Wakulima waja nayo, wanataka wapatiwe mbunge wao

By Christina Haule , Nipashe
Published at 07:22 AM Oct 04 2024
Baadhi ya washiriki zaidi ya 900 wa Kongamano la Wakulima Wadogo na Mkutano Mkuu wa Mtandao wa Wakulima Wadogo Tanzania (MVIWATA), wakifuatilia mada.
Picha: Mtandao
Baadhi ya washiriki zaidi ya 900 wa Kongamano la Wakulima Wadogo na Mkutano Mkuu wa Mtandao wa Wakulima Wadogo Tanzania (MVIWATA), wakifuatilia mada.

WAKULIMA wadogo kutoka Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA), sasa wanaazimia kuitaka serikali iwawekee utaratibu wa kupata nafasi ya uwakilishi bungeni, ili wawe na mtu wa kuwasemea changamoto zao, wakidai ni kutokana na wawakilishi wanaowachagua kutotumia nafasi hizo kwa namna wanavyotaka.

Ni kauli yao wakulima kwenye kongamano la kitaifa la wakulima wadogo linaloenda sambamba na Mkutano Mkuu wa 29 wa MVIWATA, ambao Halima Helela, mmoja wa wakulima anasema ni vema serikali ikaweka utaratibu wa nafasi ya wakulima wadogo bungeni, ili nao wapate wa kuwasemea. 

“Ni kweli kuna uwakilishi wa wizara akiwamo Waziri wa Kilimo na wabunge kutoka kwenye kata zetu lakini hatuoni msaada wowote sababu bado tunakabiliwa na changamoto nyingi.  

“Tutaendelea kuitwa hatukopesheki hadi lini, benki zilizoko zinakopesha wakulima wakubwa na watu kutoka sekta zingine licha ya kuitwa ni benki ya wakulima...” analalamika Halima. 

Mkulima mwingine kutoka mkoani Kagera, Paulina Iseje, anasema wamekuwa wakikandamizwa katika mambo mbalimbali, yakiwamo kisera na sheria ya mbegu imekuwa inawakandamiza, kwa sababu bei ya mbegu imekuwa juu huku mbegu za kuzalishwa na mawakala wadogo (QDS) zikizuiliwa kuvushwa kutoka wilaya moja kwenda nyingine. 

“Mbegu za mahindi madukani huuzwa hadi shilingi 20,000 kwa mfuko wa kilogramu mbili huku mkulima akitengeneza kwa kufuata kanuni na taratibu zinazotakiwa na Taasisi ya kuthibiti Ubora wa Mbegu nchini (TOSCI).

 “Anaweza kuuza hadi shilingi 4,000 kwa mfuko kwa kilogramu mbili na Watanzania tumezoea kupeana, tunanyimwa uhuru wa kusaidiana, tushirikishwe katika sheria za mbegu,” anasema.

 Anasema, wakala wakubwa na wenye maduka makubwa ya uuzaji pembejeo za kilimo na mbegu, ni wataalamu wa mbegu na kwamba hali hiyo inasababisha mbegu kuuzwa bei ya juu siku hadi siku jambo linalowakosesha nafasi wao kama wakulima wadogo wenye uchumi wa chini kupata nafuu ya bei ya mbegu.

 WADAU MVIWATA 

Awali, Mwenyekiti wa MVIWATA, Apollo Chamwela amesema ipo haja kwa MVIWATA kuona umuhimu wa kutimiza malengo yake waliyoazimia tangu mwaka 2023 ya kuanzisha benki yao ya wakulima ili waweze kupata pa kukopea na kuanza kukua kiuchumi. 

Chamwela anasema, mchakato wa kuanzisha benki hiyo upo katika hatua za mwanzo, ambao wana imani utakuwa chachu ya kukua uchumi wa kilimo nchini na kuinua asilimia 75 ya Watanzania waliojikita kwenye shughuli za kilimo kwa manufaa ya taifa. 

Mwanachama wa Heshima wa MVIWATA, Bashiru Ally Kakurwa, anawapongeza wakulima kwa kuwa na maono yaliyo wazi, wakitaka mwakilishi bungeni wanayedhani anaweza kuwasaidia kuchambua changamoto zao kisera. 

Kakurwa, ambaye ni mbunge wa   kuteuliwa na  alishakuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), anasema suala la kuhitaji mwakilishi bungeni halihitaji marekebisho ya katiba kwa sasa, bali ifikie mahali vyama vinavyotafuta ridhaa ya wananchi kuingia bungeni, vijitafakari kuwa  ajenda zinazobeba kwa uzito maslahi ya wakulima.

 Anafafanua kuna aina za wabunge akiwataja; wa kuchaguliwa, kuteuliwa na viti maalum, toa mfanio wa baadhi ya vyama wamewagawa katika makundi yakiwamo viti maalum kwa wenye ulemavu, wafanyakazi, wa vyuo vikuu, wanaotoka mikoani kila mkoa kuwakilisha wanawake mikoani, na vijana.

 Kakurwa anasema, jambo hilo sio la kikatiba wala kisheria, hivyo wakati katiba inaangaliwa upya, wanaweza kuangalia suala hilo na kama wanaona linafaa, wasimamishe mwakilishi wa wakulima wadogo bungeni.

 “Kwa CCM upande wa wenye ulemavu viti maalum, naona inafanya kazi kubwa bungeni, yupo Keisha yule msanii, Hadija, haaaa likipita jambo pale hata kwa lugha tu ambayo sio sawa kwa wenye ulemavu atasimama kuomba mwongozo wa spika.

 “Likija suala la kibajeti au ya ajira, utamwona amesimama na unajua kabisa hapa ni engo ya watu wenye ulemavu, hata wafanyakazi yupo mbunge wa wafanyakazi toka CCM na vijana machachari pia wanaokuja na hoja kubwa, na makundi hayo yakiwakilishwa kuna thamani inaongezeka,” anasema.

 Hata hivyo, Kakurwa anasema hilo halitoshi kwa sababu uwakilishi haupo bungeni peke yake bali ujumbe huo unapaswa kuwafikia hata viongozi ngazi ya madiwani na Baraza la Wawakilishi Zanzibar na uwakilishi katika ngazi zote hadi vitongoji kwenye serikali za mitaa na vijiji, kuwa wakulima wanataka kusikilizwa na kutatuliwa changamoto zinazowakumba.

 Changamoto za wakulima sio kwamba hazitatuliki na hata kama hazitatuliki basi zizungumzike na kujadiliwa, kwa sababu ni hatua ya maana kuelekea kwenye kutafuta ufumbuzi na kuleta maridhiano.

 “Pale msimamo wa kiserikali wa kisera au kimaamuzi na msimamo wa wakulima wa uzoefu wao na maarifa yao vikipishana tusione kama jambo la kawaida, kwa sababu tukianza kuzoea kupishana katika mtazamo kijamii tutatengeza hali ya kutoaminiana,” anasema.

 “Na uongozi wowote usipoaminika, hauwezi kupata uhalali na pale ambapo hakuna uhalali wa kiuongozi wa watu kuridhia jamii hiyo haitawaliki,” anaendelea.

 Mkurugenzi wa MVIWATA, Steven Ruvuga, anasema kila kauli iheshimiwe na nguvu ya wengi ni kubwa zaidi, kuliko mtu mmoja.

 Anasema kuna mitazamo ya kichama kwa ujumla inayomtaka mbunge asimamie na isiwe maslahi ya kundi lake na bora kusimama katika nguvu ya wengi, itakayosaidia kundi lote kusikilizwa kwa pamoja.

 Ruvuga anasema, benki nyingi nchini zimechukua mifumo ya benki za nje na kuleta nchini, mara nyingi haziwezi kufanya kazi, kutokana na hali duni za wakulima nchini.

 Anasema, anatokana na kuwapo changamoto ya kuwahudumia wakulima kupitia mifumo ya benki, ambayo wamekuwa wakikopesha watu wengine badala ya wakulima.

 Kwa mujibu wa Ruvuga, katika kukabiliana na changamoto ya kuwahudumia wakulima kupitia mifumo ya kibenki MVIWATA, imefanikiwa kufanya kazi na Shirika linaitwa ADA na kufanya wakulima kupata mikopo ya shilingi milioni 200 hadi 300 kupitia vikundi vyao mbalimbali.

 Hivyo, anaishauri serikali kuangalia jinsi ya kutengeneza mifuko rafiki kwa kundi maalum la wakulima wadogo ili kukabiliana na changamoto zinazojitokeza.

 “Hata Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, aliona kuna changamoto ya mikopo ya asilimia 10 kwenye halmashauri ambapo fedha haziendi zinakotakiwa kwa walengwa, nasi kama tukitengeneza mifuko ikawa haiendi kunakohusika itakuwa ni yale yale.

 “Kama kutakuwa na mifuko itakayolenga na kuwafikia walengwa itasaidia sana kuongeza kila kinachotakiwa katika uzalishaji ikiwamo tija na uendelevu na ustahimilivu wa wakulima kwa kufidia pale bei za pembejeo zinavyopanda na kushuka,” anasema.

 Anafafanua kuwa, MVIWATA ina mikakati mbalimbali ikiwamo iliyoanzishwa tangu taasisi ianze mwaka 1993 ambayo ni kutambuliwa kama walivyo na kuheshimiwa, kiutu na hadhi yao.

 Ruvuga anasema, wakulima walikabiliwa na changamoto nyingi ikiwamo kutoheshimiwa na kuonekana kuwa ni watu wasio na uwezo wa kufikiri wala kuamua wenyewe jambo ambalo sio kweli.

 Anasema suala la kuangalia mfumo mzima wa chakula na uzalishaji uliojikita katika mfumo tegemezi unaopaswa kugeuzwa na kuwa mfumo wa kujitosheleza kwa ndani kwa kutumia kilimo ikolojia kwa kupokea na kuendeleza dhana ya uhuru wa chakula kwa kutumia rasilimali kuzalisha ambacho kitatumika ndani ya familia yake na taifa kwa ujumla.