MABADILIKO ya tabianchi ni kitisho kikubwa cha karne ya 21 kinachohitaji kuwa na tahadhari kwenye shughuli karibu zote anazofanya binadamu.
Taasisi ya Utafiti wa Misitu (TAFORI), inaonya kuwa tahadhari ni muhimu kwa kila mmoja, ikiwakumbusha wanaofanya shughuli kwenye misitu wazingatie kuwalinda nyuki, ambao wanadaiwa kuanza kupungua.
TAFORI inawaelekeza kujiepusha na kuleta athari zinazoweza kusababisha kupungua kwa makundi ya nyuki na kuzorotesha uzalishaji wa mazao ya nyuki kuanzia asali hadi nta.
Kaimu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Utafiti wa Ufugaji Nyuki, Allen Kazimoto, ameyasema hayo wakati akizungumza na wanahabari kwenye moja ya vituo vya ufugaji nyuki vya TAFORI mkoani Morogoro.
Anasema kuna madai kuwa makundi ya nyuki yanapungua na kwamba wanaendelea kufanya tafiti katika maeneo ya Kongwa, Chamwino na Itilima jijini Dodoma kubaini kama kuna upungufu unaozungumziwa.
Kazimoto, anasema kupungua kwa makundi ya nyuki kunaweza kukasabishwa na mambo mbalimbali ikiwamo kukata miti ovyo, kuchoma mkaa na watu kuandaa maeneo ya mashamba kwenye sehemu ambazo nyuki wangeweza kutengeneza makazi yao.
Pia, aliongeza licha ya kwamba suala la ukataji miti linafanyika kwa shughuli mbalimbali lakini umakini zaidi unatakiwa zama hizi.
Anaeleza kuwa, kiwango cha kukata miti kunapaswa kusizidi sana mpaka kuhatarisha maisha ya viumbe wengine kwa sababu nyuki na mimea ni vitu vinavyotegemeana ambapo nyuki wanategemea mimea na mimea nayo inawategemea nyuki kuchavushwa.
Aidha, Kazimoto anasema mabadiliko ya tabianchi yana athari kubwa kwenye kupungua kwa makundi ya nyuki.
Anaongeza kuwa, ukiongelea suala la uhifadhi lazima kuangalia pande zote ikiwamo misitu na bayoanuai zote kwa sababu viumbe hivyo vinategemeana.
VIUATILIFU VINAHUSIKA
Kazimoto analitaja jambo jingine linaloweza kusababisha kupungua kwa makundi ya nyuki kuwa ni matumizi hatarishi ya viuatilifu kwenye mazao ya kilimo.
Anafafanua kuwa, viuatilifu vinatishia uhai wa nyuki kwa sababu viuatilifu vimetengenezwa kuua wadudu wote bila kujali ni rafiki au maadui.
Anasema nyuki naye ni mdudu na akienda pale walipopuliza dawa anakuwa ni mhanga mmojawapo na hivyo kupunguza wingi wa makundi ya nyuki na uzalishaji asali na nta.
Akizungumzia suala la masoko ya mazao ya nyuki anasisitiza wafugaji, kuzingatia ubora wa asali na bidhaa nyingine ili kuondokana na changamoto ya kuwapo kwa baadhi ya mazao yaliyoandaliwa bila kukidhi viwango vinavyotakiwa.
Pamoja na ubora anawataka pia kujali mahitaji ya soko la kimataifa na hivyo kujiepusha na changamoto za kukosa masoko ya kuuzia bidhaa zao.
Anasema TAFORI inawaunganisha wazalishaji na masoko ya ndani na nje ya nchi na kwamba hali ya biashara ya mazao ya nyuki kwa sasa siyo tatizo kwa sababu masoko ya kimataifa yana nafasi kubwa ya kuchukua bidhaa nyingi nchini.
Aidha, anawahakikisha kuwa soko lipo na bidhaa hizo zinazohitajika ni asali ambayo changamoto kubwa iliyopo leo ni kupatikana kwa mazao hayo katika kiwango kinachohitajika.
Hivyo, anawashauri vijana kujiunga kwenye vikundi vya ufugaji wa nyuki ili kuwa na uwezo kamilifu wa kufikia hata kutoa tani mbili au tatu za asali na kukidhi mahitaji ya masoko ya nje tofauti na ilivyo kwa sasa.
Kazimoto anatoa wito kwa Watanzania hasa vijana na wanawake kuingia kwenye shughuli za kufuga nyuki ili kukabili ukosefu wa ajira kwa jamii na kuwataka walimalize kupitia sekta ya nyuki.
Anasema taasisi hiyo hufanya utafiti kwa ajili ya wadau mbalimbali ikiwamo serikali na jamii wakiwa na kazi ya kutafiti, kuratibu na kusambaza matokeo ya utafiti ili jamii ifaidike na wanavyovifanya.
“Miaka ya nyuma ilizoeleka kuwa, kufuga nyuki ni kazi ya wazee lakini kwa sasa siyo shughuli ya wazee pekee bali ni kila mwanajamii mwenye ari ya kufanya hivyo, kwa kufuata taratibu zinazotakiwa ili kuleta mnyororo wa thamani katika shughuli hiy. Aidha, mtu anaweza asiende mwenyewe kuweka mizinga lakini anaweza akawa sehemu ya mnyororo ya kuwa mnunuzi wa asali inayozalishwa.
Pamoja na kununua pia akawa anachakata na kufungasha na kuuza, shughuli ambayo inaweza ikafanywa na mtu yeyote awe mwanamke na hata vijana,” anasema Kazimoto.
Hivyo, anatoa wito watu kuwa na ari ya kujiingiza kwenye shughuli ya ufugaji wa nyuki baada ya kujipima wapi panawafaa katika kukuza mnyororo wa thamani kuanzia kuweka mizinga, kuitengeneza, kuuza asali hadi au kufanya biashara ya mazao mengine kama nta, dawa na mishumaa.
Kazimoto anayataja manufaa yanayotokana ufugaji wa nyuki kama vile asali huweza kuwa ni chakula kwa ajili ya lishe na pia hutumika kwenye tiba na mazao mengine ni kama nta na sumu ya nyuki ambapo husaidia kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja kwa anayejishughulisha ufagaji nyuki, hata kwa taifa pia.
Aidha, Ofisa Misitu Mkuu kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii Idara ya Misitu na Nyuki (Elimu na Misitu ya Jamii) Emmanuel Msoffe, anawataka vijana pamoja na makundi maalum kuzitama fursa zilizopo kwenye misitu na kuzitumia kikamilifu.
Anasema vijana ni kundi kubwa kwa mujibu wa matokeo ya sensa ya mwaka 2022 ambao wanahitaji ajira na vipato kwa sasa ambapo fursa zilizopo kwenye misitu na nyuki wakizitumia vyema wanaweza kuondokana tatizo kubwa la ukosefu wa ajira na vipato.
Ofisa Mtafiti Mkuu TAFORI ambaye ni Kaimu Mkurugenzi wa Utafiti na Uzalishaji Misitu, Steven Maduka, anasema TAFORI hufanya utafiti wa miti mbalimbali kwa ajili ya manufaa kwa jamii sambamba na kuongeza thamani hasa kwenye miti ya asili iliyopo porini.
Anasema mitipori na matunda yake hutengenezewa juisi na mvinyo ambapo mtu huweza kunufaika navyo kwa kuuza ili kujiongezea kipato, hivyo tuepukane na uharibifu wa miti ili tuendelee kunufaika nayo.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED