Viongozi wasitumie Polisi kukabili wanaoongozwa

By Joseph kulangwa , Nipashe
Published at 07:26 AM Oct 04 2024
Katuni.
Mchoraji:Msamba
Katuni.

HEBU vaa viatu vya daktari aliyeko ofisini akisubiri kuonana na wateja wake, yaani wagonjwa. Ghafla uko ofisini anaingia mgonjwa, unamkaribisha anakaa, lakini anaonekana anaumwa sana unamhoji, anakwambia kweli anajisikia vibaya.

Unaingiwa shaka kwamba pengine anajifanya tu kwa sababu saikolojia yako ya udaktari inakuonyesha kabisa haumwi ila ana lake jambo. Bila shaka huwezi kumfukuza wala kumkaripia, ila utampima ili kujiridhisha.  

Kwa bahati mbaya matokeo yanasema haumwi chochote. We kama daktari na maadili yako, utakachofanya utampa pole na kumwambia ingawa vipimo havionyeshi chochote kibaya, pengine ni uchovu na anachotakiwa ni kurudi nyumbani apumzike na kunywa maji mengi hali itarejea kawaida. 

Kama alikuwa anakudanganya akitarajia pengine atapata dawa akauzie wenzake, atakuwa amegonga mwamba na kurudi nyumbani mikono mitupu, lakini amepoteza muda na nguvu zake kutembea hadi hospitalini kujaribu kuhadaa. 

Lakini kwa kuwa hana utaalamu, inawezekana pia bila shaka hali aliyokuwa anajisikia kuwa nayo, ilimfanya aamini kuwa anaumwa na hivyo kuamini kuwa matatizo yake yataishia hospitalini. Bahati mbaya kumbe haikuwa hivyo. 

Haya mambo hutokea miongoni mwetu na wakati mwingine kushindwa kuaminiana na kudhani watu wanajifanya na yakikutana na madaktari wasiojali taaluma yao, ndio mtasikia alizidiwa baada ya kurudi kutoka hospitalini akapoteza maisha. 

Kumbe daktari angekuwa makini hayo yasingemkuta mteja wake mpaka kupoteza maisha. Haya hutakuta pia katika maisha ya kawaida yasiyohusu magonjwa au ajali zingine zinazoweza kusababisha maafa katika jamii.

Ni hivi, Agosti mwaka huu mkoani Simiyu eneo la Lamadi wilayani Besega, wananchi waliandamana wakilalamikia upotevu wa watoto wakichukuliwa na watu wasiojulikana, wakielekea kituo cha Polisi kudai haki ya kusaidiwa. 

Wananchi hao walikuwa wakilalamikia viongozi wa serikali wakiwamo ngazi ya ulinzi na usalama, ambako wamekuwa wakiwasilisha malalamiko yao ya kupotelewa watoto, lakini mara zote hakuna kinachofanyika, hivyo kupuuzwa na wao kuona wamechoka sasa wakitaka kujiridhisha kulikoni. 

Lakini siku hiyo, polisi walikabiliana nao na kufyatua risasi iliyompata mmoja wa wananchi hao na kupoteza maisha, ni bahati mbaya sana kijana aliyepoteza maisha alikuwa ndiyo kwanza amemaliza kidato cha sita akijiandaa kujiunga na chuo kikuu.

 Baada ya mambo kutulia, mwezi mmoja baadaye, viongozi wanapita vijijini kusikiliza kero za wananchi, lakini kwa maajabu, linaibuka suala la waliolalamikia watoto kutoweka, wakitakiwa kutoa uthibitisho wa madai yao mkutanoni.

Mmoja wa wakazi anasimama na kudai kuna kutoweka kwa baadhi ya watu na wengine kuumizwa, mwingine akidai kuwapo matukio ya mabaya zaidi, watoto kutekwa au kupotea na mabaya zaidi, wananchi kuishi kwa shaka na kujifungia majumbani kila ifikapo saa 12 jioni. 

Pamoja na hayo, kadhia nyingine inayodaiwa kuwateka wakazi hao ni kasoro katika huduma nzuri ya kimatibabu katika baadhi ya maeneo, kukiripotiwa matukio dai la malipo kwa  watoto wasiostahili kufanyiwa hivyo.

 Kwani tayari ukiwa na kadi ya matibabu, hutakiwi kulipia, lakini unaweza kuiambulia dawa maumivu na zingine unajinunulia. 

Kitendo cha wananchi hao kulalamika, kinamsababisha Mkuu wa Mkoa, kuwataka wathibitishe madai yao chini ya usimamizi wa polisi, huku akionya dhidi ya kutoa alichokiita taarifa za uongo, hivyo watu hao kupandishwa gari l kwenda kuthibitisha. 

Kiongozi mkubwa anachukua kipaza sauti na kuhoji wananchi kama kweli kuna matukio hayo katika maeneo hayo na kujibiwa “hakunaaaa!” hata anapata nguvu ya kuwaweka chini ya ulinzi waliodai kuwapo matukio, hayo ili wakathibitishe. 

Hivi kiongozi alitarajia majibu gani mbele ya Jeshi la Polisi? Alitarajia nini wakati mwezi mmoja tu kupita aliuawa mtu akiandamana? Kwani angefanya kama daktari alipomshauri mgonjwa akanywe maji mengi kutokana na uchovu ingekuwaje? 

Kiongozi alichotakiwa kufanya ni kusikiliza malalamiko na baadaye angewaita kwa nafasi yake wananchi hao kuwahoji ofisini mwake, kwa utaratibu na pengine kama aligundua ni uongo basi 

wangemwambia kiini na angewaonya kuliko kuwakabidhi chini ya ulinzi. 

Siku nyingine, kwa utaratibu huo wananchi wanaweza hata kubaini wahalifu kijijini kwao au wakielekea kwa Mkuu wa Mkoa na kunyamaza 

kwani kusema kunaweza kuwasababisha waombwe uthibitisho.

Pia, kufanya hivi kutasababisha msuguano wa  kuchukua sheria mkononi kimyakimya, wakiepuka kubanwa na Polisi kuthibitisha. Wanahofu, wakigoma kutoa taarifa wasiambiwe wanaficha wahalifu!