Simba, Tabora Utd vita vya nafasi leo

By Saada Akida , Nipashe
Published at 09:03 AM May 06 2024
news
Picha: Simba
Juma Mgunda na Sulemain Matola wakiwa katika moja ya mchezo wa Simba.

POINTI tatu, ndiyo wimbo unaoimbwa na makocha Juma Mgunda wa Simba na Ben Fabian wa Tabora United, kuelekea mchezo wa leo ambapo kila mmoja akiwa na malengo yake.

Wekundu wa Msimbazi wanazihitaji alama hizo kwa ajili ya kusaka nafasi ya pili ya Ligi Kuu Tanzania Bara wakati Tabora United wakizitaka pointi hizo ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kujinasua kutoka nafasi ya chini ya kwenye msimamo na kusalia Ligi Kuu msimu ujao.

Timu hizo mbili leo zinakutana kwa mara ya pili msimu huu, Simba wakiwa wenyeji wa mchezo huo wakiwakaribisha Tabora United, Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi jijini Dar es Salaam, saa  12:15 jioni.

Simba wataingia dimbani wakiwa  nafasi ya tatu kwenye msimamo na alama 50 baada ya kucheza michezo 23 wakiwa na mchezo mmoja mkononi na Tabora United ambayo ipo nafasi ya 15 wakikusanya pointi 23 kwa michezo 24 ambayo tayari imecheza.

Wekundu wa Msimbazi hao wanaingia uwanjani wakiwa na kumbukumbu ya ushindi katika mchezo uliopita wa ligi hiyo baada ya kuichapa Mtibwa Sugar mabao 2-0, wakati Tabora United wakitoka kupokea kichapo cha mabao 3-0 mbele ya Yanga katika mchezo wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho la CRBD Bank.

Kwa msimu huu timu hizo zimekutana mara moja katika ligi tu na Simba kufanikiwa kushinda mabao 4-0 dhidi ya Tabora United wakiwa nyumbani katika dimba la Al Hassan Mwinyi, Tabora.

Kuelekea mchezo huo, Kaimu Kocha Mkuu wa Simba, Mgunda alisema maandalizi yameenda vizuri dhidi ya Tabora United na haijalishi wanakutana na timu ipo kwenye nafasi gani.

Alisema hakuna mchezo rahisi katika Ligi Kuu na hawaangalii wako katika hali gani zaidi ya kuandaa timu yao kwa ajili ya kushindana nao na kufikia malengo ya kusaka pointi tatu muhimu.

“Ni kweli tulikuwa na mapungufu kwenye mechi iliyopita na kurudi uwanja wa mazoezi kwa ajili ya kuyapunguza na ikiwezekana kuyaondoa kabisa ili leo tuwe vizuri dhidi ya Tabora United.

"Tunaenda kushindana na washindani wenzetu, mambo mengine tutakuja kujua mwisho wa msimu. Mchezaji yeyote anayesajiliwa na timu basi wajibu wao ni kuitumikia hali ambayo haitakuja kushangaza kuwapo na mabadiliko ya kikosi,” alisema Mgunda.

Kocha Msaidizi wa Tabora United, Fabian, alisema maandalizi yamekamilika kwa asilimia 90 na kwamba hawana majeruhi yeyote na waaamini mchezo utakuwa mgumu.

Alisema wanatambua Simba wanahitaji kupata matokeo ili kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kumaliza nafasi ya pili, lakini pia wao wanataka alama kwa ajili ya kujiondoa nafasi ya chini.

“Presha ni kubwa sana upande wetu kwa sababu ya nafasi tuliyopo,  tunataka kupata matokeo mazuri, tumewaangalia Simba ubora wao, tutaingia kwa tahadhari kubwa kuhakikisha tunapata matokeo chanya katika mchezo wa leo,” alisema Fabian.