Fei Toto: Samatta bado muhimu sana Taifa Stars

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 07:57 AM Sep 14 2024
Mbwana Samatta
Picha:Mtandao
Mbwana Samatta

KIUNGO mshambuliaji wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Feisal Salum 'Feitoto' amesema kuwa mshambuliaji Mbwana Samatta aliyetangaza kupumzika kuichezea timu hiyo bado anahitajika na muhimu kwenye kikosi chao.

Akizungumza juzi baada ya kurejea nchini akitokea Ivory Coast, ambako Stars ilicheza mchezo wa pili wa Kundi H dhidi ya Guinea, kusaka tiketi ya kucheza fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazofanyika mwakani nchini Morocco, Fei Toto, alisema hawezi kuingilia mawazo ya mtu au maoni yake, lakini Samatta bado anahitajika kwenye kikosi hicho kwani angewasaidia kwenye harakati za kusaka tiketi, lakini pia ni kiongozi mzuri nje na ndani ya uwanja.

"Huwezi kuingilia mawazo au maoni ya mtu, inawezekana mwenyewe kakaa na watu wake wamemshauri hivyo, lakini pamoja na hayo bado naona anahitajika sana,  sisi pia tunamhitaji kwenye kikosi chetu kwa sababu ni mchezaji mzuri na amekuwa na mchango mkubwa kwenye kikosi cha Taifa Stars, ni nahodha wetu na wachezaji tunampenda, amekuwa akituongoza vizuri ndani na nje ya uwanja, ila sasa sujui mwenyewe kama anaweza kubadili au kuendelea na msimamo wake, huwezi kumuingilia," alisema Fei Toto.

Akizungumzia ushindi wa mchezo wa ugenini dhidi ya Guinea, alisema baada ya sare dhidi ya Ethiopia walikaa wao wachezaji na benchi la ufundi na kuamua kwenda kusaka ushindi ugenini kwa udi na uvumba na kweli wakafanikiwa.

Kuhusu Stars kutoshinda nyumbani na kufanya vyema ugenini, Fei Toto alisema huwa inatokea tu na wala siyo kwamba wanapanga au kuna kitu ndani yake.

"Mpira una matokeo matatu, kushinda, sare na kufungwa, sisi kila mchezo tunataka kushinda, huwa inatokea tu kushinda ugenini na nyumbani kushindwa," alisema mchezaji huyo.

Alisema kwa sasa akili zao wanazielekeza kwenye maandalizi kujiandaa na michezo miwili dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo itakayochezwa Oktoba 7 nchini DR Congo na Oktoba 15, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Stars inashika nafasi yapilikwenye msimamo wa kundi lao baada ya kukusanya pointi nne katika michezo miwili wakifuatiwa na Ethiopia wenye pointi moja huku Guinea wakiburuza mkia kwa kutokuwa na pointi.

Congo inaongoza kundi hilo kwa kuwa na pointi sita huku kila timu ikiwa imecheza michezo miwili.