Vijana, watoto zamani ‘walivyoinjoi’ Krismasi zao

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 09:49 AM Dec 21 2024
Vijana, watoto zamani   ‘walivyoinjoi’ Krismasi zao
Picha:Mtandao
Vijana, watoto zamani ‘walivyoinjoi’ Krismasi zao

JUMATANO ijayo, waumini wa Kikristo wote ulimwenguni wataungana na wenzao duniani kusherehekea sikukuu ya Krismasi, ambayo kwa jina lingine huitwa Noel.

Ni sikukuu inayosherehekewa Desemba 25 ya kila mwaka kuadhimisha kuzaliwa na Masiya, Yesu Kristo zaidi ya miaka 2000 iliyopita kwenye mji ya Bethlehemu, nchini Israel.

Hii ni moja ya sikukuu maarufu zaidi duniani, ambapo hapa nchini huwa tunaona wazazi wakiwa bize kuwanunuliwa mahitaji watoto wao na kuhakikisha wanakula vizuri, kabla ya kwenda Kanisani kumshukuru Mungu, lakini baada ya hapo hugawanyika, wakubwa wanakwenda sehemu zao kwa ajili ya kuburudika na kusherehekea, pia watoto nao huelekea sehemu zao ambazo nazo huzipenda kwenda na watoto wenzao.

Wakati wakubwa hupenda kwenda sehemu zenye vinywaji na nyama choma, na burudani ya muziki, watoto wa kizazi cha sasa hupenda kwenda sehemu kama vile baharini 'bichi', au maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya watoto kama vile kubembea, kuendesha farasi wa umeme na mengine mengi.

Haya ni kwa wazazi na watoto wa kisasa. Miaka ya nyuma, maandalizi ya sikukuu hii yalikuwa tofauti na sasa. Yalikuwa makubwa zaidi na yaliyochukua muda mrefu kuliko sasa. Yalikuwa na pilikapilika nyingi kuliko sasa kwa wazazi na watoto pia.

Siku hizi baba anaweza kupata pesa na kununulia watoto nguo wakati mwingine bila hata wao kujua. Wanashtukia zimeletwa tu.  Kutokana na teknolojia kuwa ndogo, uhaba bidhaa kama nguo, viatu na vitu vingine vilisababisha kuwe na pilikapilika za aina yake.

Kwanza kabisa watoto wa siku hizi wana nguo nyingi nzuri kiasi kwamba hata akinunuliwa mpya, zinakuwa hazina sana tofauti na alizonazo.

Zamani kwenye sikukuu kama hii picha linaanza kwanza kwenye redio. Hakukuwa na redio yoyote zaidi ya RTD, hivyo nyimbo za Krismasi zikianza kupigwa tangu tarehe 15, wote mtasikiliza na kila mtu atajua sikukuu inakuja, hivyo inaleta msisimko mno, tofauti na sasa ambapo kuna baadhi ya vituo ambavyo havilazimiki kupiga nyimbo hizo.

Pia watoto na vijana wa sasa si wasililizaji sana wa redio, zaidi ya televisheni na simu za mkononi ambapo husikiliza nyimbo wanazozitaka wao tu.

Kwa miaka ya karibuni hata miti halisi ya kupamba Krismasi haipo, badala yake ipo ya kutengenezwa ambayo si halisi. Hii imekuja kuua sana biashara ya miti halisi.

Siku chache kabla ya Krismasi, baba atawapeleka kwa fundi cherehani kupima suruali, au gauni, wakati huo tayari vitambaa vimeshanunuliwa hasa wale wa vijijini. Wengine hupelekwa mjini kununuliwa gauni, shati, suruali na viatu.

Wazazi wakati huo walilazimika kuwachukua watoto wao kwenda nao mjini kwa sababu ya kujaribu nguo na viatu kwani isingewezekana kurudisha au kuanza kuirekebisha kwa fundi.

Kulikuwa maduka maalum ya kununua nguo za si kwa machinga kama sasa, lakini viatu hasa vya sikukuu na shule vilikuwa vinanunuliwa kwenye kampuni ya viatu Bora.

Na kama mtoto hatochukuliwa kupelekwa mjini kukuliwa viatu, basi litachukuliwa katarasi ngumu au boksi, atalikanyaga, huku kalamu ikizungushwa kwa kuchorwa kuzunguka mguu, ili atakapoenda mjini basi viatu vitakachowekwa na kuwa sawa na mzunguko huo ulioko kwenye boksi au karatasi ngumu, vitakuwa vinamtosha mhusika na kweli ilikuwa hivyo.

Ilikuwa ni wiki ngumu kwa watoto wa zamani kuelekea kwenye sikukuu. Tena usiombee nguo zinunuliwe mapema. Ni kwamba kila mara atakuwa anakwenda kufungua sanduku na kuziangalia. Wakati mwingine atazijaribu na kuzirudisha akiombea sikukuu ifike upesi, avae akawaringishie wenzake ambao ana uhakika nao watakuwa na nguo mpya pia. Hapo sasa ni mashindano ya nani kapendeza zaidi ya mwingine.

Ukweli ni kwamba wazazi wa sasa wako karibu zaidi na familia zao hasa siku za sikukukuu mtu anaweza kutoka yeye mkewe na watoto, wakaenda popote pale kwa ajili ya kusherehekea, tofauti na zamani ambapo baba hakuwa na muda wa eti kuondoka akiwa ameongozana na watoto wake. 

Kinababa wa enzi hizo wao walikuwa wanakwenda kivyao, kwenda kukutana wenyewe wanaume sehemu zao za burudani, hakuna mtoto yoyote anayetakiwa hapo.

Akinamama nao walikwenda sehemu zao wakiwa na watoto wenye umri mtoto mchanga hadi sita, na wale kuanzia miaka saba hadi 18 nao hawakutaka kuongozana na watoto, baba au mama. Hawa nao walikwenda sehemu zao. Hawa ndiyo asilimia kubwa ndiyo waenda 'bichi' au kule vijijini 'pikniki'.

Kwa miaka ya hivi karibuni pia kumekuwa na upungufu mkubwa wa maeneo ya watoto kwenda kusherehekea sikukuu kuliko wakubwa.

Mabaa, mahoteli, kumbi za burudani kwa wakubwa zimejaa tele, lakini watoto wamesahaulika. Hakuna maeneo ya wazi kama zamani yalikuwa yakimilikiwa na Jiji yenye bustani ambayo yatawafanya watoto kwenda kufurahia sikukuu. Kuna maeneo machache sana yaliyobaki baada ya mengi kupigwa bei, ambayo watoto hukusanyika na kupata burudani. Zamani kulikuwa na meneo mengi ya wazi ambayo yalitengenezwa kama vizimba kwa kutumia magunia, na wakawa wanaingia na pesa, humo wanakuta ngoma za asili, maigizo, na michezo mbalimbali ya watoto kama kubembea, huku kukiwa pia na vyakula mbalimbali kama mishikaki, mihogo, Ice Cream na vingine vingi ambavyo watoto walifurahia sana.

Kukosekana maeneo ya burudani kwa watoto ndiyo imesababisha miaka ya hivi karibuni watoto nao kutinga kwenye kumbi za starehe, licha ya kwamba hawaendi kustarehe, lakini wanatumia majengo hayo ambayo kiafya kwao si mazuri. Wanakuwa wengi na kunakuwa na joto kali, hivyo wakati mwingine yanatokea matatizo makubwa. Kwenye miaka ya karibuni kumetokea maafa watoto walifariki kwenye ukumbi uliokuwa na joto.

Hii imesababisha hata Makamanda wa Polisi wa Mikoani kila mwaka kupiga marufuku 'disco toto', au watoto kuingia kwenye kumbi.

Ni hatari kubwa watoto kuingia kwenye kumbi ambazo zimefunikwa juu, lakini hili lingeepukika kama nchi ingekuwa na maeneo mengi ya wazi kama zamani kwa ajili ya watoto nao kuinjoi sikukuu kama wenzao wa zamani. 

Tuma meseji 0716 350534