NI mwezi mmoja uliopita, Taasisi ya L'Oréal kwa pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), zilitangaza washindi wa Tuzo za Vijana wa Talanta kwa Wanawake katika Sayansi barani Afrika.
Hapo ikawatunuku kwa mwaka jana, watafiti 30 kutoka Afrika katika nyanja ya sayansi. Hao ni wanafunzi 25 wa shahada ya uzamivu (PhD) na wanafunzi watano wa ngazi, baada ya shahada ya uzamivu kutoka nchi 15 za Afrika.
Hapo ndipo anapopatikana mwanafunzi wa shahada ya uzamivu, kutoka nchini Benin, Marie Marthe Chabi, akipaishwa na utafiti wake katika sekta ya afya, akilenga ugonjwa unaozidi kuathiri Waafrika; kisukari.
Makadirio ya Shirika la Afya Duniani (WHO), ni kuwapo watu milioni 24 wanaotaabika na kisukari barani Afrika hadi kufika mwaka 2021, matarajio yaliyoko ni ongezeko la kufika milioni 55 ifikapo mwaka 2045; ziada ya asilimia 129.
Ugonjwa huo hadi sasa, unachukuliwa kuwa janga barani Afrika, unajitokeza kwa aina mbalimbali, kwa mujibu wa WHO.
Mwanafunzi wa shahada ya uzamivu katika sayansi ya biolojia, Marie Marthe Chabi, alichagua kutafiti kisukari cha aina ya pili, akiwa na sababu:
"Najua watu wanaosumbuliwa na ugonjwa huu na lazima kutambua kuwa wengi wao wana maisha ya ‘uchochole’ (ubabaishaji) kutokana na magonjwa yanayotokana na kisukari cha aina ya pili," anasema Marie.
Mtafiti huyo anafafanua kwamba, kisukari kinatambuliwa kwa kiwango cha juu cha sukari kwenye damu na hali hiyo inapozidi, anaeleza kwamba: "Unatanuka hadi kuwa magonjwa kama ya moyo, magonjwa ya neva na hata matatizo ya macho."
Mtazamo wake kitaaluma anafafanua kuwa, kadri yanayohitajika kufuatiliwa ili kuwa na maisha bora yanavyopuuzwa, ndivyo ugonjwa unavyoendelea kuathiri na hata kuwasababishia vifo Waafrika wengi.
Marie anaendelea: "Ndio maana napigania kupambana na ugonjwa huu wa kisukari."
TIBA YA MWANGA
Ni tiba inayohusisha kutumia mwanga kwenye mwili wa mgonjwa, ili kugundua mifumo na njia za ishara zinazozuia au kupunguza ufyonzaji wa glukosi.
Unatajwa kuwa mchakato mgumu zaidi, akiongeza kuwa anazingatia anachokitaja kuwa "mwanga mwekundu, mwanga wa sumaku umeme."
"Kweli mwanga ni nishati. Ni kama jua linalotupatia joto tunapokuwa baridi. Huu mwanga una chembe ndogo zinazojulikana kama ‘photon’ ambazo hutumika kama vyanzo vya nishati kwa mitambo midogo ya nishati inayopatikana mwilini iitwayo mitochondria."
Mtu anapomulikwa na kifaa cha mwanga mwekundu au mwanga wa sumaku umeme, kwa mfano hizi nishati ndogo katika mwili, hugundua nishati hiyo ya mwanga.
“Nishati hii itasimamia njia zinazoruhusu ufyonzaji wa glukosi, ambao umekatizwa kwa watu wanaosumbuliwa na kisukari cha aina ya pili,” anasema Mtafiti Marie.
Anaendelea: "Changamoto yetu hapa ni kuonyesha kwa mwanga mwekundu. Tunaweza kurejesha njia hii ili kuboresha ufyonzaji wa glukosi na hivyo kupunguza uchochezi unaopatikana katika viungo vinavyolengwa na insulini."
GHARAMA ZA UTAFITI
Ni teknolojia inayopendekezwa na Marie itumike kwa maagizo na matibabu ya daktari, aki
sisitiza "kwa sasa, tuko bado katika hatua ya majaribio...
Tuna majaribio mengi ya kufanya. Tuna marekebisho mengi ya kufanya ili tuweze kumruhusu mgonjwa kutibiwa."
Kwa sasa, Marie anaendelea kuboresha utafiti wake kwa kufanya majaribio kwenye mifano ya wanyama.
Ili kufikia bidhaa bora ya mwisho, mtafiti anahitaji kupitia hatua tatu zinazohitaji uwekezaji mkubwa wa muda, maarifa, na hasa rasilimali za kifedha na vifaa.
Hatua ya kwanza inatajwa ni kufanyia utafiti ndani ya glasi yenye mfanano na kiumbe hai, inafanywa kikamilifu katika maabara.
Hatua ya pili, ni majaribio kwa panya na ndicho kiwango amefikia wakati wa kuandika makala hiyo.
AENDAKO SASA
Kitaalamu inatajwa iwapo Marie atafanikiwa kutekeleza hatua hizo mbili kwa kutumia rasilimali chache alizo nazo, anahitaji fedha zaidi kuendelea na hatua ya mwisho.
"Utafiti unahitaji fedha nyingi...Kwa sasa, hatujaridhika na aina ya ufadhili tulionao, lakini tunajizatiti na kile tulichonacho," anasema, akibainisha dhamira yake, inabaki ni kutokana na uzoefu wake binafsi ulioelezwa awali.
Kwa tuzo hiyo kutoka kwa Taasisi ya L'Oréal-UNESCO, Marie anafurahia kwa kauli; "Tuna matumaini kupata ufadhili zaidi ili tuendelee na hatua ya majaribio ya kliniki."
KUSHINDA VIKWAZO
Katika Afrika ya Kusini mwa Sahara, wanawake wanawakilisha asilimia 31 tu ya watafiti wanapokea mishahara midogo na mara nyingi hawatambuliwi kama wenzao wa kiume.
"Changamoto ya kwanza tunayokutana nayo, ni ukosefu wa fedha hasa katika Afrika ya Kusini mwa Sahara, Magharibi mwa Afrika, katika nchi yangu," anasisitiza Dk. Chabi.
"Hivyo, natumai kweli kuwa naweza kuvuta umakini wa watu au taasisi zinazovutiwa na mada hii ili waweze kujitolea na kuniruhusu kuafiki ubora wangu ili kutoa bidhaa halisi inayofanya kazi."
La pili linatajwa, ni imani binafsi kulingana na mwanafunzi huyo wa sayansi za baiolojia, akiwa maelezo: "Nililazimika kufanya kazi sana na kujipa motisha ili niwe na imani na nafsi yangu na ninajijua kuwa, kadri ninavyotaka jambo fulani, najitahidi nikiwa na lengo la kulifikia."
"Sijakutana na ubaguzi mwingi, lakini haina maana hakuna ubaguzi...Kila wakati ninachukua kwa umakini ushauri kutoka kwa wazee ambaye huniambia kwamba hata kama nitajitahidi, nitahakikisha kila kitu kiko shwari bado nitakosolewa na hilo nisiweke akilini,'' anasema.
“Kwa falsafa hii, naendelea na utafiti wangu, bila kujali vikwazo vilivyopo," anahitimisha mtafiti Marie.
AINA ZA KISUKARI
Dalili zake ni pamoja na kukojoa kila mara, kiu isiyokoma, njaa ya kila mara, kupungua uzito, matatizo ya kuona, na uchovu.
Aina ya Kisukari cha Pili; WHO inasema hii inatokana na uzalishaji mdogo wa insulini au mwili kushindwa kutumia insulini vizuri. Aina hiyo ya ugonjwa, ambayo awali ilikuwa inawaathiri watu wazima, WHO inasema imeenea kwa watoto wengi.
Dalili zake ni kama za aina ya kwanza, na husababishwa na uzito kupita kiasi na ukosefu wa mazoezi. Hii imeonekana kwa asilimia 95% ya watu waliogundulika na kisukari.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED