HALMASHAURI ya Manispaaa ya Kinondoni, kitaifa iko katika manispaa tano nchini zinazosumbuliwa na maambukizi ya magonjwa ya matende na mabusha, ikiwagusa wanaume na wanawake kwa namna mbalimbali.
Ni jambo linaloifanya serikali kukosa usingizi kuondoa shida hiyo ndani ya manispaa hiyo.
Katika kata 20 zilizopo humo, takwimu na tafiti zinasema Kata 10 ndio zinaonekana korofi kwa kuonekana bado kuna wagonjwa na maambukizi ya maradhi hayo.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni Dk.Peter Nsanya, anazitaja kata hizo ni: Kigogo, Mzimuni, Magomeni, Ndugumbi, Tandale, Kijitonyama, Kinondoni, Hananasifu, Mwananyamala na Makumbusho.
Kwa mujibu wa mganga huyo, katika kata hizo, Tandale inatajwa kuwa kinara wao, ikiwa na maambukizi ya asilimia 2.3, ikilinganisha na zingine.
Hivyo mpango uliopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, inataja kuwa na mpango kabambe wa kuondoa magonjwa hayo, ikiamini yanazuilika.
Hatua mojawapo, wamekuja na kampeni ya ugawaji kingatiba, ulioanza jana na kumalizika tarehe 26, Jumapili ijayo mchakato utakaozifikia kata hizo 10, ili kuendana na kasi ya kukabiliana na magonjwa hayo.
Dk.Nsanya anasema, katika hilo wanatarajia kuwafikia wananchi wapatao 284,036 ambao walengwa ni wananchi wote kuanzia miaka mitano na kuendelea.
Imeelezwa kuwa ni kampeni itakayofanyika ‘nyumba kwa nyumba’; kwenye mikusanyiko; shuleni; vituo vya usafiri, masoko pamoja na kwenye vituo vya kutoa huduma za afya, mtazamo ni kuwafikia watu wote.
Kwa mujibu wa uongozi wa Manispaa, kumeelekezwa dira mbali inayotoa mafunzo kwa viongozi wa dini, kuhamasisha na kuwaeleza ukweli wananchi hao wajitokeze na kuacha dhana potofu kuhusiana na kinga hiyo, wakimeza dawa pasipo shaka yoyote kujihami na madhara hayo.
Shekhe Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mohamed Muhenga anaipongeza serikali, kwa kuwapatia mafunzo na mwongozo kuhusiana na kinga hiyo.
Aidha, akaahidi kwenda kuhamasisha zoezi hilo katika nyumba za ibada ili kuweza kutokomeza maradhi hayo ambayo yanaepukika.
Mkuu wa Kanisa la Tanzania Methodist, Askofu Alex Siso anasema, wako bega kwa bega na serikali kutokomeza ugonjwa huo ambao ni wa aibu katika jamii atatumia hekima ya hali ya juu kuihamasisha jamii kumeza dawa ili kutokomeza maradhi hayo ndani ya manispaa hiyo.
Ni juhudi inayojumisha watu wa kada zote, ‘watoto kwa wakubwa’ kuanzia umri wa miaka mitano na kuendelea.
Rai yake kwa umma, ni kuutaka umma kujitokeze kuchangamkia fursa hiyo ya manispaa, wakiacha dhana potofu kwa baadhi ya wananchi wanaohusisha dawa hizo tafsiri inayoenezwa na baadhi ya watu “kuzuia kuzaliana”, akikemea “jambo ambalo halina ukweli wowote.”
Mratibu wa Miradi ya kuondoa Magonjwa ya Matende na Mabusha kutoka Ofisi ya Mkoa Dar es Salaam, Alex Mkamba, akisema jukumu ya ugawaji kinga tiba iliyoanza mwaka 2019.
Ni maeneo yenye maambukizi na ikitajwa zimesaidia kupunguza maambukizi katika baadhi ya halmashauri, ikiwa na ufafanuzi kwamba mtumiaji anaweza kumeza kabla au baada ya kula.
Mbali na Kinondoni, halmashauri zingine ambazo zina maambukizi hayo na zitafikiwa kupatiwa kingatiba ni: Mtwara Mikindani; Lindi Manispaa; Mtama mkoani Lindi; na Pangani, Tanga.
Kwa niaba ya Manispaa ya Kinondoni na serikali, shime imetolewa na kuwataka wakazi wa maeneo hayo kunywa dawa pasipo woga.
Inatajwa ni dawa salama za wananchi kuacha kupotoshana na wazazi wasiwakataze watoto wao katika unywaji dawa, ili kujikomboa, pia kujikinga na maradhi hayo.
Wanawake nao ni kundi lililotakiwa kuchangamkia fursa hiyo kwani maradhi hayo hayachagui jinsia, kwani kwa maradhi ya matende yanawakumba jinsia zote, hivyo wakatakiwa kuchangamkia zoezi hilo.
Baadhi ya maeneo ambayo yamefanikiwa katika kampeni kama hizo za Manispaa ya Kinondoni, ni wilaya ya Rufiji mkoani Pwani, kulikoshuhudiwa mabadilikio kihistoroa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED