Vita vya mauaji, ubakaji, ulawiti wasiachiwe polisi pekee yao

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 12:17 PM Sep 06 2024
news
Mchoraji: Msamba
Vita vya mauaji, ubakaji, ulawiti wasiachiwe polisi pekee yao

KUMEKUWA na matukio mengi yasiyo ya kwaida nchini kwa siku za hivi karibuni ambayo yameonekana kuwashangaza wengi.

Matukio hayo ni kama utekaji, mauaji, ubakaji, ulawiti, ambapo kila kukicha inakuwa afadhali ya jana.

 Pamoja na vyombo vya habari kuandika na kufichua maovu hayo, ikitarajia kuwa na watu wataogopa, lakini ndiyo kwanza hali inazidi kuwa mbaya.

 Watu wametekwa na hawajulikani walipo, maiti na viungo vya binadamu kukutwa kwa waganga wa kienyeji, baba zima linalawiti na kunajisi watoto, hizi ni habari ambazo kama zinataka kuwa za kawaida hapa nchini.
 Cha ajabu ni kwamba hata hao wanaobaka, wengine wanafanya hivyo kwa watoto zao wa kuwazaa.

 Kusema kweli hali hii imekuwa ya kushangaza sana na haijulikani kuna kitu gani kimetokea kwa siku za hivi karibuni.

 Majuzi, Jeshi la Polisi Kanda Maalum lilikutana na waganga wa tiba mbadala na kuwaonya kuacha kufanya ramli chonganishi kwa wateja wao na kuacha kuwapa masharti wateja wao kuwa ili wafanikiwe wanatakiwa wajihusishe na vitendo vya ubakaji na ulawiti hasa kwa watoto.

 Kamanda wa Polisi kanda hiyo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP), Jumanne Muliro, aliwaonya kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya waganga hao wanaofanya ramli chonganishi na zenye madhara kwa wengine.

 Kwanza nitoe pongezi kwa Jeshi la Polisi kwa kuwa mstari wa mbele kutaka kutatua suala hilo. Hapa inaonyesha kuwa polisi haitaki tu kuwa na kazi ya kukamata watu wanaofanya tukio ili kuwapeleka mbele ya sheria kama ambayo kazi yao ilivyo, lakini wakaenda hatua nyingine mbele ya kutaka kuzuia matukio hayo yasijitokeze.

 Pamoja na hayo, kazi ya polisi haitokamilika kwa asilimia zote kama jamii nayo haitoisaidia ili kukabiliana au kumaliza tatizo hili.

 Niseme tu kuwa mambo haya yote yanaanzia ndani ya jamii yenyewe ambayo ndiyo inasababisha ya yakishatokea lawama inakuwa na vyombo vingine.

 Nadhani ifike wakati jamii ijiangalie kwa kile ambacho inakifanya. Inashangaza kuona karne hii ya 21, bado watu wanaamini uganga na ulozi, badala ya teknolojia, kufanya kazi kwa bidii na kuomba Mungu.
 Watu wengi kwa sasa wamesoma, lakini bado elimu yao imekuwa haiwasaidii kwani bado wanakuwa wanaamini njia za mkato za kupata kile wanachokitafuta.

 Binadamu wa sasa wanapenda kufanikiwa kwa njia ya mkato, kimiujiza, bila kutumia njia ambazo zinakubalika na kuelezeka, ambazo hata mtu akikuuliza mafanikio yametokana na nini unaweza kumtajia.

 Tumekuwa na kizazi ambacho hakitaki shida, hakitaki kuvumilia na kufanya kazi kwa bidii na kufanikiwa taratibu, badala yake kinachotaka kupata kazi kwa haraka, na mtu akiingia kazini miezi miwili tu awe na nyumba, gari na mshahara, mnono, akifanya biashara yake, faida iwe asimilia 300 ya mtaji wake, yaani mradi mafanikio ya haraka ndiyo wanayosababisha yote haya.

 Ifike wakati jamii irudi kwenye misingi ya kawaida ya kujua kuwa duniani hakuna kitu chochote rahisi kama tunavyodhani.

 Kuua mtu, kuchukua viungo, siyo dawa ya kupata mafanikio, utajiri, kazi, cheo, badala yake ni kupata laana kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

 Viongozi wa dini, jamii na wazazi turejee na kuanza kuwafundisha watoto wetu misingi ya maisha kama ilivyokuwa zamani ambapo pamoja na kwamba hakukuwa na elimu sana, walikuwa na imani na waliamini kufanya kazi kwa bidii kutumia vipaji na uwezo wao.

 Tiba asili walifanya kwa ajili ya kujitibia tu kwa magojwa na si kudhuru wengine au kuwapatia maisha mazuri kwa njia ya mkato.