Yanga bado pointi nane kuwa bingwa

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 08:54 AM May 06 2024
news
Picha: Yanga
Stephane Aziz Ki, akimpongeza Joseph Guede kwa kumbeba na kushangilia pamoja baada ya kuifungia Yanga bao pekee wakati ikishinda 1-0 dhidi ya Mashujaa FC kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara iliyopigwa Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma jana.

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, sasa wanahitaji pointi nane tu kuweza kutwaa ubingwa kwa mara ya tatu mfululizo, baada ya jana kupata ushindi mgumu wa bao 1-0 dhidi ya Mashujaa FC, mechi ikipigwa Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma.

Alikuwa ni straika raia wa Ivory Coast, Joseph Guede, aliyesajiliwa kipindi cha dirisha dogo la usajili aliyepachika bao pekee katika mechi hiyo ya raundi ya 25.

Guede alisajiliwa kutoka Klabu ya Tuzlaspor ya Uturuki, alifunga bao hilo akimalizia kazi nzuri iliyofanywa na Mudathir Yahya na kutimiza bao la sita kwenye orodha ya wafungaji.

Lilianzia kwa Stephane Aziz Ki, aliyeupata mpira kwenye wingi ya kulia, akawahadaa mabeki wa Mashujaa waliokuwa wanamfuata, akausogeza mpira mbele kwa Mudathir aliyekuwa karibu na mstari wa mwisho wa uwanja, alichofanya ni kugeuka na kumtazama Guede ambaye alikuwa hajakabwa na mtu yeyote, akapiga krosi ya kuurudisha mpira ndani, mfungaji kazi ikawa rahisi tu ya kuudokoa, mpira ukajaa wavuni.

Ushindi huo unaifanya Yanga kufikisha pointi 65, ikibakisha mechi tano tu kabla ya kumaliza msimu, lakini ikihitaji pointi nane ili kufikisha pointi 73 ambazo hazitoweza kufikiwa na timu yoyote.

Katika mechi tano ilizobakiza nazo, inahitaji kushinda mechi tatu, au kupata ushindi mechi mbili na sare mbili.

Takwimu zinaonyesha kuwa iwapo Azam FC iliyo nafasi ya pili itashinda mechi zake sita ilizosaliwa nazo itafikisha pointi 72, huku Simba iliyo nafasi ya tatu kama ikishinda michezo yake saba iliyobaki nayo, itafikisha pointi 71 tu.

Mchezo wa jana ulianza kwa Mashujaa 'kupaki basi', huku wakiwaruhusu wachezaji wa Yanga kuwa na mpira muda mwingi wa mchezo na wao kutaka kushambulia kwa kushtukiza, kitu ambacho hata hivyo hakikuwezekana katika kipindi cha kwanza.

Ilipofikia dakika ya 25, Mashujaa walionekana kubadilisha mfumo na kuanza kuondoka langoni mwao, wakiamua kuwabana Yanga kwenye eneo lao, na papo hapo wote walirudi nyuma walipokuwa wakishambuliwa.

Mifumo yote miwili haikufanikiwa kwani, ilifanya shambulizi moja tu kwa dakika zote 45, wakati Adam Adam alipoingia ndani ya eneo la hatari dakika ya 29, akitokea wingi ya kushoto, lakini alijikanyanga mwenyewe badala ya kufanya maamuzi, mabeki wa Yanga wakauchukua mpira kiulaini.

Mudathir kama angekuwa makini, angeweza kuipatia Yanga mabao mawili, dakika ya 24, na 28, lakini mara zote alikosa utulivu na maamuzi sahihi ya kuweka mpira ndani ya nyavu.

Faulo iliyopigwa na Aziz Ki, dakika ya 30 nusura iende moja kwa moja wavuni kama Omari Kindamba asingepiga kichwa mpira ambao ulitoka juu ya lango na kuwa kona.

Faulo hiyo ilitokana na Yao Kouassi kuangushwa pembeni mwa uwanja, ndani kidogo ya kibendera cha wingi ya kulia.

Kipindi cha pili baada ya timu zote kufanya mabadiliko, Mashujaa ilionekana kutawala zaidi, ambapo walifunguka na kucheza mchezo wa kujiachia na kama wachezaji wake wangekuwa makini wangeweza kusawazisha au kupata ushindi.

Alikuwa ni Emmanuel Mtumbuka dakika ya 60, aliyeingia ndani ya eneo la hatari la Yanga na kutazamana ana kwa ana na kipa Djigui Diarra, lakini badala ya kupiga kwa maarifa, alipiga mpira kwa nguvu ukapaa juu la lango.

Dakika mbili baadaye, Zuberi Dabi aliupata mpira uliokuwa umeokolewa ovyo na mabeki wa Yanga, lakini shuti lake lilipita pembeni kidogo ya lango.

Mashujaa ilihamia kwenye lango la Yanga, dakika 15 za mwisho, na nusura isawazishe, pale Juma Nyenyezi alipoupata mpira akiwa nje ya eneo la hatari nakuachia shuti kali la juu lililompita kipa Diarra, lakini badala ya kujaa wavuni uligonga mwamba wa juu na kutoka nje.

Matokeo hayo yanaifanya Mashujaa kuendelea kuwa nafasi mbaya ya 14, ikiwa na pointi 23, ikicheza michezo 25.