa mabao 2-0 na Azam FC kijirudie tena, tunafanya maandalizi makubwa ili kucheza na Namungo kwenye uwanja wetu na wa nyumbani, tunaimani na maandalizi ambayo tunaendelea nayo, tutapata ushindi na kuwafurahisha mashabiki wetu," alisema Mbuzi.
Ofisa Habari huyo alibainisha kuwa kikosi chao kilianza Ligi Kuu vema na kuna wakati kiliongoza ligi, lakini baadaye hali ilibadilika na kuanza kupoteza, akisema hali hiyo huwa inatokea kwenye mchezo wa soka.
Wakati Mbuzi akisema hayo, Kocha Mkuu, Mohamed Muya, alibainisha kuwa kipindi hiki cha dirisha dogo ataangalia zaidi kuimarisha upande wa ulinzi kwani unaonekana kuwa una matatizo.
Mmiliki wa klabu hiyo, Japhet Makau, amekiri kuwa na changamoto eneo la ulinzi na kuahidi kulifanyia marekebisho, huku akiisifu safu yake ya ushambuliaji kuwa ni moto wa kuotea mbali.
"Nadhani sisi ni moja kati ya timu iliyofunga mabao mengi kwenye Ligi Kuu, changamoto ipo kwenye safu ya ulinzi, tutarekebisha hilo," alisema.
Fountain Gate imefunga mabao 23 mpaka sasa, ikishika nafasi ya pili kwa kufunga mabao mengi kwenye ligi nyuma ya Simba yenye mabao 24, lakini pia inakamata nafasi ya pili kwa kuruhusu mabao mengi, ikifanya hivyo mara 25, nyumba ya KenGold ambayo imeshabugizwa mabao 27 mpaka sasa.
Timu hiyo ina wachezaji wawili wanaofuatana kwa kusaka kiatu cha dhahabu ambao ni Selemani Mwalimu mwenye mabao sita, akiwa kwenye nafasi ya pili nyuma ya Elvis Rupia wa Singida Black Stars mwenye mabao saba, na Edgar William mwenye mabao matano.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED