TANZANIA ni miongoni mwa nchi zilizozungukwa na maji ya asili, hasa Bahari ya Hindi ambayo ni chanzo kikuu cha uchumi unaopewa jina ‘uchumi wa buluu’.
Sasa serikali inatarajia kuunda meli kubwa ya kisasa yenye urefu wa mita 39 maalumu kwa uvuvi wa kibiashara.
Bahari ya Hindi ni ya tatu kwa ukubwa duniani ikichukua asilimia 20 ya uso wa dunia na kuzungukwa na mabara manne. Tanzania ni miongoni mwa nchi wanufaika wa bahari hiyo.
Mkurugenzi wa Kuendeleza Ukuzaji Viumbe Maji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Nazael Madalla, anasema hatua hiyo ni baada ya takwimu kuonyesha dunia imekwishapoteza uvuvi wa asili, kutokana na viumbe maji kupungua kutokana na mahitaji.
Anasema, kwa sasa mikakati ni kuongeza uzalishaji wa vifaranga wa viumbe hao, kwa aina tofauti kama vile samaki na kaa, ili kukuza biashara katika soko la ndani na nje.
Mgalula Lyobah, Ofisa Mkuu wa Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO), anasema shirika linatarajia kuanza shughuli baada ya kuanza kukarabatiwa, kuja na zana za kisasa za uvuvi zitazofika bahari kuu, ili kukidhi mahitaji ya kitoweo hicho.
TAFICO, ni taasisi ya umma iliyoanzishwa mwaka 1974 chini ya Sheria ya Mashirika ya Umma Na. 17 ya mwaka 1969 na ina jukumu la kuendeleza sekta ya uvuvi nchini kupitia uwekezaji katika miradi mbalimbali inayolenga kuongeza tija hasa katika uvuvi wa bahari kuu na kuimarisha mnyororo wa thamani kwa mazao ya uvuvi.
Inafanya shughuli zake katika ukanda wa Bahari ya Hindi, Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika, Ziwa Nyasa na maji madogo.
Kwa mujibu wa Dk. Madalla, matumizi ya kila mtu ya kilo 10.5 kwa mwaka bila kujumuisha mahitaji ya mauzo ya nje ambayo ni asilimia 10 ya jumla ya uzalishaji.
Mahitaji ya samaki ifikapo mwaka 2050 inakadiriwa kufikia tani milioni 1.36 kwa makadirio ya watu milioni 129 ifikapo mwaka huo.
Dk. Madalla, anasema hatua mbalimbali zinachukuliwa baada ya takwimu kuonyesha dunia imekwishapoteza uvuvi wake katika vyanzo vya asili, kama vile bahari, maziwa na mito na mwelekeo ni katika kufuga viumbe hao.
VIFARANGA SAMAKI
Katika mafunzo ya siku tano kwa wanazuoni vijana 40 kwenye sekta ya uvuvi, Dk. Madalla anasema lengo ni kuwapa mbinu za ukuzaji viumbe maji, ikiwamo vifaranga vya samaki yaliyofanyika chuoni.
“Serikali inalenga kuongeza elimu ya ukuzaji viumbe hai, ikiwamo uzalishaji wa vifaranga vya samaki hasa kaa, ili kuongeza tija, mnyororo wa thamani na kupata soko la kimataifa.
“Soko la baadhi ya viumbe maji kama kambale, kaa bado ni changamoto. Samaki aina ya kambale inatokana baadhi kuwa na imani za kidini kwamba hawali samaki asiye na magamba, pia kaa soko lipo, ila hatua za vitotoreshi ni duni.
“Serikali imedhamiria kujenga vituo viwili vya uzalishaji wa vifaranga. Duniani imebainika mwaka 2022 katika takwimu asilimia 51 ya samaki walioliwa duniani, walitoka katika mazingira ya kufuga. Tanzania pia tunajitahidi kufikia asilimia 10 ya mazao yote ya uvuvi yanatokana na mazingira ya kufuga,” anasema Dk. Madalla.
Mratibu wa mafunzo hayo, Lucka Mgwena, anasema lengo ni kuwajengea uwezo vijana wahitimu katika fani za sayansi ya viumbe maji (Aquaculture) ngazi ya cheti, diploma na shahada, ili waweze kubaini fursa zilizopo kwenye ukuzaji viumbe hao nchini na kujiajiri.
“Vile vile, waweza kuwa na maarifa ya vitendo kwenye uzalishaji wa bidhaa, usimamizi na utafutaji wa masoko ya bidhaa zitokanazo na viumbe maji nchini. Maarifa yote yemejikita katika kuendeleza ukuzaji viumbe maji kibiashara,” anasema Lucka.
Anasema akiwa mmoja wa wanufaika na ufadhili wa masomo katika Shahada ya Uzamili wa Ukuzaji Viumbe maji na Sayansi ya Uvuvi, kupitia mradi huo, alifikiri namna ya kuwafikia vijana wahitimu, ili kuwaongezea maarifa ya kuwawezesha kuzibaini fursa na kujiajiri.
Lucka aliongeza kwamba, mfadhili wa mafunzo hayo ni AQUAFISH – African Centre of Excellence in Aquaculture and Fisheries (ACE II), kupitia Chuo Kikuu cha Lilongwe cha Kilimo na Maliasili (LUANAR) cha nchini Malawi.
Lyobah anasema, wakati dunia inaelekea katika uvuvi wa viumbe hai waliofugwa, kutokana na kupungua kwa viumbe hao katika vyanzo vya maji ya asili kama vile bahari, maziwa na mito, sasa mwelekeo ni ufugaji viumbe hao kwenye mabwawa na pembezoni mwa maji ya asili.
“Tunahitaji ufugaji wa kibiashara sio ule wa mazoea. Kuna mpango wa miradi tisa, imeanza kutekelezwa mwaka jana. Tunajenga meli kwa urefu unaoutaka, itajengwa kwa siku 270 ikiwa mita kama 39 kwa ajili ya uvuvi wa bahari kuu.
“Pia tuna lengo la uchakataji wa uvuvi tuwe na kiwanda, magari ya usafirishaji, tunataka kukarabati chumba cha ‘cold room’ tayari tuna mtambo wa barafu za chenga na tuna mtambo wa tani milioni 10 na tunatarajia kuwa tunazalisha chakula cha samaki wafugwao kikiwa na uwezo wa kuzalisha tani 30 kwa siku,” anasema Lyobah.
Anasema changamoto ya upatikanaji wa chakula kwa ajili ya viumbe maji hasa samaki inatokana na uhaba wa malighafi sokoni amabayo inagombewa na watumiaji kama vile binadamu na wafugaji.
“Mahindi hayo hayo yanategemewa na binadamu, ikizalishwa pumba inahitajika kwa ajili ya mifugo mingine pia kama kuku. Ujenzi wa kiwanda cha kuchakata mazao ya uvuvi unaendelea Kilwa,” anasema Lyobah.
CHANGAMOTO
Lyobah anasema kwamba uvuvi wa sasa zaidi hauna tija kwa sababu vyombo vinavyotumika vina uwezo mdogo, jambo linalosababisha wavuvi kutofikia uvuvi mkubwa yaani bahari kuu.
“Bahari imegawanyika kwa maeneo kama manne ambayo ya ndani na EEZ. Ndani tunaita ni maji ya kitaifa (territorial water), haya m,wenye nchi una mamlaka ya kuyasimamia. Baada ya maili 12 ni eneo la kiuchumi la bahari ‘EEZ’ ni maji unayoruhusiwa kuyatumia na nchi husika na anayehitaji ataomba kibali.
Pia kuna maji ya kimataifa na kila mtu anaweza kutumia ila inatakiwa ujitambulishe kwa kupepea kwa bendera ya nchi yako. TAFICO tumerudi kivingine kwa kutumia uvuvi wa kisasa ili kwenda mbali zaidi na si katika maji ya ndani ambayo unaweza kuleta mgogoro na wavuvi wadogo.
Tutawekeza katika ufugaji wa samaki na pia kwenye uvuvi mkubwa wa kibiashara,” anaeleza.
Tulikuwa na meli ya urefu wa mita 22 tulikuwa tunavua mwanzoni mwa eneo la EEZ (exclusive economic zone) karibu na bahari kuu. Tunalenga kuvuka eneo la EEZ ni eneo la nchi nyingine ambako unafuatwa tu utaratibu na unaendelea kuvua.
Lengo kuu ni samaki aina jodari ambaye tabia yake ni kuhama, leo yupo bahari inayomilikiwa na nchi hii kesho karudi Tanzania, au Ushelisheli!” anaeleza Lyobah.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED