Azam FC warejea kisaikolojia kuivaa JKT

By Shufaa Lyimo , Nipashe
Published at 07:09 AM Aug 28 2024
Azam FC.
Picha: Mtandao
Azam FC.

LICHA ya kueleza kwamba wachezaji wake walivurugwa kisaikolojia baada ya kutolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na APR ya Rwanda, Kocha Mkuu wa Azam FC, Bruno Ferry, amesema hali kwa sasa si mbaya na wapo tayari kuivaa JKT Tanzania kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara leo.

JKT Tanzania itaikaribisha Azam FC katika mechi ya Ligi Kuu Bara, itakayopigwa majira ya saa 10 jioni kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo uliopo Mbweni, Dar es Salaam.

Azam itashuka dimbani ikiwa imetoka kutolewa kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na APR kwa jumla ya mabao 2-1 baada ya wiki iliyopita Wanyarwanda hao kupindua matokeo ya kuchapwa bao 1-0  Dar es Salaam kwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.

Kuelekea mchezo huo, jana Kocha Mkuu wa Azam FC, Ferry alisema baada ya kutolewa kwenye mashindano hayo saikolojia za wachezaji zilivurugika kwa kiasi kikubwa. 

"Baada ya kuondolewa kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa wachezaji wangu hawakuwa vizuri kisaikolojia, nilikaa na kuzungumza nao ili niwaweke sawa kwa ajili ya kujipanga na michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara," alisema Ferry. 

Alisema kwa sasa wako sawa na wanaelekeza nguvu zao kwenye mashindano ya Ligi Kuu Tanzania Bara wakianzia na mchezo wa leo. 

Aidha, Ferry alisema wachezaji ambao hawakuwapo kwa kipindi kirefu kutokana na kuwa majeruhi, bado wataendelea kukosekana mpaka hapo watakapokuwa sawa kiafya. 

Naye mchezaji wa timu hiyo,  Hamis Yassin, ambaye alizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake, alisema baada ya kuotolewa na APR hawakuwa sawa kwani hawakuyatarajia matokeo waliyoyapata, lakini sasa wapo tayari kwa Ligi Kuu. 

"Mchezo huo utakuwa mgumu na wenye upinzani mkubwa kutokana na aina ya timu tunayokwenda kukutana nayo, yaliyotokea yamepita tunaelekeza nguvu zetu katika mchezo huo," alisema Yasini. 

Kwa upande wa Ofisa Habari wa Azam FC, Thabit Zakaria 'Zaka Zakazi alisema wamejipanga vizuri na kudai bado wataendelea kuwapo na kocha wao mkuu. 

Kocha Mkuu wa JKT Tanzania, Hamad Ally, alisema wataingia kwa tahadhari katika mchezo huo kwa kuwa wanakutana na timu ambayo ina ubora mkubwa. 

"Tunafahamu Azam FC ni timu nzuri, hivyo tutaingia kwa tahadhari kubwa kwa kutambua wamekamilika idara zote ili tuweze kupata pointi tatu," alisema Ally. 

Hassan Dilunga ambaye alizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake wa JKT Tanzania, alisema wamejipanga vizuri licha ya kutarajia mchezo huo kuwa mgumu na wenye upinzani mkubwa. 

"Tunafahamu mchezo utakuwa mgumu lakini tutapambana kuhakikisha tunapata ushindi kwenye uwanja wetu wa nyumbani," alisema Dilunga.