Simulizi na ushuhuda uliotawaliwa na vifo, majeruhi, saikolojia mateso

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:58 AM Oct 24 2024
     Hali halisi ya waathirika wa shambulizi la vikosi vya Israel, ndani ya Gaza.
Picha:Mtandao
Hali halisi ya waathirika wa shambulizi la vikosi vya Israel, ndani ya Gaza.

HADI sasa simulizi hazipendezi katika makazi ya jamii ya Kipalestina, watu wanakimbia mashambulizi ya ardhini ya Israel kwenye kambi ya wakimbizi ya Jabalia, Kaskazini mwa Gaza, kukiwapo kundi la majeruhi na maiti zinazotapakaa njiani.

Ndio uhalisia wake mahali hapo, simulizi zikianza kwa mwanaume anayeeleza kwamba, kuna maiti zimetapakaa, baada ya kuamriwa kuondoka eneo hilo na wanajeshi wa Israel. 

Mwanamke mwingine naye ana hayo, kwamba watu waliondoka kwa hofu kubwa na kuwaacha watoto wao, huku Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina, linatoa wito wa kusitishwa mapigano kwa muda, ili kuwezesha njia salama kwa familia zinazotaka kuondoka mahali hapo.

Hilo linachukua nafasi, huku hospitali mbili za ndani ya Palestina, zikitahadharisha kwamba zimeishiwa vifaa za kuwahudumia wagonjwa.

Israel inasema wanajeshi wake wanaendelea na operesheni dhidi ya wapiganaji wa Hamas, huku wakiwaondoa raia kwa usalama.

Zaidi ya watu 400 wanaripotiwa kuuawa na maelfu wameyakimbia makazi yao tangu jeshi lilipoanzisha mashambulizi ya tatu katika eneo la Jabalia mnamo Oktoba 6 mwaka huu, likisema linawatokemeza wapiganaji wa Hamas waliojipanga tena huko.

Operesheni hiyo imekuja wakati Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken akielekea Israel kujaribu kufufua mchakato wa kidiplomasia uliokwama kuhusu makubaliano ya kusitisha mapigano na kuwaachilia huru mateka kutoka Gaza.

Hiyo ni baada ya mauaji yaliyofanywa na wanajeshi wa Israel ya kiongozi wa Hamas Yahya Sinwar wiki iliyopita,Waziri wa Marekani Blinken, akisisitiza haja ya Israel kuchukua hatua za kuongeza mtiririko wa misaada ya kibinadamu kuingia Gaza, kuwasaidia raia wasiokuwa na makosa.

USHUHUDA WA WANAOKIMBIA

Watu waliokimbia makazi yao katika kambi ya Jabalia na kutafuta hifadhi kitongoji cha karibu cha Rimal cha Gaza City, akiwamo mwanaume anayejitambulisha kwa jina la Saleh, ana maelezo kuu alikokuwa akiishi na familia yake.

Madaktari na wafanyakazi wa uokoaji, wanasema zaidi ya watu 20 waliuawa katika shambulio la anga la Israel eneo hilo, wiki moja iliyopita. 

Jeshi la Israel limewataja wapiganaji 18 wa Hamas na Palestina Islamic Jihad siku ya Jumanne kuwa miongoni mwa waliofariki.

"Tulipokea ujumbe kupitia droni za Israel, zikitusihi tuhame, kwa hiyo tukaanza kutembea chini ya uangalizi wa wanajeshi wa Israel, ambao walitutaka tuelekee kusini au magharibi mwa Gaza. Nilikuwa na nyanya (mama wa bibi) yangu, alikuwa hawawezi kutembea, kama wengine wengi," anasimulia.

Mwanaume mwingine, Mohammed al-Danani, anasimulia alivyokuwa katika shule hiyo na akashuhudia miili ya waliouawa barabarani. Pia, alikuwa katika eneo la bwawa mojawapo wakati droni zikitangaza amri ya watu kuelekea mji wa Beit Lahia, Kaskazini mwa kambi hiyo.

"Hali ilikuwa ngumu sana, hakuna mtu aliyejua pa kwenda. Watu wengine walilazimika kukimbia bila watoto wao na kuwaacha shuleni huku wakitoroka na wengine," anasema.

Siku ya Jumanne wiki hii, Jeshi la Israel lilitangaza kuwa wanajeshi wake wanaendelea na mapigano katika eneo la Jabalia, huku wakiwahamisha raia kutoka eneo la mapigano.

“Maelfu ya raia wamehamishwa. Makumi ya magaidi wamekamatwa kutoka miongoni mwa raia,” lilisema jeshi la Israel kwenye chapisho hilo, ila X - likijumuisha video inayoonyesha umati wa watu wakitembea katika mitaa iliyoharibiwa.

Jeshi pia linakiri, askari wake wamewaua Wapalestina 10 wakiwataja “walikuwa tishio katika shambulio moja la anga,” ingawa hawakutoa maelezo zaidi.

Nalo Shirika la Hilali Nyekundu la Palestina, lilichapisha video inayoonyesha gari la wagonjwa likisafirisha miili ya watu kadhaa waliouawa kwa kushambuliwa na makombora katika mji wa Jabalia Jumatatu wiki hii.

Pia, kuna simulizi ya video nyingine iliyorekodiwa siku hiyo, ikionyesha jitihada za mkazi mmoja anayejaribu kusaidia umma, wakiwamo kinamama na watoto waliojeruhiwa na wengine kufariki kwenye kambi ya shule iitwayo Jabalia.

Watoto waathitrika wa vita vya Israel na Palestina. PICHA ZOTE: MTANDAO
Mwanamke aitwaye Dawasah, ana simulizi ya namna alivyotoroka eneo hilo siku ya Jumanne wiki hii akisimulia hali ya usalama ni ndogo, kuwapo majeruhi na hapakuwapo gari la kubeba wagonjwa.

KUTOKA UMOJA MATAIFA

Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA), Philippe Lazzarini, anasema wafanyakazi wake Kaskazini mwa Gaza wanaripoti hawakuweza kupata chakula, maji au huduma za matibabu.

"Harufu ya maiti ipo kila mahali kwani miili imeachwa imelala barabarani au chini ya vifusi," Lazzarini aliandika kwenye mtandao ‘X’ na kuongeza: "Watu wanangojea tu kufa. Wanajihisi kutelekezwa, kutengwa, na hawana tumaini."

Lazzarini ana wito akinena: "Kusitishwe mapigano mara moja, hata ikiwa kwa saa chache, ili kuwezesha njia salama za kibinadamu kwa familia zinazotaka kuondoka eneo hilo na kufika maeneo salama."

Kutoka Umoja wa Mataifa, kuna ufafanuzi kwamba serikali ya Israel inaendelea kukataa ombi la ofisi yake ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA), kusaidia kuwaokoa raia waliokwama chini ya vifusi na kuwasilisha vifaa vinavyohitajika katika hospitali.

Mkurugenzi wa Hospitali ya Indonesia, ambayo ni mojawapo ya wanaofanya kazi karibu na Jabalia, Dk. Marwan al-Sultan, akisema wanajeshi wa Israel, walisimama nje ya lango na kulikuwa na milio ya risasi kila mara eneo hilo.

"Hilo limezua hali ya hofu na kuchanganyikiwa kwa wagonjwa na wafanyakazi wa matibabu," anasimulia Dk. Marwan al-Sultan, akiongeza: "Pia tunakabiliwa na uhaba mkubwa wa mafuta, vifaa vya matibabu, wafanyakazi, chakula na maji.

“Aidha, kukatika kwa umeme kunaendelea kulazimu hospitali kutegemea vyanzo vya nishati mbadala vinavyodumu kwa saa nane hadi 10 pekee na hilo linahatarisha usalama wa wagonjwa.”

Hata hivyo, jeshi la Israel linakanusha kwa kusema linahakikisha hospitali zinafanya kazi wakati wa mashambulizi hayo, ikiwa na uthibitisho wake kwamba hilo lipo tangu wiki iliyopita.

Kwa mujibu wa taarifa ya jeshi hilo, ni kwamba  zaidi ya malori 230 ya kubeba chakula, maji, vifaa vya matibabu na malazi yamepelekwa Kaskazini mwa Gaza, kupitia kivuko kilichoko Magharibi mwa eneo hilo.

Hiyo ni baada ya Umoja Mataifa kunena kwamba imepita wiki mbili sasa, jamii hiyo haijapatiwa mahitaji ya lazima wakati vita vikiendelea.

Israel ilianzisha operesheni ya kuiangamiza Hamas kujibu mashambulizi ya kundi hilo Kusini mwa Israel mnamo Oktoba 7, mwaka jana na takribani watu 1,200 waliuawa na wengine 251 walichukuliwa mateka.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya eneo hilo inayoendeshwa na Hamas, hadi sasa kuna zaidi ya watu 42,710 wameuawa huko Gaza, tangu operesheni hiyo ya Israel kuanza.

·     Kwa mujibu wa taarifa ya kimataifa.