Kakolanya, Singida FG ngoma bado mbichi

By Saada Akida , Nipashe
Published at 09:42 AM Apr 24 2024
Golikipa  Beno Kakolanya.
Picha: Maktaba
Golikipa Beno Kakolanya.

UONGOZI wa Singida Fountain Gate FC, umesema bado unatambua kipa Beno Kakolanya ni mali yao, lakini hatima yake itajulikana ndani ya saa 72 kuanzia jana.

Kupitia Ofisa Habari wa timu hiyo, Hussein Massanza, amesema suala la hatua gani itamchukulia kipa huyo ni baada ya Kamati ya Nidhamu itakapokutana na kujadili suala lake.

Kauli hiyo imekuja baada ya kipa huyo kugomea wito wa kamati hiyo ambayo ilitakiwa kukutana naye Aprili 19, mwaka huu, kwa ajili ya mahojiano na kumpa nafasi ya kujieleza.

Kipa  huyo hakutokea katika kikao hicho na baadaye kuandika barua kwa kamati hiyo kuwa viongozi walifanya makosa ya kutoa tuhuma kuwa anaihujumu timu hiyo kwa kitendo cha kuondoka kambini kwa ruhusu ya Meneja wa timu.

Imeelezwa kipa huyo ameondolewa katika 'group' (kundi) la mtandao wa kijamii la wachezaji ambalo anaweza kupata taarifa mbalimbali za klabu hiyo.

Akizungumza na Nipashe jana, Massanza alisema hatma ya kipa huyo adhabu au atasamehewa ni hadi kamati hiyo itakapokutana leo na ndani ya saa 72 watatoa maamuzi yao ila hadi sasa wanatambua Kakolanya bado ni mchezaji wao halali.

“Suala la kuondolewa katika group la timu na amekuja Mwanza kuchukuwa vitu vyake sifahamu, ninachafahamu ni kwamba kipa huyo hayupo kambini kabla ya kucheza mechi yetu dhidi ya Yanga, suala la adhabu gani atachukuliwa baada ya kugomea wito ni maamuzi ya kamati,” alisema Massanza. 

Hata hivyo, chanzo chetu ndani ya klabu hiyo kilisema kipa huyo ameondolewa moja kwa moja ndani ya kikosi hicho baada kutuhumiwa kuwa anahujumu timu hiyo, hivi karibuni walipokuwa wakicheza na Yanga mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Alipotafutwa Kakolanya alieleza sababu ya kutokwenda kwenye kamati hiyo baada ya kupokea Barua ya wito wa Kamati ya Nidhamu Aprili 19, mwaka huu, aliipeleka kwa mwanasheria wake (hakumtaja jina), ambapo alimshauri wanapaswa kuwajibu kwanza,

“Mwanasheria wangu akaipitia vizuri Sana, baada ya hapo aliniambia lazima tuwajibu kwani kuna makosa Singida Fountain Gate FC wameyafanga kwa kutoa hukumu mitandaoni, kupitia ukurasa wao na kurasa zingine kubwa za mitandao ya kijamii.

"Kwa hiyo nikaandika barua ya kutokuhudhuria kwenye kikao cha kamati ya nidhamu kwa kuwa tayari wameshanihukumu  hivyo hata nikienda kwenye  kikao kitakuwa si halali na ni kinyume cha sheria. Wao walitakiwa waniite kwanza wanisikilize kabla ya kutoa hukumu kwa hiyo kwenye kikao hicho nisingepata haki yangu ya msingi,” alisema Kipa huyo.