Wananchi wanahitaji kujua ukweli kuhusu tiba wanapoumwa na nyoka

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:17 AM Sep 24 2024
Wananchi wanahitaji kujua ukweli  kuhusu tiba wanapoumwa na nyoka
Picha: Mtandao
Wananchi wanahitaji kujua ukweli kuhusu tiba wanapoumwa na nyoka

MAJIRA ya kiangazi yanakaribia na wanaoishi karibu na vichaka na misitu ndiyo msimu wa nyoka kutoka mapangoni na kurandaranda.

Nyoka wapo na watu wanaumwa ndiyo maana, aghalabu ukisafiri kwenye mabasi ya masafa kuelekea au kutoka mikoani unakutana na wauza ‘mawe ya kuondoa sumu ya nyoka’.

Ni vipande vyeusi vya mawe ambavyo wengi wananunua bila kujua ni dawa au ni mazoea, hata hivyo, ni mambo yanayoachwa nyuma na sayansi ya kidijitali ya matibabu kwa walioumwa na nyoka.

Wafanyabiashara hao wanatangaza ndani ya vyombo vya usafiri kuwa ukiumwa na nyoka kwangua halafu bandika jiwe kunyonya sumu na ikimalizika litandoka.

 Unachotakiwa kufanya likianguka ni kuliloweka kwenye maziwa kulisafisha ukiendelea kulitunza kwa matumizi ya siku nyingine.

Aidha, wapo wanaosema ukigongwa na nyoka usipotumia jiwe hilo au  Shilingi 50 ama 100 kuondoa sumu mwilini, unaweza kupoteza maisha ikichukuliwa kama huduma ya kwanza.

Kadhalika, wataalamu hao wa mitaani wanasisitiza kuwa ni lazima kutoa meno ya nyoka yaliyobaki mwilini kwa kuchana na wembe au kisu kikali hata mkasi kuyakwangua na kuyaondoa. 

Wanaosema hayo wanaelekeza zoezi liwe la haraka kwani baadhi ya meno ya nyoka kama kifutu au kobra (koboko) yakibaki mwilini, ni hatari, husafiri kupitia mishipa ya damu na kufika moyoni maelezo ambayo pengine hayana ukweli.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), kuumwa na nyoka wenye sumu kunaweza kusababisha kupooza, kupumua kwa shida na wakati mwingine kukatwa kiungo iwapo sumu itaenea mwilini.

Mbali na hilo, kama sumu itasambaa  zaidi  na aliyeumwa asipata matibabu anaweza kupoteza maisha, kwa hiyo hatua zingine zinapaswa kuchukuliwa mara moja wakati unapoumwa na nyoka.

Lakini, WHO haizungumzii kubandika jiwe au kukwangua kidonda kama sehemu ya huduma ya kwanza.

Kwa mujibu waMamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA), nyoka hatari zaidi Tanzania ni koboko au cobra, ambaye akikuuma usipopata tiba haraka unaweza kupoteza maisha. 

Kobra huyo anayepatikana Tabora na ukanda wa magharibi kama Mwanza na Shinyanga, wapo pia kwenye misitu mingi ikiwamo ya Udzungwa.

Anaelezwa kuwa ana sumu kali inayoumiza moyo na nyingine mishipa ya fahamu na ndani ya dakika chache majeruhi anaweza kufariki dunia. 

Sasa cha kujiuliza aliyeumwa na mnyama huyu anaweza kutumia jiwe la nyoka na kupona?

CHA KUFANYA UKIUMWA

Shirika la Habari la BBC linafafanua mambo kadhaa ya kuzingatia, likisema jambo la kwanza usitembee wala kukimbia, kaa kimya na kutulia na ikiwezekana usinyanyue sehemu iliyogongwa iwe mkono au mguu.

Kwa ajili ya kuzuia kusambaza sumu kunakotokana na kukimbia au kutembea.

Aidha,  usafiri utumike kumpeleka majeruhi hospitalini na  kama ni kijijini abebwe bila kupoteza muda, ili kuokoa maisha yake.

Pia, majeruhi na anayemsaidia kumpa huduma ya kwanza wakae mbali na nyoka wasijaribu kumkamata.

Iwapo majeruhi umevaa saa, mkufu, vikuku, bangili au nguo ya kukubana eneo ulipoumwa na nyoka vivuliwe mara moja.

USIYOTAKIWA KUFANYA

BBC inaonya usiweke bandeji kwa nguvu wakati umeumwa na nyoka, hata kama imefungwa, ilegezwe kidogo.

Kumbuka kuwa kama bandeji imefungwa na kukazwa sana,  sumu inaweza kuenea kwenye jeraha na sehemu hiyo kukatwa kwasababu ya  ‘kuoza’.

Usiende kwa waganga wa kienyeji au kutumia dawa yoyote ya mitishamba au nyingine isiyojulikana kama umeumwa na nyoka, kwa hiyo aachana na mawe ya nyoka.

Usitumie kinywaji cha aina yoyote kwanza hadi utakapomuona daktari.

Aidha, madai kuwa kuua nyoka au kutumia barafu kunaondoa sumu, yote hayo sio ya kweli.

Wakati ukiumwa na nyoka mwenye sumu, matibabu sahihi ni muhimu ili kuokoa maisha ya majeruhi.

Katika hali nyingine, kifo au uharibifu wa kudumu wa kimwili unaweza kutokea ikiwa hautibiwi mara moja au kama aliyeumwa hatapata matibabu sahihi. 

Kwa hivyo usisikie au kutumia njia zingine za matibabu ya kuua nyoka, kuweka barafu kwenye jeraha au hata mbinu nyingine za kijadi zinazopendekezwa.

EPUKA HAYA

Usikwangue wala kunyonya sumu kutoka kwa mtu aliyeumwa na nyoka, ni hatari unaweza kuwa na vidonda mdomoni ukajiua kwa ‘kula’ sumu hiyo.

Lakini pia usiikwangue na kuichana ili kutoa meno sehemu iliyoumwa na nyoka.

Wakati wote kumbuka kuwa usiende kwa waganga wa kienyeji anza kwanza na dawa za hospitalini.

Usisafishe wala kupaka chochote kwenye sehemu iliyogongwa na nyoka.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani, watu wanaofanya kazi katika kilimo na watoto ni waathirika wakubwa wa nyoka.

 Watoto ndio walioathirika zaidi na sumu ya nyoka na kwa ujumla matukio hayo hupatikana duniani kote, lakini kiwango cha vifo katika visa kama hivyo ni kikubwa katika nchi za Kusini-Mashariki mwa Asia ikiwa ni pamoja na India.

Ripoti ya serikali ya India, inasema matukio ya kugongwa na nyoka ni ya kawaida zaidi katika vijiji na maeneo ya mijini. 

Aidha, inaeleza kuwa kuna aina zaidi ya 250 za nyoka nchini India, kati ya hizo nyoka 52 wana sumu kali wakiwamo kobra na nyoka wa baharini.