Dk. Yonazi aagiza kuwekwa anwani za makazi Hanang

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 01:46 PM May 05 2024
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dk. Jim Yonazi, wapili kushoto akikagua maendeleo ya ujenzi wa nyumba za wahanga Hanang.
PICHA: MAULID MMBAGA
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dk. Jim Yonazi, wapili kushoto akikagua maendeleo ya ujenzi wa nyumba za wahanga Hanang.

KATIBU Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu, Dk. Jim Yonazi amesisitiza uwekaji wa anwani za makazi katika nyumba za wahanga wilayani Hanang ili kurahisisha ufikishaji wa huduma zinazoletwa kwa wananchi hao.

Ameyasema hayo baada ya kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa nyumba 108 za waathirika wa maafa ya maporomoka ya mawe, tope na miti kutoka mlima Hanang’ yaliyotokea Wilayani Hanang’ Mkoani Manyara mwishoni mwa mwaka Jana.

Amesema serikali imetenga eneo la ekari 100 ambako jumla ya viwanja 269 vimepimwa kati ya hivyo, viwanja 226 ni makazi, 26 ni makazi na biashara na 17 ni maeneo ya huduma za kijamii, huku akisisitiza wakandarasi kukamilisha ujenzi kwa wakati na kuzingatia ubora.

“Mradi ukamilike kwa wakati kama ilivyokubalika yaani ndani ya siku tisini na uendane na thamani ya fedha itakayotumika pamoja na hilo endeleeni kushirikiana na wenyeji wa eneo hili ili kuimarisha mahusiano na wazawa,” amesisitiza Dk. Yonazi.

Akizungumza kuhusu maendeleo ya mradi huo Luteni Kanali Ashraf Hassan, ameahidi kuhakikisha kuwa maelekezo yaliyotolewa na kiongozi huyo yanazingatiwa ili ujenzi ukamilike kwa wakati.

Aidha, ameeleza kuwa ujenzi huo wa nyumba 73 umefikia asilimia 40, na unajengwa kwa kuzingatia vigezo vya ubora uliokusudiwa na serikali.

"Tumefurahi kutembelewa na Katibu Mkuu Dk. Yonazi ambaye ameeleza kuridhishwa na maendeleo ya mradi, na sisi tunamuahidi kuwa ujenzi huu utakamilika kwa wakati lakini pia kwa kuzingatia viwango vya ubora vilivyoelekezwa," amesema Hassan.

Hata hivyo, amesema mradi huo umetoa fursa za ajira kwa wenyeji ikiwemo Mama lishe, kukuza uchumi wa wakazi wa Katesh pamoja na kuimarisha mahusiano na wakazi wa maeneo hayo pamoja na uboreshwaji wa miundombinu ya barabara, maji na umeme katika maeneo ya mradi.

Desemba 3, 2023 Wilaya ya Hanang’ ilikubwa na maafa yaliyosababishwa na maporomoko ya tope, miti na mawe yaliyosababisha vifo vya zaidi ya watu 80 huku mamia wakiachwa bila makazi.

Serikali imeratibu masuala yote ya menejimenti ya maafa ikiwa ni pamoja na hatua ya kurejesha hali ambako kwa sasa zinajengwa nyumba 108 za waathirika wa maafa hayo, huku 73 zikijengwa na serikali kupitia SUMAJKT na 35 zikijengwa na Chama cha Msalaba Mwenkundu, ili kurejesha makazi kwa wananchi hao.