HUKU ikiendelea kuhaha kubaki Ligi Kuu Zanzibar kwa kumaliza nafasi za juu msimu huu, timu ya Jamburi imesema mpango wao huo utaimarishwa zaidi kwa kuwa wanaamini katika michezo 10 iliyosalia iwatoa walipo kwa sasa.
Akizungumza na gazeti hili jana Kocha Msaidizi wa timu ya Jamhuri, Mfaume Shaaban, alisema wanasuka mipango imara ili kuhakikisha wanacheza tena Ligi Kuu msimu ujao.
Jamhuri ambayo makazi yake yapo Wete Pemba, ni miongoni mwa timu ambazo zipo katika mstari wa hatari wa kushuka daraja katika msimamo wa Ligi Kuu Zanzinibar wenye timu 16, ligi ambayo inadhaminiwa na Benki ya Watu wa Zanzibar, PBZ.
Kocha huyo alisema hesabu na mipango yao wanaielekeza katika michezo 10 iliyobaki kwa kuhakikisha wanapata alama za kuwaondoa katika hatari ya kushuka daraja.
Alisema timu hiyo licha ya kuvunja mazoezi kupisha mwezi wa Ramadhani, hiyo haitawazui kutimiza lengo na mikakati yao ushindi katika michezo iliyosalia.
Alisema miongoni mwa mpango mkubwa ni kuhakikisha hawapotezi kwa kufungwa katika michezo yote watakayocheza ugenini (Unguja), lakini pia kupata alama tatu kwa michezo yote watakayocheza nyumbani Kisiwani Pemba.
“Michezo mitatu ya mwanzo kati ya kumi, tunataka kuhakikisha tunashinda ili kututoa katika nafasi ambayo tupo na hii itatupa nguvu ya kuvuta pumzi na kujua tunahitaji alama ngapi ili kujihakikishia kama hatutoshuka daraja,” alisema.
Aidha, alisema timu hiyo inatarajia kuanza mazoezi mapema mwezi Eid pili, ili kuajiandaa na michezo 10 ya lala salama katika ligi hiyo ambayo inatarajiwa kuongezeka ushindani.
Timu ya Jamhuri ipo nafasi ya 15 katika msimamo wa Ligi Kuu Zanzibar ikiwa na alama 18, baada ya kushuka dimbani mara 20, ambapo imeshinda michezo minne, sare sita na kupoteza mechi 10.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED