Simba na bajeti ya bilioni 28/- 2024-25

By Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 07:17 AM Oct 07 2024
Mwekezaji na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Mohamed 'Mo' Dewji, akiwa na viongozi mbalimbali wa klabu hiyo, akiwasalia wananachama wakati wa Mkutano Mkuu wa Mwaka uliofanyika jijini Dar es Salaam jana.
PICHA:MPIGAPICHA WETU
Mwekezaji na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Mohamed 'Mo' Dewji, akiwa na viongozi mbalimbali wa klabu hiyo, akiwasalia wananachama wakati wa Mkutano Mkuu wa Mwaka uliofanyika jijini Dar es Salaam jana.

KLABU ya Simba imepanga kutumia kiasi cha shilingi bilioni 28.4 kwa ajili ya msimu huu wa 2024-25, huku Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa klabu hiyo, Mohamed 'Mo' Dewji akiahidi makubwa zaidi.

Simba jana walifanya Mkutano Mkuu wa Wanachama jijini Dar es Salaam ambapo pamoja na yote walijadili taarifa ya fedha msimu uliopita na kupitisha bajeti ya msimu wa 2024-25.

Akitoa taarifa hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Fedha wa klabu hiyo, Suleiman Kaumbu, alisema msimu huu wanatarajia kutumia zaidi ya shilingi bilioni 28 kwa ajili ya matumizi mbalimbali.

Suleiman alisema fedha hizo wanatarajia kukusanya kupitia vyanzo mbalimbali vya mapato ikiwamo viingilio vya uwanjani ambapo malengo yao ni kukusanya zaidi ya shilingi bilioni moja katika mechi za ligi na mashindano ya kimataifa.

"Lakini pia tunatarajia kukusanya shilingi bilioni 3.3 kwa wadhamini Simba TV, kampuni ya Azam Media, tunatarajia kukusanya milioni 480 kama haki ya matangazo, lakini pia tunatarajia kukusanya shilingi milioni 500 kutoka kwenye jengo la klabu kama kodi," alisema Suleiman.

Aidha, akitaja vyanzo vingine, alisema wanatarajia kukusanya shilingi bilioni 1.4 kutoka kwa wanachama kama ada, shilingi bilioni 508 kama watafanikiwa kufika nusu fainali ya mashindano ya CAF, shilingi milioni 494 kwenye Tamasha la Simba Day na shilingi milioni 400 kutoka Simba App huku pia wakitarajia kukusanya zaidi ya shilingi milioni 500 kwa kuuza wachezaji.

Pia alisema wanatarajia kupata Shilingi bilioni 2.9 kutoka kwa mdhamini mkuu wa klabu hiyo, M-Bet, bilioni 1.5 kutoka kwa mdhamini wa jezi, milioni 155 mdhamini wa Ligi Kuu Benki ya NBC, milioni 500 Kampuni ya Serengeti, milioni 250 kutoka Kampuni ya A1 na shilingi milioni 250 kutoka vyanzo vingine.

Alisema fedha hizo zimeanza kutumika kwenye maeneo mbalimbali kama malipo ya mishahara kwa wachezaji, usajili, kulipa kodi mbalimbali za serikali, gharama za safari, gharama za ofisi, gharama za masoko na promosheni mbalimbali na gharama za kambi ya timu hiyo.

 Mo Dewji atoa bilioni saba

Akiwasilisha taarifa hiyo ya fedha mbele ya wanachama zaidi ya 700 walioudhuria mkutano huo, Suleiman alisema Mwekezaji wa klabu hiyo na Mwenyeiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Mohamed 'Mo' Dewji, tayari ametoa shilingi bilioni saba ambazo tayari zimeanza kutumika kwenye usajili wa klabu hiyo.

"Fedha hizi ziliwekwa kwenye akaunti ya klabu na sehemu zimetumika katika usajili wa wachezaji wapya kwenye kikosi chetu, tunamshukuru sana mwekezaji wetu," alisema Suleiman.

... Aahidi makubwa

Akizungumza kwenye Mkutano huo ulioanza saa 4:26 asubuhi, Mo Dewji, alisema bado ana maono makubwa na klabu hiyo kutwaa ubingwa wa Afrika siku moja.

Alisema amerudi tena kwenye nafasi yake ndani ya klabu hiyo ili kuongeza msukumo kwenye maono yake hayo.

"Tumesajili wachezai wapya 14 akiwamo [Elie] Mpanzu, lengo ni kuona Simba inacheza soka safi na kutwaa ubingwa wa Afrika siku moja, tuna imani kubwa na benchi letu la ufundi na kwa muda mfupi mabadiliko tumeanza kuyaona, tutaendelea kubuni mifumo mipya ili Simba iweze kurejea kwenye makali yake na kufanya vizuri," alisema Dewji.

Alisema hivi karibuni wataanza rasmi ujenzi wa majengo mbalimbali kwenye uwanja wao wa Mo Simba Arena ikiwa ni pamoja na kambi ya mazoezi, ujenzi wa hosteli, bwawa la kuogelea, ujenzi wa viwanja vitano, jengo la makumbusho ya klabu hiyo pamoja na kuanzisha akademi ya vijana.

"Tutafanya haya yote kwa sababu mchakato wa mabadiliko ya katiba upo ukingoni kabisa, tusingeweza kufanya hivi kwa sababu bado mchakato ulikuwa haujafikia mwisho, lakini kwa sasa tupo hatua nzuri na ujenzi huu utaanza hivi karibuni," alisema Mo.

 Akemea fitna klabuni

Mo Dewji amewataka wanachama wa klabu hiyo kuacha fitna kwa viongozi na badala yake kuungana kwa pamoja kuhakikisha wanaifikisha Simba kwenye malengo yao.

"Hatutaki fitna, tukaze kamba na tuwe kitu kimoja tusigawanyike ili tufikie malengo yetu, fitna inaondoa baraka ndani ya klabu yetu, na niwaambie watu, Simba si mnyama mkubwa zaidi, si mnyama mwenye mbio zaidi, lakini anabaki kuwa mfalme kutokana na ujasiri wake, tuoneshe ukubwa wetu ki vitendo, mimi nipo nanyi," alisema Dewji huku akishangiliwa na wanachama wa klabu hiyo.

 Jaji Mihayo ateuliwa Mjumbe Bodi ya Wadhamini

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa klabu hiyo, Murtaza Mangungu, mbele ya wanachama alipendekeza jina la Jaji Mstaafu, Thomas Mihayo, kuwa mjumbe wa bodi ya wadhamini ambapo wanachama wa klabu hiyo kwa kauli moja walimpitisha.