Marufuku ya Samia 2021, nchi kung’aa kimataifa na ukakasi wake katika kodi

By Neema Emmanuel , Nipashe
Published at 07:15 AM Oct 04 2024


Mtaalamu wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Prof. Abel Kinyondo, akitoa mada kwa wanasemina kihusu kodi.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mtaalamu wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Prof. Abel Kinyondo, akitoa mada kwa wanasemina kihusu kodi.

RUSHWA imekuwa kikwazo katika mfumo wa haki ya kodi nchini, hata kuchangia watoa huduma, viongozi na wafanyabiashara wengi kuamua yasiyo sahihi, ili kupata faida binafsi hali inayoharibu maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Kwa mujibu wa Ripoti ya Mwaka 2022/23 ya Utendaji Kazi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), imetaja udhaifu wa kiutendaji na vitendo vya rushwa katika taasisi za serikali, baadhi ya vigogo wakifikishwa mahakamani na hata kuhukumiwa kifungo gerezani. 

Miongoni mwa yaliyobainishwa ni malipo ya fedha za utekelezaji miradi ilhali miradi yenyewe haijatekelezwa, ujenzi holela wa vituo vya mafuta na nyaraka feki kuthibitisha malipo ya safari za nje. 

Hilo lipo katika mifumo mbalimbali, kwani hata alipokuwa akikabidhi Ripoti ya Rushwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan, jijini Dodoma Machi 28, mwaka huu, aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Kamishna Salum Hamduni, akaitaja miradi iliyofuatiliwa ni pamoja na maendeleo inayotekelezwa kwa utaratibu wa ‘Force Account’. 

Pia, akataja miradi 12 ya ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji yenye thamani ya Sh. bilioni 107.4 katika mikoa ya Morogoro, Dodoma, Iringa, Tabora na Mbeya. 

Anasema, matokeo ya ufuatiliaji yalionyesha kuwapo mianya ya rushwa, baadhi ya miradi ikionekana kutosajiliwa na Bodi ya Usajili ya Makandarasi na Wakala wa Usalama Mahali Pa Kazi, sambamba na ucheleweshaji malipo kwa makandarasi. 

“Matokeo mengine ni malipo kufanyika pasipo kufanyika baadhi ya kazi, malighafi za ujenzi kutopimwa ubora wake kinyume cha mkataba na kutozingatiwa kwa sheria na kanuni za ununuzi wa umma na kuwapo kwa nyongeza ya kazi pasipo kufuata utaratibu," anasema. 

Aidha, kunatajwa rushwa sio tu tatizo la kimaadili, pia ni tatizo la kiuchumi na kijamii, rushwa akiitaja inachangia kupunguza mapato ya serikali, miradi kutokamilika na kuwa chanzo cha watoa huduma kushindwa kulipa kodi stahiki kutokana na hongo wanazotoa. 

Hiyo ikatajwa kuchangia serikali kukosa fedha ambazo zingetumika katika maendeleo ya jamii, hata kuathiri huduma za kijamii kama vile elimu, afya na miundombinu, ikisababisha madhara makubwa kwa wananchi.

 Tatizo hilo linatajwa kuhatarisha kuchangia kuvuruga imani ya wananchi katika mifumo ya kisheria na utawala, pia kutokulipa kodi na kujihusisha na udanganyifu wakikufuata nyanyo za viongozi wao, hali inayozorotesha ukuaji uchumi na inakwamisha juhudi za serikali kuboresha mazingira ya biashara. 

Alipohutubia Bunge Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, akaeleza dhamira ya serikali kuendeleza mapambano dhidi ya rushwa kwa kutowaonea aibu viongozi na watumishi wazembe, wezi na wabadhirifu wa mali za umma.

 “Tutaendeleza pia juhudi za kupambana na rushwa kwenye utumishi wa umma,” akasisitiza Rais Dk. Samia.

 Kwa mujibu wa Jarida la TAKUKURU la mwaka huu, inarejea utafiti uliofanywa na Transparency International ya Mwaka 2023 Kwa jina la ‘Corruption Perception Index (CPI)’ inaonyesha  Tanzania imefanya vizuri na kupata alama 40 na kushika nafasi ya 87 kati ya nchi 180 zilizofanyiwa utafiti, ikilinganishwa na alama 38 ilizopata mwaka 2022 ambapo ilishika nafasi ya 94.

 Tanzania, kwa mujibu wa taarifa hiyo, imeshika nafasi ya pili katika mapambano dhidi ya rushwa katika ukanda wa Afrika Mashariki ikitanguliwa na nchi ya Rwanda. 

ATHARI ZA RUSHWA 

Akizungumza na Nipashe, Emmanuel Lewis, mkazi wa Dodoma anashauri ni muhimu kwa serikali na jamii  kuchukua hatua madhubuti kupambana na rushwa na kuboresha mfumo huo, kuhakikisha haki ya kodi inatekelezwa kwa usawa na ufanisi, ili kuleta matokeo chanya kwa jamii na kuimarisha maendeleo yao. 

Lewis anafafanua kwamba rushwa inadhuru ukuaji uchumi, kwa kuzuia uwekezaji wa ndani na kigeni kwa sababu wawekezaji wanahitaji mazingira safi ya biashara bila vitendo vya rushwa, akisema kukosekana haki ya kodi kunawakatisha tamaa, mifumo duni ya usimamizi wa kodi huongeza nafasi ya ufisadi, serikali inatakiwa kuimarisha mifumo yake kuzuia rushwa. 

"Rushwa inakwamisha uwezo wa serikali kutoa huduma bora zinazotegemea mapato ya kodi, wananchi wanapolipa kodi lakini wanakosa huduma za msingi kama elimu na afya bora, wanashindwa kuona umuhimu wa kulipa kodi,” anasema. 

Elizabeth Faustine kutoka Mwanza, anaeleza rushwa inarudisha nyuma maendeleo, maana mfanyabiashara anapotoa rushwa ‘kurahisishiwa maisha’ inaikosesha serikali mapato.

 Vitalis Dahaye, anasema chanzo kingine ni wananchi kutokuwa na  uelewa wa kutosha kuhusu wajibu wao wa kulipa kodi, pia umuhimu wake, hata inawarahisishia watumishi wa umma wapotofu kutumia elimu duni ya wananchi kujinufaisha kwa rushwa. 

Anataja chanzo kingine ni mamlaka zinazodhibiti rushwa kulegalega, katika udhibiti.   

WASOMI WAFUNGUKA 

Mtaalamu wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Prof. Abel Kinyondo, anaeleza kuwa uwajibikaji ni nguzo muhimu ya kudhibiti mambo mbalimbali ikiwamo rushwa, ukwepaji kodi na utoroshaji fedha. 

Anasema, ili kujinasua kunahitajika kutumika malighafi zinazopatikana nchini, viongozi kuwa mbali na maslahi binafsi, wawekezaji kutokutumia njia za udanganyifu kukwepa kodi au kulipa kidogo na wananchi kutokulichukulia suala la ulipaji kodi ni hiyari. 

Pia, anaeleza umuhimu wa kuwapo mabadilishano ya taarifa kutoka nchi moja kwenda nyingine ni jambo la muhimu na lenye maslahi mapana ya nchi. 

Aidha, katika utoroshwaji fedha, Prof.Kinyondo ameweka wazi kuna vyanzo vikuu vitatu visivyo halali kwa mapato, usafirishaji haramu wa fedha na matumizi haramu ya fedha mfano kuwezesha matukio ya kigaidi. 

NENO LA TRA  

Kwa mujibu wa Taarifa ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ya Kodi na Ushuru 2023 /2024  inaweka wazi umuhimu wa kulipa kodi na adhabu zinazoutolewa. 

Pia, inataja kusajili wafanyabiashara wadogo na watoa huduma kwenye sekta isiyo rasmi watatambuliwa na kupewa vitambulisho, wenye mauzo ghafi yasiyozidi Sh. milioni nne kwa mwaka nao hawatalipa kodi. 

Taarifa inafafanua, mauzo ghafi kwa mwaka yanapozidi Sh. milioni 100, wauzaji watawajibika kutengeneza hesabu za mizania, huku mtu binafsi mwenye mauzo ghafi kwa mwaka kuanzia Sh.milioni 11 anatakiwa kutoa risiti za kielektroniki. 

Aidha, inafafanuliwa mlipakodi mwenye mauzo ghafi chini ya Sh.milioni 11 anatakiwa kutoa risiti ya kuandikwa kwa mkono zenye jina la muuzaji,TIN yake, jina la mnunuzi, aina ya bidhaa na thamani yake. 

Taarifa hiyo inaongeza kuwa muuzaji atakayeshindwa kutoa risiti ama akatoa risiti yenye thamani ya uongo atalipa faini ya kiasi kikubwa kati ya asilimia 20 ya thamani ya bidhaa au huduma ama kulipa  shilingi milioni 1.5, huku mnunuzi asiyedai risiti atalipa faini ya kiasi kikubwa kati ya asilimia 20 ya kodi iliyokwepwa.