Samia anavyoendesha ‘SU’; mwongozo wa Mzee Mwinyi, ubunifu na mahitaji ya leo

By Peter Orwa , Nipashe
Published at 07:39 AM Aug 30 2024
Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
Picha:Ikulu
Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.

KADRI muda unavyopita ndio tafsiri yake Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, aendako kiuchumi na mipango ya maendeleo inazidi kuwa mubashara kwa anakonuia kuufikisha uchumi wa nchi, ikiwamo eneo mahsusi mashirika ya umma.

Juzi akiwa jijini Arusha kukutana na wenyeviti wa bodi, pia watendaji wakuu wa taasisi za umma nchini, Rais Dk. Samia akafichua zaidi dhima yake kiuchumi, upande wa mashirika ya umma, maarufu ‘SU’. 

Hadi sasa mzizi wa anachoamua Rais, unaegemea mambo kadhaa kuanzia siasa hadi uchumi, yanayojumuishwa na mambo kama: Msukumo wa Ilani ya Uchaguzi chama chake – CCM; mipango ya taifa; kimataifa na ushauri kitaalam; mtazamo na dira yake binafsi. 

Pia, kuna matukio ya kijamii kama vile maafa na magonjwa, pia mwendelezo wa mipango na yaliyoamuliwa kitaifa kihistoria, mathalani mikakati mkubwa kitaifa anayoihangaikia sasa. 

Hapo umo mradi wa Maji wa Mwalimu Julius Nyerere, wazo lililoanza zama za serikali Awamu ya Kwanza, huku mradi wa reli ya kisasa- SGR, wazo lilianzia katika Awamu ya Nne. 

Pia, katika mstari huo, majumuisho ya tafsiri ya anachoamua leo kwa mashirika ya umma, dira ya utendaji wake ina utashi na zao la nchi inakotoka kiuchumi, pia inakoelekea, ikisawazishwa na mahitaji ya sasa, chini ya usukani wa Mama. 

Rais Dk. Samia akiwa muumini wa ushirikiano wa sekta binafsi na umma, maarufu PPP hoja yake ya juzi ikabeba ushuhuda wake alipochambua ‘nje ndani’ zilivyo, anachokihitaji kuwa mwelekeo wa taasisi hizo kitaifa sasa na kesho. 

Kihistoria, msingi na mzizi wa mashirika ya umma nchini unaanzia miaka mitatu baada ya Uhuru, 1964 ulipobuniwa Mpango wa Maendeleo ya Nchi wa Miaka Mitano, ambao ni wa kwanza.

Mwaka huo 1964, pia ulianza na kuwapo mfumo hodhi kiuchumi na kisiasa, kutoka huria, hata kufungua mlango zaidi kwa ‘SU’ kuwa msimamizi mkuu wa biashara na uzalishaji wa kitaasisi nchini. 

Ni mpango ulioitaka nchi kujitegemea na mahitaji ya msingi baada ya Uhuru, uzalishaji wake kufanywa na taasisi za nchini.  

Hata wakati mpango huo ulipokuwa unakamilika mwaka 1969, tayari kulishapatikana mashirika mengi ya umma, vikiwamo viwanda vilivyoundiwa sheria na chombo cha kusimamia chini ya Ofisi ya Rais kwa jina la SCOPO.

Kwa mujibu wa Sheria ya SCOPO 1969, shirika la umma lilikuwa lenye hisa za serikali kuanzia asilimia 51 na zaidi, ingawaje katika zama hizo za uchumi hodhi, mengi yalikuwa na hisa asilimia 100. 

Mageuzi ya mashirika hayo baada ya kufikia mafanikio makubwa na mapinduzi ya viwanda vya ndani, yalionekana kwa mara ya kwanza mwaka 1985, baada ya mabadiliko ya kisiasa, kiuchumi na kisera nchini, kuelekea mfumo huria. 

Ni uamuzi ambao nyuma yake ulisukuma na mageuzi ya kidunia, kwenye kusukumana dola kuu mbili; Magharibi waumini wa mfumo huria chini ya ngome yao NATO na Mashariki chini ya mfumo hodhi, wakiongozwa na iliyokuwa Jamhuri ya Muungano wa Kisovieti (USSR), wakiwa na ngome ya Warsaw Pact, wakizibeba hadi nchi za Ulaya Mashariki. 

Ni bahati mbaya ngome hiyo ilianguka na dunia ikabakiwa na mbabe mmoja pekee, upande wa NATO, chini ya kiongozi wao Marekani. 

Nchini katika mageuzi hayo, hatua mojawapo ilikuwa kubinafsisha ‘SU’, imudu kasi ya shinikizo la mageuzi kuelekea soko huria lililofunguliwa milango kitaifa. 

Rais Ali Hassan Mwinyi, aliyebatizwa  ‘Baba wa Mageuzi’ aliyajengea mazingira mageuzi, ikiwamo ya kisheria na kisera, hasa Mzee Mwinyi alipotumikia muongo wa pili wa uongozi wake, kukafanyika marekebisho mengi kisheria na kisera. 

Baadhi ya mabadiliko kisheria yalitumika sana katika mageuzi hayo, mojawapo ni katika tafsiri ya shirika la umma, kubaki zinazohusika na uzalishaji au uchumi pekee. 

Mageuzi hayo ya kisheria na kisera, mengi yalionekana kati ya mwaka 1991 na 1995 ikiwamo sheria nyeti za fedha, pia benki na mrithi wake, Rais Benjamin Mkapa, akayaendeleza kukamilisha mazingira yaliyoanzishwa na  Mzee Mwinyi. 

Rais Mkapa mwaka 1999, aliunda Tume ya Rais ya Kurekebisha Mashirika ya Umma (PSRC), kufanikisha majukumu makuu manne katika namna ya kuzibinafsisha ‘SU’. 

Kwanza, ni mashirika yaliyosuasua, hisa nyingi aliuziwa mwekezaji na sehemu chini ya asilimia 50 zikawa za serikali na wananchi waliouziwa. 

Kwa mashirika yaliyofanya vibaya sana, hisa zote ziliuzwa kwa wawekezaji wayaendeleze. Aidha, kukawapo mashirika maalum kimkakati kwa uchumi wa taifa, ubinafsishaji wake ukawa wa kipindi maalum na baada ya hapo, hisa zote kurudi serikalini, nchini ilifanyika kwa Shirika la Reli Tanzania (TRC). 

Aina ya nne ya mfumo huo, ni kwamba kuna baadhi ya taasisi kama vile Kiwanda cha Uchapishaji cha Taifa (KIUTA), hisa zake waliuzwa watumishi wake wanaokiendesha kiwanda, wakiwa wana mmiliki wake, maarufu kwa jina la MEBO (Management by Ownership). 

Hata hivyo, mradi huo wa mageuzi kitaifa ulioratibiwa na PSRC hakufanikiwa sana, kukijumuishwa hujuma na taasisi nyingi zilizobinafsishwa, hazikutimiza malengo. 

Mfano katika TRC, mwekezaji kutoka India alionyesha udhaifu ndani ya miaka michache katika mkataba wa miaka 20, hata serikali kuuvunja mkataba wake. Ndio sura iliyotwala katika ‘SU’ nyingi.

 Ni sababu mojwapo, eneo maarufu la viwanda Dar es Salaam wakati huo, Barabara ya Nyerere, sasa ni ya taasisi za kibiashara. 

Wakati Rais Mkapa akiendesha gurudumu la mageuzi kwa mkono wa PSRC nchini, hatua hizo hazikutoa matunda makubwa kwa mageuzi yaliyotarajiwa, nyingi zilikwama, kushindwa kuhimili kasi soko la kigeni lililofunguliwa milango na baadhi zilitoweka au kubadili majukumu. 

Mambo makuu kadhaa yalishuhudiwa kuwa sababu: kushindwa kuhimili nguvu ya soko la kigeni, teknolojia, mitaji, wimbi la mageuzi kidunia, uwezo mdogo wa uzalishaji kwa gharama ndogo na ubora duni wa bidhaa nchini.   

DIRA YA DK. SAMIA  

Inapoangaliwa kwa kina anachotekeleza Rais Dk. Samia leo ndani ya mageuzi ya mashirika ya umma ni matumizi ya darasa lake hasa kutoka mfumo hasa Serikali ya Awamu ya Pili na Tatu, aliyoishuhudia akiwa ameshahitimu elimu yake chuoni yenye unasaba na biashara. 

Eneo mojawapo analoliweka wazi ni staili ya marehemu Rais Mwinyi wa Awamu ya Pili, kuwa na utekelezaji wa kutokukumbatia mashirika yanayosuasua, kama ilivyokuwa mwongozo wa PSRC. 

 Ni hoja iilyowahi kuanikizwa na Rais Mkapa alipoingia madarakani, akizama zaidi katika mitazamo iliyoasisiwa na Rais Mwinyi kuelekea mfumo huria, kwamba serikali itabaki na majukumu yake ya msingi, kuratibu biashara na uzalishaji na si kuingilia kati. 

Hayo yanabeba ushuhuda wiki hii, pale Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu alipotangaza haja ya serikali kuachana na mashirika 30 hadi 40 yanayojiendesha kwa hasara, huku Rais naye juzi akatolea ufafanuzi kikaoni Arusha. 

Rais akasisitiza haja ya taasisi kuwa na ubunifu katika miradi yake, akituhumu uwekezaji butu usiofanyiwa utafiti unavyoipa serikali mzigo, akitoa mifano ya majengo ya Benjamin Mkapa Tower, pia Ubungo Plaza, yote ya Dar es Salaam, kwamba ni hasara ya mtaji. 

Pia akatumia nafasi ya kutetea staili ya ubunifu katika kujiendesha, akiwa na mfano wa mamlaka inayosimamia maji mkoani Tanga kufikia ubunifu wa kupanua pato kujiendesha, mwisho wake inatanua wigo wa mapato kujiendesha. 

Ndani ya mtazamo huo uliokuwapo katika serikali ya Awamu ya Pili, Rais Dk. Samia anahimiza mahitaji ya sasa kwa taasisi za umma, hasa watendaji wake wakuu na viongozi waandamizi, watanue wigo wa kuelewa ikiwamo kwa mafunzo, wakikaribisha ushirikiano kutoka taasisi binafsi. 

Kimsingi, ni urithi unaanzia katika Serikali ya Awamu ya Nne ilipoamua rasmi kufanya kazi ya kina, aina hiyo ya uhusiano ikiwamo kibiashara, ilipopitishwa Sera na Sheria ya Ushirikiano kati ya Sekta za Umma na Binafsi (PPP). 

Ndani ya mtazamo huo, Rais Dk. Samia, anazihimiza mamlaka zinazohusika serikalini, kuangalia haja ya taasisi wanazohisi tija zake ni mzigo, ama hisa kuunganishwa au kuuzwa, kurejesha uzalishaji wenye tija kimasoko.

 Katika dira hiyo ikihusiana na mtaji ya umma kwa maslahi ya sasa, Rais anasisitiza kuwapo mtaji wa umma unaojitegemea, wenye tafsiri pana kwa uchumi wa sasa kitaifa na iendako, uitwao ‘Sovereign Fund,’ akinena ni mfumo unaotawala duniani sasa.  

Hilo analioanisha na haja ya ubunifu wa kiserikali unaohitaji sasa kuvutia fedha za kigeni ndani kuingia nchini, jambo litakaloiwezesha serikali katika eneo hilo, akisisitiza mageuzi ya mashirika ya umma kuwa endelevu.

 Kimsingi, wanachoelekezwa wakuu hao wa ‘SU’, pia utendaji wake Rais katika eneo hilo, hayupo mbali na orodha ya miongozo yake kisiasa na kiutawala, kufanikisha uchumi wa nchi katika nyenzo ya taasisi hizo.