Uchaguzi unapokaribia, Pwani mguu sawa kufunza wapigakura

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 07:02 AM Sep 24 2024
Mjumbe wa NaCoNGO mkoani Pwani, Prisca Ngweshemi (kushoto), akishiriki jukwaa.
PICHA: SABATO KASIKA
Mjumbe wa NaCoNGO mkoani Pwani, Prisca Ngweshemi (kushoto), akishiriki jukwaa.

MWAKA huu ni wa uchaguzi wa serikali za vitongoji na vijiji pamoja na mitaa maeneo ya mijini, ukitarajiwa kufanyika Novemba 27, kisha utafuatiwa na uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani, Oktoba mwakani.

Kabla ya uchaguzi huo mkuu ambao wapigakura wanawachagua rais, wabunge na madiwani kwa upande wa Bara, Zanzibar wanawachagua marais wa Zanzibar na Jamhuri ya Muungano, wabunge, wawakilishi na madiwani, kuwaandaa wapigakura ni kipaumbele mijini na vijijini. 

Kabla ya kufikia hatua hiyo michakato mbalimbali inaendelea, ikiwamo kuboresha daftari la kudumu la wapigirakura, jukumu linalofanywa na Tume Huru ya Uchaguzi ya Taifa (INEC) na ZEC.
 
  Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO), nalo linakumbushwa kutoa elimu ya mpigakura kwa wananchi ili wajue umuhimu wa kushiriki uchaguzi kuwapata viongozi wanaowataka.
 
 Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Simon Nickson, akiongea kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani,  Abubakar Kunenge, anayesema hayo, hivi karibuni, katika mkutano wa jukwaa la mashirika yasiyo ya kiserikali mkoani humo.
 
 Ni kutokana na umuhimu wa elimu hiyo kwa wananchi, anasema mkoa huo unayahimiza mashirika yasiyo ya kiserikali kutoa elimu itakayowajengea uwezo wa kutoa maoni mbalimbali na kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu. 

Nickson, anasema elimu ya mpigakura inamsaidia mwananchi kuelewa kuhusu kushiriki mchakato wa uchaguzi kwa kuchagua au kujitokeza kuomba kuchaguliwa kuwa kiongozi.
 
 "Tunategemea mashirika yasiyo ya kiserikali kushirikiana nasi kukabiliana na changamoto zinazoikabili jamii, hasa uelewa kuhusu uchaguzi," anasema Nickson.
 
 Anafafanua kuwa mashirika hayo pia yana jukumu la kuunganisha wananchi, kwa sababu wakati wa kampeni za uchaguzi kuna mambo mengi yakiwamo kuhasimiana kutokana na itikadi za kisiasa.
 
 "Kwa hiyo pamoja na majukumu mbalimbali mlio nayo, kushiriki kutoa elimu ili kusaidia wakazi wa  Pwani kujua haki yao kwenye uchaguzi ni jambo muhimu," anasema.
 
 Aidha, Nickson anasisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya mashirika hayo na serikali na pia kati yao  ili kurahisisha utekelezaji wa mipango ya maendeleo.
 
 "Kuleta maendeleo kunahitaji ushirikiano hata katika uchaguzi, kwa ajili ya kupata viongozi bora watakaoisaidia nchi kuendelea kusonga mbele. Ili kufikia hatua hiyo, elimu ya mpigakura kwa wananchi ni ya muhimu ili waweze kushiriki kwa wingi katika uchaguzi, wachague viongozi sahihi wa kuendelea kusimamia nchi vizuri," anasema.
 
    Mjumbe wa NaCoNGO mkoa wa Pwani, Prisca Ngweshemi, anasema mkoa huo una zaidi ya mashirika 30 yasiyo ya kiserikali, na kwamba yale ambayo hayafanyi kazi kikamilifu, 'watayaamsha'.
 
 Anasema baraza hilo linatamani mashirika yote ya kiraia mkoani humo yawe hai na kufanya kazi kikamilifu, ili kusaidiana na serikali kuwaletea wananchi maendeleo.
 
 "Hivyo, tutayaamsha mashirika yaliyolala kwa kuyafuatilia kujua chanzo ya kutofanya kazi ili iwe rahisi kwetu kuchukua hatua za kuyasaidia kurudi kwenye majukumu yaliyofanywa yakaanzishwa," anasema Prisca.
 
 Prisca anafafanua kuwa baraza lao linatekeleza majukumu mbalimbali ikiwamo kulinda maslahi ya AZAKI,  kujenga mitandao na mashirikiano miongoni mwa mashirika yasiyo ya kiserikali na kuwa sauti ya umoja kwenye masuala yao.

 “Nchi ina mikakati na mipango iliyojiwekea hasa maendeleo, hivyo nasi ni muhimu kuwa miongoni mwa wadau wanaochangia katika hilo, kwa kuhamasisha wananchi kushiriki shughuli mbalimbali," anasema.
 
 Adha, anaongeza kuwa katika kipindi cha kutekeleza majukumu yao mwaka 2024 hadi hadi 2027 watahakikisha kama kulikuwa na mapungufu kwenye baraza lililopita, wanayarekebisha.
 
 Prisca anasema wamejipanga kusaidia mashirika yasiyokuwa ya kiserikali katika nyanja mbalimbali ikiwamo kuyajengea uwezo mashirika yasiyokuwa ya kiserikali kitaasisi na kiutendaji.
 
 "Tunataka kusaidia mashirika kuzingatia sheria na taratibu za nchi, kuimarisha ushirikiano kati ya serikali na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali, kuimarisha ushiriki wa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali katika kuchangia maoni kwenye Dira  ya Maendeleo ya 2050," anasema.
 
 Anasema, wamepanga kuongeza juhudi kutekeleza mipango ya taifa kama Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, mikakati mbalimbali ikiwamo kuelimisha wananchi kujua umuhimu wa kujenga taifa lao na kuwa na Tanzania bora kwa Watanzania wote.
 
 Mjumbe anasema baraza lao linatamani kila asasi ya kiraia na wananchi washiriki katika kutoa maoni kwenye dira hiyo ili iwe jumuishi.
 
 Anafafunua kuwa, maendeleo hayo jumuishi, ni katika ushiriki wa makundi maalum kwenye shughuli za kiuchumi na huduma za jamii ili upewe kipaumbele kwenye utekelezaji wa afua mbalimbali za kiserikali na wadau wengine.
 
 “Vipaumbele vya baraza letu katika kipindi cha kutekeleza majukumu yetu kwa mwaka 2024 hadi ifikapo mwaka 2027 ni kurekebisha mapungufu yote ya baraza lililopita na kuja na vingine vipya.”