Bodi ya Ligi yaijadili Yanga kuhamia KMC

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 09:42 AM Nov 12 2024
 Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.
Picha: Mtandao
Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.

BODI ya Ligi imesema imepokea barua ya klabu ya Yanga inayoomba kuhama kutoka, Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, na kuhamia, KMC Complex kwa sasa wapo kwenye mchakato na kutazama sababu pamoja na kanuni ili kutoa uamuzi.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi hiyo, Almasi Kasongo, alisema kuwa barua hiyo ilipokelewa juzi na sasa iko kwenye mchakato na siku si nyingi watatoa maamuzi ya kuwakubalia ama vinginevyo.

Klabu ya Yanga juzi ilitangaza kuhama Uwanja wa Azam Complex na kuhamia KMC Complex, katika michezo yao ya Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na Kombe la FA ambalo bado halijaanza.

"Tumepokea barua ya Yanga kutaka kucheza Uwanja wa KMC Complex, nadhani leo (Jumatatu) siku ya kazi, vijana wataanza kazi ya kuichakata, baada ya hapo tutakuwa na nafasi nzuri na kutangaza maamuzi ya Bodi.

Barua inaeleza makusudio yao ya kuhama kutoka Uwanja wa azam Complex kwenda KMC Complex, Mwenge, wameeleza sababu zao lakini zinabaki kuwa siri yetu baina ya klabu na Bodi na wamiliki wa uwanja wa Azam,

Sababu zinafikirisha, zina mashiko au hazina mashiko, hayo yote yapo kwenye mchakato, sisi tunautazama mpira zaidi, Bodi ni chombo cha klabu zote kwa hiyo kipo kwa maslahi yao kama chombo chao, tunakaa kujiridhisha," alisema.

Hata hivyo alisema yote hayo ni lazima yawe kwenye kanuni, hivyo pia watakaza kanuni zinasemaje, lakini bila kuacha maslahi ya kimpira.

Baada ya kuchapwa mabao 3-1 dhidi ya Tabora United Alhamisi iliyopita kwenye uwanja huo ikiwa ni siku chache tu tangu kupokea kipigo kingine cha bao 1-0 dhidi ya Azam FC, tetesi zilianza kusikika kuwa viongozi walikuwa na mpango wa kutaka kuhama kwenye uwanja huo.

Juzi klabu hiyo ilitoa taarifa yake rasmi kupitia Ofisi ya Mtendaji Mkuu kuwa timu hiyo ikielezea kuhamia Uwanja wa KMC.

Hata hivyo uwanja huo kwa sasa unatumiwa na timu ya Simba na KMC kama viwanja vya nyumbani hivyo kama Yanga itakubaliwa, basi ni wazi kuwa ratiba ya Ligi Kuu Tanzania Bara itabadilika, hasa tarehe ambazo timu hizo zilitakiwa kucheza kwa siku moja kwenye viwanja vya nyumbani.