Katibu Mkuu CCM ampigia simu waziri akatatue kero

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 09:59 AM Oct 07 2024
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi.
Picha:Mtandao
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi.

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi jana alimpigia simu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa kutaka ufafanuzi wa lini soko na stendi vitajengwa Lamadi, mkoani Simiyu.

Balozi Dk. Nchimbi, akiwa katika siku ya kwanza ya ziara yake ya siku saba mkoani Simiyu, wakati akihutubiwa wananchi katika mkutano wa hadhara, alielezwa kero kuu zinazowasumbua na kuwakwamisha kwenye utekelezaji wa majukumu yao. 

Akitoa ufafanuzi huo, Waziri Mchengerwa alisema: "Rais Samia Suluhu Hassan amezingatia malalamiko hayo na alituelekeza kuhakikisha eneo hilo zinapelekwa fedha za ujenzi wa soko na ujenzi wa barabara. 

"Lakini pia kwa kuwa kuna ukimya  tutakuwa hapo (Lamadi) kuanzia mwezi ujao kuona namna gani tutakwenda kufanya maboresho kwa sababu fedha tulionayo kwa sasa ni ya ujenzi wa soko la kisasa na barabara kwa kiwango cha lami  urefu wa kilomita nane," alisema Mchengerwa. 

Aliongeza kuwa wataalamu watakaokwenda, wataangalia uwezekano wa kufanya tathmini na kuongeza ujenzi wa stendi na kwamba kuanzia mwezi ujao wanategemea kutangaza zabuni ya kuanza ujenzi wa soko la kisasa na barabara. 

Aliwahakikishia wananchi wa Lamadi kwamba changamoto zao zitatatuliwa na suala la stendi amelichukua na wanaangalia uwezekano wa kulijumuisha wakati wa ujenzi wa soko na barabara.

Akikata simu ya Mchengerwa, Balozi Dk. Nchimbi alirusha dongo kwa vyama vya upinzani kwamba havina mipango thabiti ya kuongoza nchi. 

"Kiongozi madhubuti anazungumzia mipango ya kuongoza nchi. Lakini vyama vya upinzani wakipata nafasi wanazungumza maandamano, kuchana kanga na kuzomea. 

"Viongozi wa CCM wanaandaliwa, hakuna kiongozi ndani ya chama atakaa miaka 40. CCM kitaendelea kuwa chama kijana zaidi kwani kina viongozi vijana na wazee wenye kuwalea vyema," alisisitiza.

 Alitoa wito kwa wananchi hao kuendelea kushirikiana na CCM, akisisitiza chama hicho kimeendelea kuonesha nia njema katika kuwatumikia wananchi. 

Kuhusu Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi ujao, Katibu Mkuu alitoa rai kwa wananchi kujitokeza kwa wingi, akitamba kuwa chama chake kitateua wagombea wenye kujali changamoto za wananchi na si maslahi binafsi. 

"Ikifika muda wa kujiandikisha, tujitokeze kwa wingi kujiandikisha katika Daftari la Wakazi kuanzia Septemba 11 hadi 20, 2024 ambalo litahusika katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Novemba 27, 2024. Daftari la Kudumu la Wapigakura ni kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu 2025," alibainisha. 

Katika hatua nyingine, Balozi Dk. Nchimbi alisema CCM itachangia Sh. milioni mbili kuunga mkono ujenzi wa vituo vya madereva bodaboda katika Mji wa Lamadi baada ya kundi hilo kulalamika linateseka na jua wakati wa kutafuta ridhiki. 

Katibu wa NEC Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa, Amos Makalla alisema mkoa wa Simiyu ni wa 18 kufanya ziara za kikazi na kukagua utekelezaji ilani na kusikiliza kero za wananchi. 

Mbunge wa Busega, Simon Lusengekile alisema eneo lake lina changamoto ya viboko na tembo kuvamia makazi ya wananchi na kuharibu rasilimali zao na kuomba serikali iruhusu wavunwe ili wananchi wanaozunguka ziwa, wawe salama.  

Balozi Dk. Nchimbi alimwahidi kulifikisha suala lake kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dk. Pindi Chana ili changamoto hiyo itafutiwe ufumbuzi. 

Kada wa CCM aliyejiengua akitokea Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Peter Msigwa alisema Tanzania iko salama chini ya uongozi wa chama hicho na kwamba wanaodhani vyama vya upinzani vitawaletea maendeleo, wafumbue macho kwa kuwa vyama hivyo vimebaki kile alichokiita kulialia. 

Katibu wa NEC Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Rabia Abdallah Hamid aliwataka vijana kujituma na kufanya kazi za kuwaingizia kipato, akiwahimiza kuchangamkia fursa ya mikopo ya asilimia 10 inayotarajiwa kuanza kutolewa muda wowote kuanzia sasa.