Sura mbili za Dube Yanga na kelele za kukosa mabao

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 09:42 AM Sep 16 2024
news
Picha: Mtandao
Prince Dube.

UNAWEZA kufunga zaidi ya wengine, lakini huwezi kufunga kila mechi na kuweka mpira wavuni kila nafasi inayopatikana.

Mijadala imekuwa mikali kuhusu kiwango cha straika wa Yanga, Prince Dube, baada ya kumalizika kwa mchezo wa mkondo wa kwanza, Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya raundi ya kwanza, uliochezwa Uwanja wa Abebe Bikila nchini Ethiopia dhidi ya wenyeji, CBE.

Licha ya kufunga bao pekee katika mchezo huo, lakini ndiye aliyekosa mabao mengi ya wazi katika mchezo huo.

Alikosa mabao manne, lakini matatu yakionekana ni rahisi zaidi kukosa kuliko kupata.

Pamoja na ushindi wa bao 1-0 ugenini, lakini mijadala kwenye mitandao ya kijamii, kwenye vijiwe vya michezo, redioni na televisheni, imekuwa ni jinsi Yanga ilivyokosa mabao mengi, hasa straika huyo raia wa Zimbabwe.

Baadhi ya mashabiki wa Yanga jana walionekana kutoridhishwa na mwenendo wake wa kukosa mabao, wakikumbushia hata kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Kagera Sugar.

Hata hivyo, pamoja na Dube kwa siku za karibuni kuonekana kukosa mabao mengi, rekodi na takwimu zinambeba, kwani yeye na Stephane Aziz Ki, ndiyo wachezaji waliofunga mabao mengi ya Yanga mpaka msimu huu, tangu kuanza kwa msimu huu, akianzia kwenye michezo ya kirafiki ya kimataifa 'pre season', hadi mechi za kimashindano ikiwamo ya juzi.

Haya ndiyo mabao ya Dube aliyopachika akiwa na Klabu ya Yanga baada ya kujiunga nayo msimu huu akitokea Azam FC. 

TS Galaxy vs Yanga

Alifunga bao kwa mguu wa kushoto akiwa kwenye wingi ya kushoto dakika ya 55, dhidi ya TS Galaxy ya Afrika Kusini katika mchezo maalum wa kimataifa kugombea Kombe la Mpumalanga Julai 24, mwaka huu, Uwanja wa Mbombela nchini Afrika Kusini. Lilikuwa bao la kwanza kwa straika huyo akiwa na klabu hiyo. Yanga ilishinda bao 1-0. 

Kaizer Chiefs vs Yanga

Katika mchezo mwingine wa kimataifa Yanga ikiwa Afrika Kusini, Dube alipachika bao moja katika mchezo wa Kombe la Toyota dhidi ya Kaizer Chiefs, uliochezwa Julai 28, mwaka huu, Uwanja wa Bloemfonteim.

Alifunga dakika ya 24 baada ya mabeki wa timu mwenyeji kujichanganya wenyewe na kuukwamisha kwa mguu wa kulia, Yanga ikishinda mabao 4-0, mengine yakipachikwa na Stephane Aziz Ki, aliyefunga mawili na Clement Mzize moja. 

Yanga vs Azam FC

Ilikuwa ni Agosti 11, mwaka huu, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, katika mchezo wa fainali ya Ngao ya Jamii, Yanga ikishinda mabao 4-1 dhidi ya Azam FC.

Katika mabao hayo, Dube pia alitupia moja, lililokuwa la kusawazisha baada ya Feisal Salum kutangulia kufunga bao dakika ya 13.

Alitanguliziwa mpira mrefu, kama kawaida yake akawaacha kwa mbio, mabeki wa Azam, akaupachika wavuni kwa mguu wa kulia, dakika ya 19.

Mabao mengine ya Yanga katika mchezo huo yalifungwa na Aziz Ki, Mzize, Yoro Diaby akijifunga mwenyewe. 

Vital'O vs Yanga

Alifunga kwa mguu wa kushoto likifanana kabisa na lile alilofunga dhidi ya TS Galaxy ya Afrika Kusini.

Ilikuwa ni Agosti 17, mwaka huu, Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, katika mchezo wa hatua ya awali, Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Vital'O ya Burundi.

Aliupata mpira kwenye wingi ya kushoto kama kawaida yake, akaingia ndani kidogo akaukwamisha wavuni dakika ya sita ya mchezo. Katika mchezo huo Yanga ilishinda mabao 4-0, mengine yakifungwa na Aziz Ki. Clatous Chama na Mzize. 

Yanga vs Vital'O

Dube alifunga tena bao katika mchezo wa marudiano Ligi ya Mabingwa Afrika hatua za awali dhidi ya Vital'O ya Burundi, mechi ikichezwa tena Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, na Yanga kushinda mabao 6-0.

Katika mchezo huo uliochezwa, Agosti 24, mwaka huu, mabao mengine yalifungwa na Pacome Zouzoua, Mzize, Chama, Aziz Ki na Mudathir Yahaya.

Dube, alifunga kwa mguu wa kulia akitokea upande wa kushoto ambako ndiko anapendelea zaidi kutegea mipira yake, aliingia nao ndani kidogo, akaupiga kwa mguu wa kulia na kujaa nyavuni.