Marekebisho sheria rushwa ya ngono kumbana mwathirika kama mtuhumiwa

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 08:37 AM Sep 17 2024
 Crispin Chalamila Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU.
PICHA:MTANDAO
Crispin Chalamila Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU.

RUSHWA ya ngono kwa wanaharakati na watetezi wa haki za wanawake ni tatizo kubwa na zaidi ni ukiukwaji wa haki unaochangia kuendeleza unyanyasaji wa kijinsia na kuenea magonjwa kama VVU, UKIMWI na homa ya ini.

Rushwa hiyo inahusisha maneno au bila maneno na mara nyingine ni kujenga mazingira ili kuwaingiza wanawake kwenye kutoa ngono ili wapate huduma au haki.

Mojawapo ya kampeni zinazofanyika jijini Dar es Salaam ni 'Safari salama bila rushwa ya ngono inawezekana', iliyoasisiwa na Shirika la Wanawake Katika Jitihada za Kimaendeleo (WAJIKI).

Kampeni hiyo inafanyika katika wilaya za Kinondoni, Ilala na Temeke, kwa kushirikiana na wadau madereva wa bodaboda, bajaji, daladala na jamii, anasema Mkurugenzi wa WAJIKI, Janeth Mawinza.

Anasema inalenga kumaliza rushwa ya ngono kwa wasichana na wanawake, wanaosafiri ndani ya vyombo hivyo na popote pale.

Mkurugenzi wa Janeth anasema, kampeni hiyo imesaidia pia kuondolewa kifungu cha (10) (b) cha Sheria ya Rushwa ya Ngono cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), kinachombana mtoaji wa rushwa hiyo sawa na mpokeaji.

"Hatua hiyo imetuongezea nguvu ya kuendelea na kampeni ya vita dhidi ya rushwa ya ngono, kwani moja ya vitu ambavyo tulikuwa tunavipinga, ni kifungu hicho na sasa kimeondoka," anasema Janeth.

Anasema, kwa muda mrefu wadau walitamani kifungu hicho kirekebishwe, kwa maelezo kuwa wanafunzi na wanawake wengi hulazimishwa kutoa rushwa ya ngono bila ridhaa yao.

"Harakati za WAJIKI na wadau wengine wakiwamo Mtandao wa Kupinga Rushwa ya Ngono Tanzania za kupinga kifungu hicho, hatimaye zimezaa matunda baada kilio chao kusikika," anasema.

Ndivyo anavyosema Janeth katika mazungumzo yake na gazeti hili jijini Dar es Salaam wakati akitoa maoni yake baaada ya kifungu walichokiwa wakilalamikiwa kufanyiwa kazi bungeni hivi karibuni.

"Rushwa ya ngono ni matokeo ya tofauti, katika madaraka kati ya mhalifu na mwathirika, anayehitaji huduma kutoka kwa mwenye madaraka hana uhuru wa maamuzi," anasema.

Anafafanua kuwa kama sheria ingeendelea kutumika jinsi ilivyo, wanafunzi na wanawake wangeumia zaidi bila hatia, kwa kuwa wengi wao wanalazimika kutoa ngono bila ridhaa yao.

"Hao wanaotoa rushwa kwa kutaka wapate unafuu katika jambo fulani, waendelee kubanwa na sheria, lakini wale ambao tumekuwa tukiwapigania wanalazimishwa kutoa ridhaa yao," anasema.

Mkurugenzi huyo anasema, kumuunganisha anayeumizwa na mwenye madaraka katika rushwa ya ngono, ili atajwe kama mtoa rushwa, si sawa bali anatakiwa kutajwa kama mwathirika wa rushwa ya ngono au shahidi.

 MTANDAO WANENA

Mtandao wa Kupambana na Rushwa ya Ngono Tanzania, umetoa tamko, kwa kuzingatia matokeo ya utafiti uliofanywa na TAKUKURU kwa kushirikiana na wanamtandao kuwa wanatambua ukubwa wa tatizo hilo kwenye jamii.

Mwenyekiti wa mtandao huo, Profesa Penina Mlama anasema, tatizo hilo liko nyumbani kwa watumishi wa kazi za ndani, wakiwa waathirika wakuu, vyuoni na shuleni, wanafunzi wakiathirika zaidi.

"Kwenye maeneo mengi ya utumishi wa umma na binafsi, maeneo ya biashara, kwenye hospitali zetu, hasa kwa wagonjwa wa kike na hata kwenye taasisi za dini kuna rushwa ya ngono," anasema Profesa Penina.

Anaeleza kuwa mtandao huo unatambua mwitikio wa elimu ya kuzuia na kupinga rushwa ya ngono umekuwa mkubwa kwa wazazi, watoto shuleni, vijana vyuoni, kwenye taasisi za kidini, waajiriwa majumbani, ofisini na katika tasnia ya sanaa na utamaduni.

"Kwa kuzingatia maamuzi ya bunge yaliyofanyika Septemba 2, mwaka huu, ambapo serikali iliazimia kukubaliana na mapendekezo ya Kamati ya Bunge, ambayo yamekuwa msimamo wa Mtandao wetu pia, tumefurahia.”

Anasema aidha kufuta kifungu 10 (b) na kuacha kama kilivyo kifungu 25 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya Ngono, 2007 ni hatua ya kushangiliwa.

Anasema bunge lilikwenda mbali zaidi na kuongeza wigo wa ukomo wa adhabu kwa waomba rushwa ya ngono kutoka miaka mitatu hadi 10 na faina ya Sh. milioni tano hadi 10.

"Sisi wanamtandao wa kupambana na rushwa ya ngono, tunapenda kuchukua fursa hii kupongeza wanamtandao wote kutoka kona zote, waandishi wa habari, wadau wa kimataifa waliotuunga mkono,” anasema Profesa Penina.

Anafafanua kuwa kwa kusimama kidete kupaza sauti zao na kukataa mapendekezo ya kifungu 10 (b) kilichotaka mwathirika wa rushwa ya ngono ashtakiwe kama mhalifu, kumeleta mafanikio katika jitihada za kuongeza utu wa mwanamke.

Mwenyekiti huyo anafafanua kuwa, bunge kuridhia kutopitisha kifungu hicho na kuongeza adhabu kwa waomba rushwa ya ngono, ni ushindi mkubwa kwenye mapambano dhidi ya unyanyasaji kijinsia.

Aidha, anasema ni uthibitisho tosha wa nguvu ya wananchi na umuhimu wa sauti za wanamtandao kama wanajamii katika kukataa mifumo kandamizi imezaa matunda.
 Aidha, anasema kamati ya utawala, katiba na sheria imetimiza wajibu wake na kuishauri serikali kutopitisha kifungu hicho.

MAREKEBISHO

Bunge linaelezwa kuwa adhabu ya faini isiyopungua Sh. milioni mbili na isiyozidi Sh. milioni 10 au kifungo kisichopungua miaka mitano imewekwa katika makosa ya rushwa ya ngono.

Ni kwenye muswada wa marekebisho ya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa wa mwaka 2024.
 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene, anasema bungeni kuwa kifungu cha 25 kinaweka masharti kwa mwenye mamlaka.

Kinatamka kuwa ni kosa kwa mwenye mamlaka kuomba rushwa ya ngono au upendeleo wa aina nyingine kama sharti la kutoa au kupata ajira, cheo au haki.

Katika ufafanuzi wake, anasema kifungu hicho kinaeleza kuwa ni kosa kwa mtu anayeahidi au kutoa rushwa ya ngono au upendeleo mwingine kwa mwenye mamlaka.

Kwa mwenye mamlaka au aliye katika nafasi ya mamlaka ili kumshawishi mtu huyo kutoa upendeleo wa ajira, cheo, haki au upendeleo mwingine wowote.

Aidha, muswada wa marekebisho ya sheria hii umependekeza kuongeza kosa na adhabu ya rushwa katika uchaguzi, michezo, michezo ya kubahatisha na burudani.

“Kamati ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria nayo inapigilia msumari kuwa, wadau wengi wamelalamikia kifungu cha 10 (b) kwa kuwa  kinawanyima waathirika wa rushwa ya ngono haki zao stahiki na kinawapa kinga wahusika wa vitendo hivyo.” anasema.