Misitu vijijini ilivyo kisima cha utajiri kwa wananchi

By Christina Haule , Nipashe
Published at 09:31 AM Oct 08 2024
Kufuga nyuki moja ya shughuli zinazofanyika vijijini.
PICHA: MTANDAO
Kufuga nyuki moja ya shughuli zinazofanyika vijijini.

KUWAPO kwa misitu ya vijiji katika mikoa mbalimbali ni fursa ya kufuga nyuki kibiashara pamoja na kutunza mazingira na kukabili athari za mabadiliko ya tabianchi.

Ni ujumbe unaoelekezwa kwa wanachama wa Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA), walio kwenye kanda sita za kitaifa.

Wanashauriwa kuanzisha miradi ya ufugaji nyuki katika misitu ya vijiji, kuitunza na kuongeza mapato sambamba na kuhifadhi mazingira.

Meneja Mradi wa Forest and Farm Facility (FFF) wa MJUMITA Daniel Lucas, anasema hayo kwenye mkutano mkuu wa wanachama wa mtandao huo ukileta pamoja wajumbe 1,500 wa kanda hizo sita.

Wajumbe hao ni pamoja na maofisa misitu, madiwani, viongozi wa vijiji, wafadhili na wafanyakazi wa Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG).

 Anasema kufuga nyuki kibiashara ni muhimu kwani kunalinda mazingira kwa sababu huzingatia kanuni za kitaalamu na kutunza ikolojia.

Anaongeza kuwa kuna misitu mingi ya asili inayofaa kuzalisha asali na wananchi wakijikita katika miradi ya  nyuki watakuwa wasimamizi misitu kwa ufanisi zaidi.

 “Kama tutafuga nyuki na kushiriki kikamilifu kuhifadhi misitu na kuongeza kipato kupitia uzalishaji wa asali na bidhaa nyingine zitokanazo na nyuki tutaboresha maisha,” anasema.

 “Tutazalisha asali, nta ya nyuki, sumu ya nyuki, chavua, sabuni na kupata vipodozi vya ngozi na nywele na manukato hatimaye kujiongezea kipato na kuhifadhi misitu. Ndiko kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.” Anasema Lucas.

Akielezea mchango wa MJUMITA kwa jamii kupitia sekta ya kufuga nyuki, Lucas anasema wametoa mafunzo ya namna ya kuongeza thamani kwenye mazao ya nyuki kwa watu 61 ambao kati yao wanawake ni 48 na wanaume 13.

Aidha, mtandao umeunganisha wafuga nyuki na  kuanzisha shirikisho wilayani Kilosa, kuandaa kitabu cha ufugaji nyuki kwa ajili wanafunzi wa shule za misingi kujifunzia ili washiriki kwenye kuhifadhi misitu.

Kadhalika, anataja kupata wanachama wa MJUMITA ambao wanaanzia ngazi ya chini hadi kufikia viwango vya juu vya ukuaji.

Aidha, Lucas anasema MJUMITA imeshindanisha shule za misingi kupitia uandishi wa insha na kutoa mizinga 100 kwa shule 10 zilizoshiriki mashindano sambamba na kushiriki maonyesho ya kikanda na kitaifa.

Lengo ni kufikia masoko na kutangaza bidhaa zinazotokana asali na kuanzisha manzuki ya mfano kwa ajili ya ufugaji nyuki.

TANZANIA IKO JUU

Tanzania ni ya pili kwa kuzalisha asali barani Afrika baada ya Ethiopia na inashika nafasi ya 14 duniani.

Mwaka 2022, ilizalisha tani 32,691 za asali na kwa sasa inachangia asilimia 1.7 ya asali yote inayozalishwa duniani.

Lucas anasema sekta hiyo huchangia Dola za Marekani milioni 5.8 kwa mwaka kazi ikifanywa na jamii zinazoishi pembezoni mwa misitu kama shughuli za kijadi.

KUFUGA KIZAMANI 

Kadhalika, asilimia 90 ya ufugaji nyuki hufanywa kwa njia ya kienyeji na asilimia 70 ni mizinga ya asili.

Ufugaji kienyeji unafanywa na makabila mengi kimazoea kwa kutumia mizinga ya asili bila kuzingatia kanuni bora za ufugaji. Matokeo yake ni kuambulia mazao kiduchu kutokana na matumizi ya zana za asili, duni na kuwaacha nyuki kuzagaa pasipo uangalizi wa karibu. 

Uwekezaji  huo ni hasara ndiyo maana kuwekeza kwenye ufugaji wa  tija au  kibiashara kwa kutumia mbinu na kanuni bora kama kutumia mizinga  ya masanduku yenye viunzi au fremu na iliyo na kitenga malkia. Kadhalika unavuna mazao mengi kama asali, nta, maziwa na sumu ni muhimu.

Anasisitiza kuwa sekta ya ufugaji nyuki ina uwezo mkubwa wa kuongeza uchumi wa taifa, kuboresha maisha, kutoa ajira, kuongeza kipato na kutatua matatizo ya kiafya, kuhakikisha usalama wa chakula, na kudumisha mifumo ya ikolojia kupitia uchavushaji mimea.

Washiriki wa mkutano huo akiwamo Baraka Ibrahimu wanaiomba serikali kuweka utaratibu wa kuwapimia misitu ya hifadhi ya vijiji iliyoko karibu na wananchi na kuwapatia hati miliki ambazo zitawawezesha  kuwa na uhalali wa kuendesha shughuli mbalimbali kama ulinzi,  uhifadhi na kufugaji nyuki.

Aidha, anasema wanawaomba viongozi wa vijiji na madiwani kusimamia sheria za matumizi bora ya ardhi ili kuepukana na changamoto za migogoro ya ardhi ambayo inasababisha kuleta uvunjifu wa amani na hivyo nchi kuwa salama.

Anaiomba MJUMITA kutoa elimu zaidi kwa wananchi kuhusu sheria za ardhi na uhifadhi wa misitu na mazingira kwa sababu wengi hasa vijijini hawafahamu sheria hizo ambazo zinapunguza migogoro ya ardhi.

“Usimamizi wa misitu na ufugaji nyuki unapaswa kufuatwa kisheria na ikiwa mtu atahitaji kufanya ufugaji nyuki anapaswa kuzijua sheria za uhifadhi wa mazingira kwasababu ni sehemu ya uhifadhi, usimamizi na utunzaji wa mazingira,” anasema.

Mkurugenzi Mtendaji wa MJUMITA, Rahima Njaidi, anasema wamejadiliana na  wadau pamoja na serikali kuangalia changamoto wanazokutana nazo katika uhifadhi na usimamizi wa misitu.

Aidha, kupanga mkakati wa kupunguza uharibifu wa misitu na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Rahima anasema upo umuhimu wa jamii kujikita katika kufuga nyuki kusaidia kuhifadhi na kusimamia rasilimali misitu.

Anawaagiza wafugaji kutumia mbinu wanazofundishwa na kufuga nyuki kisasa kwa kutumia teknolojia ili kupata manufaa zaidi.

Mwenyekiti wa Bodi ya MJUMITA Rehema Ngelekela, anasema mtandao huo umehifadhi hekta milioni 1.8 za misitu iliyopo kwenye ardhi ya vijiji na kutoa fursa ya umiliki na usimamizi katika nyanja mbalimbali.