MWAKA huu kwa maombi yangu, napenda ukawe unakupa fursa ya kujipa nafasi ya kujali afya ya mwili na akili kwa umma.
Huwa tunasahau sana kupanga malengo ya kiafya, pindi tunapopanga malengo ya mwaka.
Afya imebeba hatima zetu nyingi za malengo tunayoyapanga. Ikitetereka kidogo tu, hakuna kinachoweza kwenda vizuri na wakati mwingine kudorora kwa afya kunaweza kumfanya mtu kuanguka hata kiuchumi, yeye binafsi na hata jamaa zake.
Afya ya akili inabeba tafsiri kubwa ya mtu ni afya. Msingi wake ni pindi inapoguswa, basi inaangukia mtu ameguswa namna anavyofikiri, kuhisi, kutenda kwake na ufanyaji wake wa maamuzi.
Afya ya akili inapokuwa duni, inaweza kuchangia utendaji wa mtu wa kawaida ushuke, akajiumiza au kuumiza watu wengine. Hivyo inapoguswa uzito wa afya ya akili ni kuonyesha kujali umuhimu wake mkubwa kwa ufanisi wa mtu na hatimaye wa jamii inayojenga taifa.
Mwaka uliopo katika mwezi wa kwanza, zikihesabika wiki kadhaa, ni muhimu tukajenga na kuyakumbuka haya maeneo matano nitakayoenda kuyazungumzia kuyapa kipaumbele kikubwa katika hatua ya mwanzo kabisa ya kulinda afya ya akili ya mtu mzima, kwa ujumla wake.
USISUBIRI KUELEMEWA
Watu wengi wanaingia katika changamoto zinazohusiana na afya ya akili, kwa kuogopa kuelezea yale wanayoyapitia.
Mtu anaweza kuwa anapitia mambo mengi yanayompa mawazo au msongo mkali wa mawazo, kiasi kwamba hata utendaji wake wa mambo ni dhahiri umeshuka, si mtu wa furaha, mtu mpweke na aliyejitenga.
Hatua hizo zote kutokea, huwa kwa dharura ya mara moja. Ni vile mtu kwa muda amekuwa akipambana mwenyewe kutatua mambo ambayo hajaweza kuyapatia majibu hata hivyo.
Tumepoteza baadhi ya watu, kwa wao wenyewe kuchukua uamuzi wa kujiumiza na hata wengine kujiua, kwa kushindwa kuzungumza na watu wa karibu.
Mwaka ulipo usisubiriwe mambo yakawa magumu na yamefikia hatua mbaya, kwani ukiwa katika hatua hiyo kushughulika kwa mambo huwa ni kugumu zaidi.
Wahi mapema kusema, kuzungumza mambo yakishaanza kuonyesha hayana majibu.
KUEPUKA UTUMIAJI VILEVI
Ni rahisi watu wengi wanapokuwa katika hali ngumu wapitiazo za msongo wa mawazo kukimbilia kutumia vilevi mfano pombe, ili kupoteza mawazo au kama njia ya kukabiliana na magumu wapitiayo.
Ubaya wa mtu aliye katika msongo mkubwa wa mawazo na vilevi ni kuwa na nafasi kubwa ya kutumia kiwango kikubwa zaidi kuliko kawaida yake.
Matumizi ya kupindukia yanaweza kuchangia zaidi matatizo kwa mtu kwa kumpa nafasi ya magonjwa ya matumizi ya vilevi, maisha kijamii kuwa na migogoro, uchumi kushuka.
Pia, ufanisi wa kazi kushuka na hata wengine kuingia katika hatari ya tabia hatarishi zinazoweza kuchangia kuingia katika ngono zembe, zinaongeza hatari ya maambukizi ya magonjwa ya zinaa, Virusi Vya Ukimwi au hata homa ya ini.
Wapo wanaotajwa kuingia kwenye vilevi kama majaribio, hususani kundi la vijana wadogo baada ya balehe.
Wengine ndio mwanya wa kujikuta tabia hiyo inakuwa endelevu na yenye kuleta madhara hapo baadaye.
Jitahidi kama unaweza kuacha, kutoingia au kuepuka matumizi yoyote ya vilevi maana hatari ya matumizi ya vilevi yaweza kuleta uraibu na uraibu wa tabia.
ANAYEWEZA KUZUNGUMZA APITIAYO
Maisha yanajumuisha watu wanaokuzunguka. Ni rahisi kwa wengine wanapopitia magumu wakajikuta wamejitenga kwa kupambana wakiwa peke yao, kuhusu magumu wapitiayo.
Huenda zipo sababu kadha wa kadha, zinazochangia watu wasipende kuzungumza magumu yao.
Moja ya sababu, niliwahi kuhoji katika semina niliyoendesha, mshiriki mmojawapo akawa na majibu:
“Tunaogopa kuzungumza yale tupitiayo, kwa sababu wengine baada ya kutusaidia wao wataanza kututangaza.”
Hapo inapatikana sababu za msingi kwa watu kuogopa kuzungumza. Ikiwa una mtu anayeminiwa, basi haipaswi kungoja mambo magumu kummaliza.
Cha muhimu kinachosisitizwa hapo ni kuchukuliwa hatua ya kuzungumza au kama hakuna imani, wapo wataalamu wa afya ya akili au viongozi wa kiroho wana nafasi yao.
Kwa ujumla wake, suala la kuzungumza linapunguza uchungu na mzigo mzito mtu anaobeba ndani yake.
MSAADA NI UDHAIFU?
Kuomba msaada pale unapokuwa na mambo mengi kichwani au moyoni, si ishara wewe ni dhaifu. La hasha! Ni kukubali jambo hilo mwenyewe umeshindwa kukabiliana nalo.
Kuhitaji msaada ni hatua ya kuonyesha ubinadamu wetu kuwa hatutaweza kuyatatua mambo yote sisi wenyewe.
Omba msaada unapoona huoni njia, huoni mwanga, huoni pa kutokea, umejaa uchungu, maumivu na hasira.
Omba msaada wakati wowote ambao unaona binafsi umefikia njiapanda. Omba msaada kwa kushirikisha kile unachopitia, ili watu wengine kama ni wataalamu au ni watu waweze kukusaidia kwa namna mbalimbali unavyoweza kutoka au kuvuka.
Usikomae mwenyewe kuonesha wewe ni jasiri sana na huombi msaada wakati mambo yako wazi umetingwa mno na njia mbele yako ina kiza kizito.
USIJITENGE, BALI JITAHIDI
Popote maishani inatajwa ni muhimu kuwa sehemu ya jamii inayozunguka. Hao ni watu wenye msaada unaotosha wakati wowote ule unapojikuta katika hali ngumu.
Lingine ni kujenga ushirikiano mzuri na watu kila sehemu iendayo, mtu akijichanganya nao, kujenga urafiki, kushiriki kazi mbalimbali za jamii na wanajamii waweze kuona mchango wako wowote ule.
Hilo limeonyeshwa katika utafiti, kuwapo watu wanaojichanganya na kuwa karibu na jamii, ni namna moja ya kujikuta wapo katika mfumo unaowalinda kupata msaada au kutambulika haraka zaidi pindi wanapokuwa wanapitia wakati mgumu na kupata msaada, mbali na
na wale wanaojitenga wakawa na maisha ya pekee, pasipo kuchangamana.
Nikikutakia heri ya mwaka 2025, ukawe na ya kuyakumbuka, ikiwa moja ya misingi ya kuilinda afya binafsi ya akili, yakiwa salama wakati wote.
Afya ya akili kwanza, ni msingi wa jamii salama, utendaji na isiyoona haya kuzungumza mambo yote yahusuyo afya ya akili.
Dk. Raymond Mgeni; ni mtaalamu wa afya na magonjwa ya akili. Kwa sasa anasoma stadi hiyo kwa ngazi ya ubingwa, katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Shirikishi Muhimbili (MUHAS). Anapatikana kwa simu: +255 676 559 211
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED