SAKATA BINTI WA YOMBO: 'Afande' kupanda kizimbani leo

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 09:54 AM Oct 07 2024
Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma.
Picha: Mtandao
Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma.

FATMA Kigondo anayetuhumiwa kuwatuma vijana kumbaka kwa kundi na kumwingilia kinyume cha maumbile binti mkazi wa Yombo Dovya, jijini Dar es Salaam, leo anatarajiwa kufikishwa kupanda kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma kujibu mashtaka yanayomkabili.

Septemba 5, mwaka huu, mahakama hiyo iliahirisha shauri lililofunguliwa na Wakili Paul Kisabo dhidi ya Afande Fatma kutokana na hakimu aliyekuwa anasikiliza shauri hilo kuhamishwa kituo cha kazi huku shauri hilo likiwa halijapangiwa hakimu mwingine.

Kesi hiyo ilipangwa kusikilizwa Septemba 5 mwaka huu katika mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Fransis Kishenyi, afande huyo akikabiliwa na shtaka kuwasaidia wahalifu kutenda kosa la ubakaji kwa kundi.

Akizungumza nje ya mahakama hiyo baada ya kuahirishwa kwa shauri hilo, Wakili Kisabo aliyefungua mashtaka hayo dhidi ya afande huyo, alidai ni kuhamishwa kituo cha kazi kwa hakimu aliyepangiwa kesi.

"Lakini leo kama mlivyoona, mshtakiwa tayari amefikishwa mbele ya mahakama na kusomewa mashtaka yanayomkabili," alidai wakili huyo.

Katika kesi namba 23476 ya mwaka 2024 ya ubakaji kwa kundi na kumwingilia kinyume cha maumbile iliyokuwa ikisikilizwa na Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, ilitolewa hukumu yake Septemba 30 mwaka huu.

Katika hukumu hiyo washtakiwa wote walikutwa na hatia na kuhumumiwa kifungo cha maisha gerezani na kutakiwa kulipa Sh. milioni moja kila mmoja.

 Waliohukumiwa kifungo hicho ni pamoja na aliyekuwa askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), MT 140105, Clinton Damas, maarufu Nyundo, aliyekuwa askari Magereza C.1693 Praygod Mushi, Nickson Jackson, maarufu Machuche na Amin Lema, maarufu Kindamba.

Wote kwa pamoja walikuwa wanakabiliwa na mashtaka ya kubaka kwa kundi na kumwingilia kinyume cha maumbile binti wa Yombo Dovya, jijini Dar es Salaam aliyetambulishwa kwa jina la XY.