Gamondi avalia njuga janga la mabao Yanga

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 09:39 AM Sep 17 2024
KOCHA Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi
Picha:Mtandao
KOCHA Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi

KOCHA Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, amesema kazi aliyokuwa nayo kuelekea mechi ijayo ya marudiano ya hatua ya kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya CBE ya Ethiopia, ni tatizo la kukosa mabao linaloikabili timu yake kwa sasa.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, kocha huyo alisema kuelekea mchezo ujao atalifanyia kazi tatizo hilo ili lisijirudie tena kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, Jumamosi ijayo.

Gamondi alitoa sababu ambazo anaamini huenda zilisababisha hilo, lakini hataki liendelee kwa vijana wake.

"Nahitaji kukaa nao na kuwaweka kwenye mtazamo na umakini ule ambao tumeuzoea, hii ya kukosa mabao nadhani imetokana na kutokuwa fiti pamoja na umakini. Sikuwa na wachezaji 14 ambao walikuwa kwenye vikosi vya timu za taifa, kitu ambacho kimesababisha wengi wasiwe kwenye viwango vya kawaida na umakini na hii huwa linatokea sana wachezaji wanapokwenda kwenye timu za taifa," alisema.

Alisema katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Abebe Bikila, Ethiopia, walikosa jumla ya mabao saba ambayo kama wangeshinda wangekuwa wameimaliza mechi ugenini.

"Sijafurahishwa na kiwango kwa sababu tumepoteza nafasi nyingi sana, tulikuwa tuimalize mechi kule kule kama tungepata nafasi zile kwa hiyo, ni lazima nilifanyie kazi kabla ya kukutana na CBE Jumamosi kwenye mchezo wa marudiano, nahitaji tutumie nafasi kadri zinavyopatikana," alisema kocha huyo.

Akizungumzia mchezo wa marudiano, alisema hautokuwa rahisi kama ambavyo wengi wanavyodhani, lakini akawataka mashabiki wa Yanga kufurika uwanjani kwani amewaandalia mambo mazuri.

Katika mchezo wa Jumamosi Yanga ilishinda bao 1-0, lililofungwa na straika raia wa Zimbabwe, ambaye amekuwa akilaumiwa kwa kukosa mabao mengi katika mchezo huo.

Yanga inahitaji ushindi au sare yoyote ili kuweza kutinga hatua ya makundi kwa mara ya pili mfululizo, ambapo msimu uliopita ilifanya hivyo na kuishia hatua ya robo fainali.