Polisi Dar wajitosa mtaani vita ukatili unaoendelea kwa watoto

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 07:57 AM Aug 29 2024
Polisi wakiwa katika mafunzo, kabla ya ya kutawanywa kufanya kampeni ya kupambana na ukatili wa kijinsia kwa Watoto, wilayani Ilala.
PICHA: SABATO KASIKA
Polisi wakiwa katika mafunzo, kabla ya ya kutawanywa kufanya kampeni ya kupambana na ukatili wa kijinsia kwa Watoto, wilayani Ilala.

MATUKIO ya ukatili wa kijinsia, ni miongoni mwa yale yaliyoshamiri ndani ya jamii yakiumiza makundi mbalimbali, wakiwamo watoto wadogo.

Kutokana na mazingira hayo hatarishi, Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Ilala Dar es Salaam, limeamua kuanzisha kampeni ya miezi sita ya kuwaepusha na vitendo hivyo, vikiwamo ulawiti na ubakaji. 

Ni kampeni iliyopewa jina 'Tuwaambie Kabla Hawajaharibiwa', iliyoanza wiki iliyopita na inatarajiwa kuhitimishwa Februari mwaka ujao. 

Mbali na shule za msingi, sekondari na vyuo, kampeni hiyo itafikishwa katika nyumba za ibada, pia kwenye vijiwe mbalimbali, vikiwamo vya bodaboda. 

Mratibu wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa utendaji kazi askari wa madawati ya jinsia na watoto mkoa huo wa kipolisi, Inspekta wa Polisi, Dk. Christina Onyango, ndiye anayesema wakati wa kufunga mafunzo hayo mjini Dar es Salaam, wiki iliyopita. 

Anasema, matukio mengi yanayoripotiwa katika vituo vya mkoa huo ni ya ulawiti na ubakaji na kwamba, wameona waanzishe kampeni ya kutoa elimu itakayosaidia kuepuaha makundi hayo na ukatili huo, ili kunusuru kizazi kijacho. 

"Tutatoa elimu kwa wanafunzi wa shule za msingi na wote wa vyuo, lakini wa sekondari ni kwa kidato cha tano na sita," anasema. 

JINSI ITAKAVYOKUWA 

Afande Dk. Christina anasema, wakuu wa madawati ya jinsi na watoto, watakuwa wanazuru katika shule za msingi, sekondari na vyuo, wakiitisha midahalo na kujadili madhara ya vitendo, wakiwapa nafasi wanafunzi kujieleza. 

"Kwa mfano, wale wa shule za msingi tunataka kuwaelimisha madhara ya ukatili wa kijinsia ikiwamo rushwa ya ngano pia," anasema. 

Anafafanuwa kuwa, wahusika hao watafundishwa pia kutambua viashiria vya ukatili wa kijinsia na namna ya kutoa taarifa, ili watuhumiwa wakamatwe na kufikishwa katika vyombo vya sheria. 

"Katika ‘vijiwe’, sehemu za biashara na nyumba za ibada, tutawaelekeza wazazi na walezi kuzingatia umuhimu wa malezi bora ili watoto waendelee kuwa salama," anasema. 

Dk. Christina anasema, baadhi ya wazazi na walezi hadi sasa wamekuwa wanazembea, wakiwaacha watoto wanajilea wenyewe, huku ndugu wa karibu  wakihusika katika vitendo hivyo. Kwa hiyo tunataka wajue umuhimu wa malezi bora," anasema. 

Anafafanua kuwa mmomonyoko wa maadili ni tatizo kwa nchi nzima, akiamini katika eneo lake askari wenzao wa mikoa mingine wako kwenye mikakati ya kufanya kampeni kama hiyo. 

ANGALIZO KWA POLISI 

Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Kipolisi wa Ilala. ASP Gloria Urassa, anatoa angalizo kwa polisi wa dawati hilo watakaoenda kufanya kampeni hiyo, wazingatie maadili kwa kufuata kaulimbiu ya jeshi hilo anayoitaja kuwa ni nidhamu, haki na weledi. 

"Ili askari aonekane ana nidhamu, tunazingatia mambo kadhaa kama uvaaji wake, kuwahi kwenye tukio, kutoleta taharuki kwenye jamii, kwani tumekuwa tukifanya kazi kwa watu walioumizwa kimwili na kisaikolojia," anasema ASP Glory. 

Anasema, askari hapaswi kuchanganya mambo yake ya nyumbani anapokuwa anashughulikia sera za madawati ya jinsia au kutanguliza urafiki ama upendeleo, bali azingatie haki, nidhamu na weledi. 

 "Huko mnakokwenda kufanya kampeni, mtaletewa waathirika wa ukatili wa kijinsia, hivyo, ni muhimu mtumie weledi wenu vizuri mnapojadiliana nao. Lugha nzuri kutoka kwa askari wa dawati la jinsia ni ya muhimu." anasema. 

Aidha, anasema mkoa huo una wilaya za kipolisi tano za Buguruni, Kariakoo, Chanika, Ukonga na Kati zikiwa na madawati tisa ya jinsia na watoto.

 Mratibu wa Diwani la Usalama Wetu Kwanza, wilaya ya Kipolisi ya Kariakoo na Kati Mkaguzi wa Jeshi la Polisi, Japhet Shilla, anasema malezi duni na teknolojia ni chanzo cha mmomonyoko wa maadili katika jamii.

 "Wazazi na walezi hawana muda wa kusimamia malezi bora, wako 'bize' na mambo yao, watoto wamejiingiza katika mambo yasiyofaa, kwa sababu ya kukosa malezi. 

 “Hivyo, tunakwenda kuwakumbusha kila mmoja atimize wajibu wake ili kupunguza tatizo la ukatili wa kijinsia," anasema Shilla.

 Inspekta wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lydia Mrema, anasema wazazi na walezi watenge muda wa kukaa na watoto wao, pia wajenge urafiki nao ili hata watoto wanapokuwa na matatizo, wawe huru kuwaambia.

 "Watoto Wana vitu vingi wanavyokumbana navyo shuleni, mitaani na hata nyumbani, lakini hawawezi kuvisema kama wazazi na walezi hawako karibu nao," anasema Lydia.

 Mkuu wa Kituo cha Polisi Kati, ASP Sophia Dilunga, anasema bila wazazi wa kike kubadilika na kusimamia malezi ya watoto, vita dhidi ya ukatili wa kijinsia inaweza kuchukua miaka mingi.

 "Ninasema hivyo, kwa sababu sisi wanawake ndio tunaokaa na watoto kwa muda mrefu, lakini bahati mbaya hatusimamii malezi kikamilifu, tuwakumbushe hilo tunapokwenda kutoa elimu," anasema ASP Sophia.