UCHAGUZI wa Mwenyekiti wa Tume ya Afrika (AUC), unaomalizika hivi karibuni umeendelea kuonyesha namna uhusiano ulioanzishwa na ukoloni unavyoendelea kusimamia mipango mingi ya Afrika.
Matokeo yamempa ushindi Mahamoud Ali Youssouf (59), wa Djibout aliyepata kura chache za ushindi dhidi ya Raila Odinga (80), kutoka Kenya.
Kwa mara ya tatu mfululizo kamisheni au tume ya Afrika inaongozwa na viongozi kutoka mataifa yaliyotawaliwa na Ufaransa maarufu Francophone dhidi yale yanayozungumza Kiingereza Anglophone, kutokana na kutawaliwa na Waingereza.
Kwa hiyo Mwenyekiti wa sasa ni Youssouf kutoka Djibouti na Makamu wake ni Selma Malika Haddadi kutoka Algerian. Wote wanatoka kwenye mataifa yanayozungumza Kifaransa, wakichaguliwa katika uchaguzi uliomalizika Jumatatu wiki hii.
Mwenyekiti wa kwanza na msimu wa uongozi kwenye mabano alikuwa Jean Ping (2008 hadi 2012) kutoka Gabon.
Aliyeshika wadhifa huo baada ya Ping ni Nkosazana Dlamini-Zuma (2012 hadi 2017), Kutoka Afrika Kusini.
Anayeondoka madarakani wiki hii ni Moussa Faki Mahamat kutoka Chad. Akianza kazi 2017 na kuhitimisha Februari 2025.
Yako mambo muhimu yaliyombeba Raila na mpinzani wake, Youssouf, wakati wa mchakato wa uchaguzi kuanzia awamu wa kwanza hadi ya saba, kwa utaratibu uliotumika.
Mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Abdulkarim Atiki, akizungumzia uchaguzi huo, anasema Raila ameshindwa kutokana na hesabu zilizopigwa.
“Ameshindwa kimahesabu, hakukuwa na sababu ya wanaozungumza Kiingereza kuweka mgombea mmoja, Madagascar alipotolewa kura zake zikaenda kwa Djibouti.
Ushindi huo ni wa Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa anayetaka Umoja wa Afrika (AU) umsaidie kujenga mahusiano na makoloni yake ya zamani, anaeleza.
Wakati huohuo, uchambuzi wa vyombo vya habari kimataifa kama DW pamoja na wachambuzi wa kisiasa, wanataja mambo kadhaa yaliyomwangusha Raila, kwenye kinyang’anyiro hicho.
Kwanza ni jamii ya Kifaransa ambayo iliungana kumuunga mkono mtu wao Youssouf. Pili, inadaiwa kulijitokeza mgawanyiko ndani ya wadau wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).
Tatu, kilichotia doa kwa Raila ni vurugu za vijana waliojiita ‘Gen Z’ huko Kenya, suala ambalo lilisababisha kumwangusha. Mwaka jana mwishoni wakati ndio kipindi cha kuomba kura, machafuko yalipamba moto nchini mwake.
Suala la nne, linalotajwa ni umri mkubwa wa miaka 80 huku mpinzani wake akiwa na miaka 59 ndiyo maana akawekwa pembeni.
Mchakato wa kupiga kura ulikwenda hadi awamu sababu. Matokeo ya awamu ya sita yalionesha Youssouf kupata kura 26, Kenya ikipata kura 22. Hakukuwa na kura iliyoharibika huku taifa moja likiacha kupiga kura.
Awamu ya mwisho Raila alidondoshwa kwa kura tatu dhidi ya mpinzani wake, Youssouf Waziri wa Mambo ya Nje wa Djibouti, akatangazwa mshindi.
AKUBALI YAISHE
Raila, Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya, anapozungumza kwa mara ya kwanza baada ya kutangazwa kushindwa, huko Addis Ababa, Ethiopia, anampongeza Youssouf, kuibuka mshindi akasema:
"Ninakubali matokeo ya kura. Kwa hivyo mwenyewe ninakubali kushindwa. Wanasema kwamba lazima tuimarishe demokrasia katika bara letu ninataka tutumie hii kama mfano mwema," Raila anasema.
"Hivyo basi, namtakia mshindani mwenzangu Mahmoud Ali Youssouf kila la kheri na mafanikio katika kazi yake".
Raila anawashukuru waliompigia kura na ambao hawakumpigia: “Kwa sababu wametumia vyema haki zao za kidemokrasia," akasema.
Raila Odinga anaongeza kwamba alikuwa tayari kwa kila hali, itakayotokea au kushinda ama kushindwa kabla ya uchaguzi.
"Sina machungu. Nina furaha sana na kama haitoshi, bado ninapatikana kutoa huduma yoyote kwa bara hili katika uwezo mwingine wowote," alisema.
Akagusia safari yake ya kampeni na kukiri kuwa alisafiri maeneo mengi barani Afrika, kujitangaza.
"Nilijitolea kama mgombea na kwa miezi kadhaa iliyopita nimetembea maeneo mbalimbali kukutana na viongozi, nikiwadai wanipigie kura. Leo wamejieleza hali ilivyo, ni kwamba hatukufanikiwa," anasema.
Raila anasema hitaji ni kuimarisha usawa katika bara hili. "Ninashukuru sana kwa zoezi la leo. Ninawashukuru watu wa Afrika."
Alipoulizwa na wanahabari nini kinafuata, Raila anasema: "Sasa nitarudi nyumbani, kuna mambo mengi ya kufanya".
Alizungumzia changamoto inayoendelea kukabili eneo la Afrika kwa sasa, mzozo wa DR Congo.
"Suala la DRC bado linaendelea kuwa tata. Mateso tunayoshuhudia hayakubaliki kabisa. Watu wasiokuwa na hatia wanauawa, watoto, wanawake na kadhalika. Lazima isitishwe," anasema.
Ingawa huko Kenya wachambuzi wa siasa wanasema ushindi wa Raila, ungepiga jeki azma ya Rais William Ruto kuwania tena urais 2027.
Hii ni kwa sababu Ruto angekuwa mgombea mwenye nguvu zaidi, wakati kiongozi wa upinzani hayupo kwenye ulingo wa siasa.
Tayari Kiongozi wa Taifa anafurahia kuungwa mkono mkubwa sana kutoka kwa wakazi wa Nyanza hasa alipozuru eneo hilo.
Hivi karibuni, Seneta wa Siaya Oburu Oginga anadokeza kuwa chama cha ODM kinaweza kuwa na mgombea wa urais 2027.
Tangazo hilo linaibua wasiwasi kuhusu uwezekano wa Chama cha Orange au Chungwa kumuunga mkono Rais Ruto atakapotafuta muhula wa pili Ikulu.
Oginga, ambaye ni kaka yake Raila, anasema kinara huyo wa ODM angali na uwezo wa kuwania urais.
“Tutakuwa na mgombea wetu wa urais kama ODM na iwapo kutakuwa na haja ya muungano na vyama vingine vyenye mawazo sawa, tutaamua anayewania kwa pamoja. Lakini tutatoa uamuzi muda ukifika,” anasema.
Baada ya uchaguzi wa AUC, Mwenyekiti wa ODM Gladys Wanga, anachapisha kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Facebook: “Baba, bado wewe ni Baba kila wakati”.
BBC/TAIFA LEO
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED