BAADA ya kulazimishwa suluhu juzi dhidi ya Mashujaa FC kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma, klabu ya Azam FC imesema wanachokutana nacho sasa ni mapito tu na muda si mrefu watarejea kwenye kiwango chao na kuanza kupata matokeo mazuri.
Akizungumza baada ya mchezo huo wa juzi, ofisa habari wa klabu hiyo, Hasheem Ibwe, alisema Mashujaa waliingia kwa nguvu kwenye mchezo huo hasa baada ya kumbukumbu ya kipigo cha mabao 3-0 ilichokipata kwenye uwanja huo msimu uliopita.
Azam haijapata ushindi kwenye michezo miwili ya Ligi Kuu, ambapo Alhamisi iliyopita ilishindiliwa mabao 2-0 dhidi ya Simba katika mchezo uliopigwa, Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
"Ni suala la muda tu timu yetu itarudi kwenye kiwango chake, unakumbuka kuwa msimu uliopita tuliwafunga hawa Mashujaa mabao 3-0 hapa hapa, leo walijua nini kingeweza kuwatokea, wakajipanga vizuri na kupata suluhu, na mmeona baada ya mechi walivyokuwa wakishangilia, kama wamepata ushindi, tunajipanga katika mechi ijayo," alisema.
Alibainisha kuwa hakuna kiongozi yeyote wa Azam aliyehuzunika kutokana na matokeo hayo kwani wanajua ni ya kawaida, huku akisema lengo lao la kusaka ubingwa au kusaka nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao ipo pale pale.
Kocha Mkuu wa Mashujaa, Mohamed Abdallah 'Bares' aliwamwagia sifa wachezaji wake, ingawa alisema kwenye kikosi chake kuna tatizo la kukosa mabao.
"Haikuwa mechi rahisi, niwapongeze vijana wamefanya kazi nzuri licha ya kwamba hatukupata ushindi, tumepata pointi moja inabidi tu tushukuru Mungu, kikubwa tu niseme timu yangu bado ina tatizo la kutotumia nafasi, kwenye mchezo huu tumepata nafasi chache, lakini vilevile tumeshindwa kuzitumia, tungefanya hivyo tungeibuka na ushindi," alisema Bares.
Matokeo ya mechi hiyo yameifanya Azam kushuka kutoka nafasi ya nne hadi nafasi ya tano ikiwa na pointi tisa, ikicheza michezo sita, Mashujaa pamoja na suluhu imeshuka kutoka nafasi ya tano hadi ya sita, pia ikiwa na pointi tisa.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED