Madaktari wamlilia Prof. Shao, mwanamageuzi wa tiba nchini

By Salome Kitomari , Nipashe
Published at 10:09 AM Oct 07 2024
Aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya KCMC na Makamu Mkuu wa kwanza wa Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira mstaafu, Prof. John Shao (80).
Picha: Mtandao
Aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya KCMC na Makamu Mkuu wa kwanza wa Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira mstaafu, Prof. John Shao (80).

MADAKTARI wamesema aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya KCMC na Makamu Mkuu wa kwanza wa Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira mstaafu, Prof. John Shao (80), ameacha alama kubwa.

Akimzungumzia Prof. Shao aliyefariki jana hospitalini KCMC, Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk. Mugisha Nkoronko, alisema ameacha alama kubwa na isiyofutika katika sekta ya afya kukiwa na mageuzi makubwa, ikiwamo idadi kubwa ya madaktari wabobezi. 

Alisema kuwa Prof. Shao alikuwa miongoni mwa madaktari wa kwanza kusoma shahada ya magonjwa ya vimelea mbalimbali, akiwa mkufunzi katika Chuo Kikuu cha Tiba Muhimbili.

“Ni mwanamageuzi wa sekta ya afya, alishiriki mageuzi wakati tunaingia katika mpango wa kuruhusu sekta binafsi kuendesha shughuli za kijamii ikiwamo afya. Baada ya sheria kupitishwa kuruhusu sekta binafsi kuwekeza mwaka 1995 ndio walikuwa wa kwanza kuanzisha chuo kikuu binafsi cha kwanza cha Tumaini na Chuo Kikuu cha Tiba, Kitivo cha KCMC akiwa mkuu wa chuo wa kwanza," alisema.

Aliongeza: "Akiwa Mkurugenzi wa KCMC, tulishuhudia alisomesha madaktari, madaktari wote unaowaona leo walishawishiwa na yeye kusomea ubingwa na ubobezi walionao sasa hivi. Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dk. Peter Kisenge ni matunda ya dhati ya Prof. Shao,” alisema rais huyo.

Alisema kuwa Prof. Shao alianzisha Kituo cha Utafiti (KCRI), ambacho alikianzisha kwa kushirikiana na wadau, akianzisha pia maabara ya bayoteknolojia, iliyoshirikI katika utafiti wa udhibiti wa malaria duniani chini ya Mpango wa Bill & Melinda Gate. 

“Ameacha alama nyingi katika afya, ukiona taasisi ya tiba za njia ya mkojo pale KCMC ni yeye, huwezi kuitaja bila kumtaja Prof. Shao. Uchunguzi wa magonjwa ya tumbo kwa kutumia kamera maalum inayomezwa ni yeye,” alisema. 

Pia alisema ameshiriki utafiti wa matibabu ya kifua kikuu (TB) kwa kushirikiana na Hospitali ya Rufani ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi Kibong’oto, mkoani Kilimanjaro na alianzisha kliniki shirikishi ya VVU na Ukimwi kwa familia. 

Dk. Mugisha alisema kwa kushirikiana na viongozi wengine, walisababisha kukawa na CT Scan ya kwanza kwa Kanda ya Kaskazini.

 "Pia alishirikii mageuzi ya kisera na kimuundo, alifanikisha uanzishwaji Mpango wa Elimu ya Madaktari (MEPI), ndio kiini cha ushirikiano baina ya Chuo Kikuu cha Duke Marekani na KCMC, na Chuo Kikuu Radbound Nijmegen cha Uholanzi. 

Taarifa ya tanzia iliyotolewa kwa umma jana na Katibu Mtendaji wa Shirika la Msamaria Mwema (GSF) na Mkurugenzi Mtendaji wa KCMC, Prof. Gileard Masenga, ilieleza kuwa Prof. Shao alikutwa na umauti jana Oktoba 6, 2024. 

Prof. Shao alizaliwa mwaka 1944, ni mtanzania wa kwanza kuwa na shahada ya magonjwa ya vimelea vya magonjwa mbalimbali, aliwahi kuwa mkufunzi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1978-1981, Mshauri wa wanafunzi UDSM kuanzia 1981-1986, Profesa Mshiriki mwaka 1982-1990 na Profesa tangu 1986.

 Tangu mwaka 1994, alikuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Umoja wa Madaktari Afrika, mwaka 1992 alikuwa mjumbe wa Kamati ya Mabadiliko ya Sekta ya Afya Tanzania na Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania mwaka 1990-1992. 

Bwana alitoa na Bwana ametwaa. Jina la Bwana lihimidiwe.