Ukeketaji unavyozidi kuwa suala sugu kwa jamii nyingi

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 10:47 AM Aug 13 2024
Elimu ikitolewa kwenye kijiwe cha wacheza drafti Kipunguni Dar es Salaam.
PICHA: MPIGAPICHA WETU
Elimu ikitolewa kwenye kijiwe cha wacheza drafti Kipunguni Dar es Salaam.

TAARIFA ya hivi karibuni ya mtandao wa asasi 12 za kupinga ukeketaji nchini inaonesha kuwa, licha ya jitihada zinazofanywa na serikali na wadau kupambana na ukeketaji, bado vitendo hivyo vinaendelea bila uoga.

Anaonya Mkurugenzi wa Kituo cha Sauti ya Jamii Kipunguni jijini Dar es Salaam, Seleman Bishagazi, alipozungumza na gazeti hili kuhusu mbinu wanazotumia kupambana na vitendo hivyo.
 
 Anasema wameanza kampeni na wataendelea hadi Desemba, mwezi ambao ukeketaji unashamiri wakati wa likizo, na kwa kisingizio kuwa mwaka huu unagawanyika kwa mbili,  hivyo umejaa neema.
 "Kwa wale wasiojua, Dar es Salaam ukeketaji upo, ingawa kwenye kata yetu ya Kipunguni vitendo hivyo vimepungua, lakini ni muhimu tuendelee kuelimisha umma ili visiongezeke.” Anasema.

Anataja kata za jirani ikiwamo ya Msongola kuwa, ukeketaji upo na kwamba walianza kampeni hiyo hivi karibuni, na wanatarajia kufika katika maeneo mengi yenye mkusanyiko. 

Anasema wanalenga kufikia masoko, gereji, kwa mama na baba lishe, viwanja vya mipira, stendi za bajaji na bodaboda, vijiwe vya kahawa na vya madalali.
 
 "Lengo letu ni kuijengea jamii uelewa wa kutosha kuhusu madhara ya ukeketaji na pia kuwaelimisha watu kutambua viashiria vya ukatili.

Pia, kuwapa elimu ya afya ya uzazi, kadhalika kuwapa maelezo ili kujua mahali sahihi pa kutoa taarifa za ukatili huo unapotokea kwenye jamii, anasema Bishagazi.
 
 Aidha, watatoa elimu kuhusu ulinzi wa mtoto, madhara ya rushwa ya ngono na umuhimu wa wanaume kushiriki kuzuia ukatili hasa ukeketaji na ukandamizaji wa wanawake.
 
 Mkurugenzi huyo anasema, mwaka unaogawanyika kwa mbili kama huu wa 2024 unachukuliwa kama msimu maalumu wa ukeketaji, kwa maelezo kuwa washiriki wanaamini kuwa ni mwaka wa neema.
 
 "Si kwamba miaka mingine isiyogawanyika kwa mbili hawakeketi, wanafanya hivyo lakini si kwa wingi kama inavyofanyika kwenye mwaka unaogawanyika kwa mbili," anasema.
 
 WADAU WA KAMPENI
 
 Bishagazi anawataja washiriki wa kampeni hiyo kuwa ni klabu za kupinga ukatili zilizo chini ya kituo hicho, wataalamu wa afya ngazi ya jamii, viongozi wa serikali za mitaa na Diwani wa Kata ya Kipunguni.
 
 Anasema, mkakati huo ni kutekeleza mpango kazi waliokubaliana kwenye vikao vya klabu wa kupita sehemu yoyote yenye mkusanyiko wa watu kutoa elimu hiyo ili kutokomeza ukeketaji katika eneo lao ambayo ni mila yenye athari kiafya.
 
 Diwani wa Kata ya Kipunguni, Steven Mushi, anasema ameungana na kituo hicho katika kampeni hiyo ili kuwafikia vijana, kina mama, wanaume, wazee na watu wenye ulemavu.
 
 "Wazo la kuanzisha kwa kampeni hii lilitokana na klabu za kupinga ukatili ndani ya jamii ambapo viongozi wa Kituo cha Sauti ya Jamii walinishirikisha niwasaidie katika kampeni hii," anasema Mushi.
 
 Diwani anasema, atajitahidi kwa hali na mali kampeni hiyo imfikie kila mwanajamii katika eneo lake ili kufanikisha kuwapo mabadiliko katika jamii.
 
 "Kipunguni imepakana na kata ambazo zinakeketa, kwani baadhi ya wakazi wake wametokea katika mikoa inayoendeleza mila hiyo, hivyo hatuna budi kuendelea kuelimisha umma kuacha vitendo hivyo," anasema.
 
 Anasema, taarifa za mashirika mbalimbali zimekuwa zikionesha jinsi ambavyo ukeketaji bado ni hatari na kwamba wao kwenye Kata ya Kipunguni wameamua kuchukua hatua hizo.
 
 "Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalotetea haki, Usawa wa Wanawake na Wasichana UN, zaidi ya wanawake na wasichana milioni 200 duniani kote wamepitia ukeketaji.” Anasema Munisi. 

Anasema, shirika hilo linaeleza kuwa, mwaka huu wa 2024, takribani wasichana milioni 4.4 watakuwa katika hatari ya kufanyiwa ukatili huo, ikiwa ni wastani wa zaidi ya kesi 12,000 kila siku.
 
 "Lakini takwimu za demografia ya afya za mwaka 2015 zinaonyesha kuwa, asilimia 10 ya wanawake wenye umri kati ya miaka 15 hadi 49, wamekeketwa hapa Tanzania, huku takwimu za mwaka 2022 zikionesha kuwa, idadi hiyo imepungua kwa asilimia mbili tu ambapo kwa sasa ni asilimia nane ya wanawake wa umri huo wamekeketwa," anasema.
 
 Wakati kata hiyo ikiwa katika kampeni hizo, taarifa zinazotolewa hivi karibuni na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima, zinataja mikoa yenye kiwango kikubwa cha ukeketaji ambapo kwa sasa ni Arusha yenye asilimia 43.
 
 Kwa mujibu wa Waziri, mikoa mingine na asilimia zake kwenye mabano ni Manyara (43), Mara (28), Singida (20), Tanga (19), Dodoma (18), Iringa (12) na Morogoro (10).

Pia anautaja Mkoa wa Kilimanjaro kuwa na asilimia tisa, Njombe saba, Pwani tano na Mbeya asilimia tatu, na kwamba wizara inaendelea kutekeleza mkakati wa kupunguza vitendo hivyo kufikia asilimia tano ifikapo mwakani ambao ni ukomo wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025.