WATU wametoka mbali bwana acha wee! Kina baba siku hizi wanapokuwa sebuleni wanaangalia na watoto wao wakati mwingine wanakumbuka mbali sana. Ni kwamba wao wakati wa utoto wao hawakupata bahati kama hiyo.
Hawakupata bahati ya kukaa pamoja na wazazi wao kuangalia runinga, na si kwamba wazazi walikuwa hawataki kufanya hivyo. Kwanza kabisa picha linaanza hazikuwepo. Tanzania mambo ya runinga yalianza katikati ya miaka ya 1990, kipindi cha Awamu ya Pili, iliyokuwa ikiongozwa na hayati Ali Hassan Mwinyi.
Kasheshe sasa zilipoanza kuingia nchini, zilimilikiwa au kununuliwa na watu wachache sana. Si wengi walioweza kumiliki TV kutokana na kuwa ghali sana nyakati hizo.
Hebu fikiria, hata miji mikubwa kama Dar es Salaam, unaweza kukuta mitaa mitatu hadi minne wenye runinga ikawa ni familia moja au mbili tu. Kitongoji chote wenye TV ni wa kuhesabu na tochi.
Halafu sasa runinga zenyewe siyo kama za sasa hivi kwani zilionekana kama redio kubwa hivi. Zilinakishiwa au kutengenezwa kwa mbao pembeni, na hata batani zake ni za kufunga na kufungua hazikutofautiana sana na redio. Tofauti na sasa ni za kubonyeza au kutumia kiunga mbali.
Na hata ulipoanza utaratibu wa kutumia kiunga mbali (rimoti), ilikuwa inakaa chumbani kwa baba, na kama yeye hayupo kunakuwa na mtu maalum kwa kazi ya kuwasha na kuzima na huyo ndiye tu anayekaa nayo hapo asipokuwepo hamtazami ng’o.
Aidha, kutokana na kuwapo kwa watu wachache tu kuwa na runinga, waliozimiliki walijichukulia umaarufu mkubwa kwani walijulikana sehemu mbalimbali na kuonekana kama ni watu wenye uwezo mkubwa pia.
Watoto wengi wa majirani walikuwa wakimiminika kwa wenye runinga kwenda kuangalia mikanda ya filamu, muziki, na hata vituo vya runinga vilipoanzishwa, watoto hao pamoja na hata baadhi ya watu wazima walikuwa wakienda kuangalia tamthilia mbalimbali zilizokuwa zikioneshwa wakati huo.
Sasa turudi kwa watoto wa enzi hizo ambao ikifika saa 12:00 jioni hivi na saa moja wanamiminika kwenda kuangalia TV kwa jirani walikutana na changamoto mbalimbali za kuchekesha, kushangaza na kuhuzunisha kwa wakati mmoja.
Wale waliozaliwa miaka ya 2000 kurudi nyuma, watakuwa wakikumbuka masharti mbalimbali na vikwazo ambavyo walikuwa wakivipata wanapokwenda kuangalia TV kwa jirani.
Ingawa si wote waliokuwa na matatizo, lakini ukiongewa na kina baba wengi wa sasa ambao kwa wakati huo walikuwa watoto au vijana, watakwambia changamoto nyingi walizokuwa wakizipata wanapokwenda nyumba kwa jirani kuangalia runinga.Aidha, kabla ya kutaja masharti hayo nitawapa kisa kimoja nilichosimuliwa na rafiki yangu mmoja kuwa walikuwa na tabia ya kwenda kuangalia TV nyumba ya jirani. Yeye na wadogo zake wawili na mama yao hasa siku za tamthilia.
Lakini kuna siku kwa wenye runinga walikuwa wamenuna. Na kubwa zaidi walimwagiwa maji ya ukoko. Walirejea nyumbani na kumkuta baba yao ambaye alishangaa kuona wamerudi mapema na wamelowa, tena maji yenye ukoko. Mama yao akahadithia kilichowatokea. Kwanza kabisa akawapiga marufuku kwenda tena. Hakuona umuhimu wa kwenda kulianzisha kwa jirani yake aliyeidhalilisha familia yake.
Mwisho wa mwezi ulipofika baba yao alirudi na runinga pamoja na antena yake, ikafungwa na wao wakawa na TV nyumbani kwao.
Kumbe mzee wao aliumizwa sana na tukio lile, akaamua mshahara wake wote na pesa zingine alikopa, akanunua runinga ili familia yake isinyanyaswe tena.
Baadhi ni ya masharti kwanza kabisa ni kuwa msafi ukiingia kuangalia TV. Ama mtoto awe ameoga kwao, na akiingia anakaguliwa.
Kuna mzee mmoja alikuwa anaweka beseni la maji mlangoni ili kila anayeingia kwanza kutazama TV anawe miguu kwanza na akiwa anakula kwanza wote mnatoka, mtakaa nje hadi wamalize ndiyo mtarudi tena.
Kuna masharti ya kuvua ndala au kandambili ambazo mtoto amevaa, na akiingia hakuna kukaa kwenye kochi ni chini kwenye sakafu au kapeti, basi na hakuna kupiga kelele, kucheka, au kukohoakohoa ukifanya hivyo unaenda na maji (unatimuliwa).
Yupo mmoja aliniambia kijijini kwao mtu wa kwanza kuwa na TV, alikuwa akiwafanya watoto kama watumwa kwani walikuwa wakipewa ndoo kwenda umbali mrefu kuchota maji ndiyo waje kuangalia, na mwingine akasema wao walikuwa na kazi ya kupukuchua mahindi aliyokuwa nayo, hiyo ndiyo ilikuwa kama ujira wa kuangalia runinga yake. Je wewe ulikutana na masharti gani?
Tuma meseji 0716 350534
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED