Rekodi 10 kali za raundi ya 7 Ligi Kuu

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 07:28 AM Oct 07 2024
news
PICHA: MTANDAO
Kiungo mshambuliaji wa Yanga, Pacome Zouzoua, akitafuta mbinu za kumtoka beki wa Pamba Jiji, Pauline Kasindi, katika mchezo wa raundi ya saba ya Ligi Kuu, uliochezwa Alhamisi iliyopita kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

LIGI ya soka Tanzania Bara imeingia kwenye raundi ya saba, timu nyingi zikiwa zimefikisha michezo hiyo, zingine zikibaki na viporo kwa baadhi ya mechi za raundi za nyuma kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo kushiriki michezo ya kimataifa, hususan, Simba, Yanga, huku Azam na Coastal Union zikiwa zimeshamaliza viporo vyao baada ya kuaga kimataifa.

Ligi hiyo imesimama kwa wiki mbili kupisha Kalenda ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA), ambapo baadhi ya wachezaji watakwenda kuunda vikosi vya timu zao za taifa.

Baadhi ya wachezaji wa Tanzania wamekwenda kwenye kambi ya Timu ya Taifa ya Taifa Stars kwa ajili ya kujiandaa na mechi dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, kusaka tiketi ya kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025, zitakazofanyika nchini Morocco.

Wakati ligi imesimama, mechi nyingi za raundi ya saba zilizomalizika wiki hii zimeweka rekodi kadhaa kwa timu mbalimbali.

Katika makala haya tunakuletea rekodi hizo na zingine zilizowekwa hadi kufikia raundi hiyo, twende sasa... 

1# Yanga ushindi asilimia 100

Yanga hadi kufikia raundi ya saba ndiyo timu pekee ambayo imeshinda michezo yote iliyocheza na kutoruhusu wavu wake kuguswa. Ushindi wa mabao 4-0 iliyoupata Alhamisi iliyopita dhidi ya Pamba Jiji FC, kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, umeifanya kushinda michezo yote minne mfululizo.

Mbali na hilo, Yanga ndiyo timu pekee mpaka sasa haijaruhusu wavu wake kuguswa kwenye Ligi Kuu msimu huu, ikicheza mechi nne, kushinda zote, imefunga mabao manane, haijaruhusu bao, ikishika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu. 

2# Simba imefunga mengi nyumbani

Simba ndiyo timu iliyofunga mabao mengi ikicheza kwenye uwanja wake wa nyumbani hadi kufikia raundi hiyo. Sare ya mabao 2-2 nyumbani, Ijumaa iliyopita dhidi ya Coastal Union, Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam, imeifanya kufikisha mabao tisa ya kufunga kwa michezo mitatu tu iliyocheza.

Imeyapata kwa kuifunga Tabora United mabao 3-0, Fountain Gate 4-0 na sare ya Ijumaa zote zikichezwa kwenye uwanja huo uliopo, Mwenge Dar es Salaam, na kuzipiga kumbo timu zote za Ligi Kuu.

 3# Namungo haijapata sare

Namungo ndiyo timu pekee ambayo mpaka sasa haijapata sare yoyote kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara hadi kufikia raundi ya saba. Timu hiyo ambayo imecheza michezo sita, ikiwa na kiporo kimoja, imeshinda michezo miwili na kupoteza minne.

Hadi ligi inakwenda mapumzikoni, inakamata nafasi ya 12 kwenye msimamo ikiwa nafasi ya sita.

 4# Fountain Gate mabao mengi ugenini

Timu ya Fountain Gate imefunga mabao mengi ikicheza ugenini kuliko nyingine yoyote kwenye Ligi Kuu mpaka sasa. Imefunga mabao saba ikicheza nje ya uwanja wake wa nyumbani, idadi ambayo haijafikiwa na timu yoyote.

 5# JKT Tanzania, Mashujaa zafungwa

Michezo ya raundi ya saba ya Ligi Kuu, imeshuhudia timu za Mashujaa FC na JKT Tanzania zikipoteza mechi zao kwa mara ya kwanza.

Baada ya kucheza michezo mitano, ikishinda miwili na sare tatu, Mashujaa ilipata kipigo cha kwanza tangu kuanza kwa ligi dhidi ya KenGold kwa bao 1-0, mechi iliyochezwa, Ijumaa iliyopita, Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

JKT Tanzania ambayo ilicheza pia michezo mitano ilipata kipigo kwenye mechi ya sita, ilipolala bao 1-0 nyumbani, Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma dhidi ya Singida Black Stars.

Timu zote mbili zimepoteza michezo yao zilipocheza mechi zao za sita, lakini zikiwa raundi ya saba.

 6# Pamba Jiji haijui utamu wa ligi

Pamba Jiji ndiyo timu pekee kwenye Ligi Kuu ambayo haijaonja ushinda mechi yoyote mpaka sasa.

Licha ya kucheza michezo saba kwenye Ligi Kuu, haijaonja utamu wa ligi, ikicheza kwa mara ya kwanza baada ya miaka 22. Timu hiyo inayoburuza mkia, imetoa sare mechi nne, kupoteza mitatu.

 7# KenGold, Prisons zaona mwezi

Hatimaye timu za Kengold na Prisons zote za Mbeya, zimeshinda michezo yake ya kwanza kwenye raundi ya saba ya Ligi Kuu.

KenGold, ambayo ilicheza mechi zake sita za kwanza, ikiwa ni mara yake ya kwanza Ligi Kuu bila kupata ushindi wowote, hatimaye ilipata ushindi, Ijumaa iliyopita, Uwanja wa Sokoine, Mbeya, ilipoichapa JKT Tanzania bao 1-0. Kabla ya hapo ilikuwa imepoteza mechi tano mfululizo za kwanza, kabla ya kutoka sare moja, na baada ya hapo ikapata ushindi.

Prisons, baada ya sare nne mfululizo, kabla ya kupoteza moja, hatimaye ilipata ushindi wake wa kwanza, Jumanne iliyopita wa mabao 3-2 dhidi ya Fountain Gate, mechi iliyochezwa, Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

 8# Singida BS ugenini kama nyumbani

Singida Black Stars ndiyo timu iliyozoa pointi nyingi ikicheza viwanja vya ugenini hadi kufikia raundi ya saba.

Timu hiyo ambayo imecheza michezo sita, imeshinda mechi zote nne ilizocheza ugenini, ikikusanya pointi 12, huku ikicheza mechi mbili tu nyumbani, ambazo imeshinda moja na kutoa sare moja, ikipata pointi nne. Inaongoza ligi ikiwa na pointi 16 mpaka sasa.

 9# Simba sare ya kwanza, yaruhusu mabao

Sare ya mabao 2-2 iliyoipata Simba, Ijumaa iliyopita, Uwanja wa KMC Complex, imeifanya timu hiyo kupata sare ya kwanza kwenye Ligi Kuu baada ya kushinda michezo minne ya kwanza.

Pia imeruhusu wavu wake kuguswa mara ya kwanza, kwani kabla ya mchezo huo, ilikuwa haijaruhusu bao. Inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu, ikiwa na pointi 13, sawa na Fountain Gate, lakini ina tofauti nzuri ya mabao ya kufunga na kufungwa.

 10# Fountain Gate, fowadi wembe, beki njia

Fountain Gate ndiyo timu pekee iliyofunga mabao mengi kwenye Ligi Kuu kuliko timu nyingine yoyote.

Imeshapachika mabao 14 mpaka sasa. Hata hivyo, ndiyo timu iliyoruhusu mabao mengi zaidi wavuni kwake. Imesharuhusu mabao 12 mpaka sasa na inakamata nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi hiyo, ikiwa na pointi 13.