Gamondi: Si kila mechi tutapata mabao mengi

By Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 10:05 AM Oct 01 2024
Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi
Picha:Mtandao
Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi

BAADA ya juzi kushuhudia timu yake ikiibuka na ushindi wa bao 1-0 na kujikusanya pointi tatu, Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi, amesema hatarajii kuona kila mechi wanapata ushindi wa mabao mengi, lakini kwake muhimu ni pointi tatu.

Kauli ya Gamondi imekuja baada ya baadhi ya mashabiki kuanza kuzungumzia ushindi mdogo wa bao 1-0 walioupata kwenye michezo yao miwili iliyopita ya Ligi Kuu.

Juzi usiku Yanga ilishinda bao hilo moja pekee kwenye mchezo dhidi ya KMC, lakini huo ulitanguliwa na mchezo dhidi ya KenGold FC ambao nao walipata ushindi kama huo na kuanza kuibua maneno kutokana na kawaida ya timu hiyo kupata ushindi mkubwa kwenye michezo yake.

"Sio kila mchezo utapata idadi kubwa ya magoli, ni lazima tucheze kwa kufikiria zaidi pointi tatu, KMC wamecheza vizuri sana, hatujapata mabao mengi lakini nafurahi tumepata pointi tatu, hili ndio jambo la muhimu zaidi," alisema Gamondi.

Alisema kila timu imejiandaa kufanya vizuri na ndio sababu wanapambana uwanjani.

"Itakapotokea kuna nafasi ya kufunga mabao mengi tutakuwa tukifanya hivyo, lakini muhimu sana kupata pointi tatu, hatujafunga mabao mengi kwenye mechi mbili, lakini tumepata pointi zote kwenye kila mchezo," alisema.

Katika mchezo wa juzi usiku uliochezwa Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, KMC walijitahidi kuwabana Yanga lakini hata hivyo hawakuwazuia kuondoka na pointi zote tatu.

"KMC wamecheza vizuri sana, walikuwa wengi nyuma ya mpira na hata wakipoteza wanarudi wengi golini kwao, wamecheza vizuri na nawapongeza," alisema Gamondi.

Kwa upande wake, Kocha wa KMC, Abdihamid Moalin, aliwapongeza wachezaji wake kwa kufuata maelekezo yake licha ya kuruhusu bao moja lililowapa ushindi Yanga.

"Sio kazi nyepesi kucheza na timu bora kama Yanga ukawabana kwa namna tulivyofanya, wachezaji wangu wamejitahidi sana lakini kosa moja tu limewapa nafasi Yanga kupata bao, tunaenda kujipanga kwa ajili ya mchezo ujao," alisema Moalin.

Ushindi huo unaifanya Yanga kufikisha pointi tisa katika michezo mitatu ya Ligi Kuu iliyocheza na kushika nafasi ya nne kwenye msimamo.