RASASHA Amin Hamis na Ramra Tamad Abdullah ni wanafunzi wa kike wanaosoma katika Shule ya Sekondari Lumumba, iliyoko visiwani Unguja.
Wanafunzi hao mwaka huu wameibuka washindi wa jumla katika tuzo za Wanasayansi Chipukizi Tanzania (YST), baada ya kubuni mradi wa kutumia mbinu mbadala inayohifadhi mazingira na kuokoa ukataji wa misitu katika kilimo cha mwani.
Kwa mujibu wa wanafunzi hao watafiti, asilimia kubwa ya wakulima wa zao la mwani visiwani Zanzibar hukata miti hasa mikoko, ambayo wanatengenezea vijiti vinavyotumika kwenye kilimo hicho.
“Mradi wetu ulihusu utumiaji wa matumbawe katika kilimo cha mwani, ambayo tuliichagua kwa sababu kwa Tanzania hasa Zanzibar. Tuna watu wengi wanaojishughulisha na kilimo cha zao hilo, lakini namna wanavyokiendesha, wanahusisha ukataji wa misitu hasa mikoko ambavyo wanatengeneza vijiti ambavyo wanavitumia katika kilimo hicho cha Mwani,” anasema Ramra na kuiongeza:
“Licha ya kwamba tunaamini kuwa kilimo hicho cha mwani ni kizuri na muhimu, lakini kinachangia uharibifu wa misitu na mazingira hasa mikoko ambapo baada ya kutafiti tulibaini kwamba takribani misitu 400,000 inakatwa kila mwaka kwa ajili ya matumizi ya kilimo cha zao hilo.”
Anasimulia kwamba, kwa kubaini uharibifu huo wa mazingira, ndipo wakapata wazo la kuja na mradi unaonusuru mazingira na wakati huohuo, inakomboa kilimo.
“Tukafikiria kwamba miaka ijayo kama wakulima wa mwani wataendelea kukata mikoko namna hiyo, yote itapotea na hali huenda ikazidi kuwa mbaya zaidi kwa miaka 10 au 20 ijayo.
“Hivyo tukaona tutafute majibu au njia ambayo itakuwa mbadala wake kwamba badala ya kutumia au kukata mikoko kwa ajili ya kutengeneza hivyo vijiti, tukaona inawezekana kutumia Matumbawe,” anasema Ramra.
“Baada ya kupata hilo wazo, tulienda tukafanya utafiti wa Matumbawe, tukaona kwamba yenyewe yatasaidia katika matumizi ya kilimo hicho cha mwani, kwa sababu yanatoa virutubisho ambavyo vinahitajika katika upandaji zao hilo na tukabaini kwamba yenyewe ina uwezo wa kuruhusu viumbe vingine viishi kama samaki na viumbe wengine.
“Pia, tulibaini kwamba matumbawe pamoja na mwani yana uwezo wa kufyonza cabondioxide kwa hiyo tukaona itasaidia kupunguza kiwango cha hewa hiyo, tukaona ndio njia sahihi ya kutumia,” anaeleza.
Kadhalika, anataja kutumia Matumbawe, kupitia utafiti waliofanya katika vijiji vinne vinavyolima sana zao hilo la mwani, upo uwezekano wa kuvuna mwani mwingi zaidi na kwa muda mfupi tofauti na ilivyo kwa kutumia vijiti vya miti kama ambavyo wamekuwa wakifanya siku zote.
“Kwa hiyo njia yetu sisi ilihusisha utumiaji matumbawe katika kukuza mwani badala ya kutumia vijiti na kwa kuwa tulikuwa na miezi mitatu tu ya kufanya mradi, badala ya kutumia Matumbawe.
“Tulitumia mawe ambayo yana sifa sawa na hayo na hivyo tukagundua kwamba kwa kutumia mawe hayo. Mwani unaweza kukua kwa haraka na tukakuza pia samaki kwa wakati mmoja,” anasema Ramra.
Anaendelea: “Na kwa kutumia njia hiyo, tukatunza mazingira, tukavuna mwani mwingi na tukavuna pia samaki. Kwa hiyo, tunajikuta tunapata faida nyingi zaidi, tena kwa muda mfupi.
“Kwa hiyo endapo tungetumia njia wanayotumia wakulima kwa sasa, tungekata misitu tukaharibu mazingira, tunatumia muda mwingi mpaka kuvuna lakini hata wakati wa mavuno unapofika, tunavuna kidogo.
“Tukagundua kwamba njia ya kutumia matumbawe ni bora zaidi kwa sababu mbali na kutunza mazingira lakini faida za kiuchumi ni kubwa zaidi.”
USHAURI KWA KILIMO
Wanafunzi hao wanaishauri serikali iangalie namna ya kutoa elimu kwa wakulima wa zao hilo, ili watumie njia nzuri ya kulima ambayo haitaendelea kuharibu misitu na mazingira.
Wanasema endapo wakulima wataendelea kutumia njia hiyo ya kukata miti katika zao hilo la Mwani, hali ya mazingira itazidi kuwa mbaya na kwamba njia mbadala isiyoharibu mazingira, ndio itasaidia kuimarisha uchumi wa buluu.
“Kama sisi tumefanya utafiti na tukabaini kwamba kwa kutumia njia mbadala inawezekana tukaokoa misitu yetu, hatuoni haja ya kuendelea kulima kwa kukariri au mazoe kwa sababu ni hatari kwa vizazi vijavyo,” anasema Ramra.
Ikumbukwe kwamba, mashindano hayo ya YST, mwaka huu yamefanyika kwa mara ya 14 na hufanyika kila mwaka kwa kushirikisha wanafunzi wanasayansi kutoka katika shule mbalimbali za sekondari Tanzania Bara na Zanzibar.
YALIVYO MASHINDANO
Mashindano hayo ambayo huambatana na maonesho ya kazi za kibunifu za kisayansi, huanza kushindanisha kazi za kibunifu za kisayansi za wanafunzi hao kuanzia katika mikoa mbalimbali lakini pia huwa inafanyika fainali ambayo hushindanisha kazi bora zaidi ambazo hupatikana baada ya mchuJo kutoka katika maonyesho ya kazi hizo yanayofanyika mkoani.
Fainali za mashindano hayo kufanyika baada ya kupatikana kazi bora zaidi na miaka yote hiyo, yamekuwa yakihitimishwa jijini Dar es Salaam na mwaka huu imefanyika Septemba katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC), washindi katika makundi mbalimbali hupata tuzo za medali, fedha tasilimu pamoja na ufadhili wa masomo wa chuo kikuu.
Washindi wanne pekee ndio hubahatika kupata ufadhili wa masomo ya vyuo vikuu, wawili wakiwa washindi wa jumla na wawili wengine ni wale wanaobahatika kushinda katika kategoria maalumu ya Karimjee Jivanjee Foundation ambao ndio wadhamini wakuu wa mashindano hayo ya YST kwa miaka 14 mfululizo.
Washindi wengine kutoka katika kategoria mbalimbali hushinda medali pamoja na fedha tasilimu.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Bodi ya YST, Prof. Yunus Mgaya, washindi hao wa jumla walipatikana baada ya kufanyiwa mchujo ulioshirikisha kazi 1,055 kutoka kwa wanafunzi wa sekondari wa mikoa mbalimbali ya pande zote za muungano.
Prof. Mgaya anasema gunduzi za mwaka huu, zilijikita katika masuala mbalimbali, ikiwamo uhifadhi salama wa mazao ya kilimo, afya ya binadamu, mifumo ya umwagiliaji, utunzaji wa mazingira, upatikanaji wa nishati ya umeme, usalama wa chakula na utatuzi wa changamoto kidijitali.
Mwazilishi mwenza wa YST, Dk.Gozbert Kamugisha, anasema kupitia tuzo hizo, wameanza kuona tija yake hasa katika kutengeneza wabunifu na wanasayansi wengi nchini na pia kuwahamasisha wanafunzi kupendelea masomo ya sayansi.
Anasema baadhi ya wanafunzi waliowahi kupata tuzo tangu zianzishwe miaka 14 iliyopita, tayari wengine ni madaktari wazuri, wahandisi na wana-teknolojia wa kubuni mambo mbalimbali.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED