Harakati kutetea, kuwaelimisha abiria haki zao zaanzia stendi hadi darasani

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 08:15 AM Feb 11 2025
Abiria katika kituo kikuu cha mabasi Dar es Salaam.
Picha: Mtandao
Abiria katika kituo kikuu cha mabasi Dar es Salaam.

KUENDELEA kuwapo usumbufu wa abiria kila wakati kwenye vituo vya mabasi na ndani ya magari kunaliamsha Shirika la Kutetea Haki za Abiria (SHIKUHA), kuwafikia ili kuwapa somo la kujiepusha na ulaghai.

Ni kutokana na ukweli kuwa abiria wawe wa  masafa marefu na daladala wanakumbana na changamoto wanapotafuta usafi au wakiwa ndani ya vyombo vya usafiri.
 
SHIKUHA inasema baadhi ni kuzidishiwa nauli au kutozwa zaidi ya iliyopangwa na serikali na kusababisha usumbufu na gharama kwa udanganyifu
 
Wakati mwingine huenda abiria wanahangaika kwa kutokuwa na elimu ya kutosha kuhusu haki zao wanapotafuta usafiri au wakiwa ndani mabasi kwenda maeneo mbalimbali.

SHIKUHA, inakabiliana na changamoto hizo kwa kuwaelimisha abiria kujua haki zao, anasema Mwenyekiti  Solomon Nkiggi.

Katika mazungumzo na Nipashe jijini Dar es Salaam, anasema wanashirikiana na trafiki na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), kuelimisha abiria kujua haki zao ili wasiendelee kuonewa na kuvurugwa.
 
Anasema abiria wanakumbana na changamoto ya kupandishiwa nauli, kubadilishiwa mabasi bila ridhaa yao, kusumbuliwa na wapigadebe vituoni, hayo yakifanywa na wapigadebe, makondakta na madereva.

Anasema hayo yanafanyika bila kujua kuwa wana haki ya kukataa.
 
"Shirika letu linafanya kazi nchi nzima kwa kushirikiana na wadau hao pamoja na abiria wenyewe. Wanapopata changamoto wanatupigia simu ili kupata msaada kutoka SHIKUHA, trafiki au LATRA," anasema Nkiggi.
 
WANACHOFANYA 
 
Nkiggi anasema SHIKUHA ina mtandao Tanzania nzima, na kwamba kila mara wanajipanga katika vituo vya daladala na mabasi kuzungumza na abiria wanaofika kwa ajili ya safari au kukata tiketi.
 
"Kama ni wale wanaofika stendi kukata tiketi, tunawahimiza watumie teknolojia  tiketi mtandao, lakini pia wanachama wetu huingia katika mabasi kabla ya kuanza safari na kuwapa elimu ya kujua haki zao," anasema.
 
Anafafanua kuwa wameanzisha shirika kwa jukumu hilo la kuelimisha abiria wasikubali kuzidishiwa nauli hasa vipindi vya sikukuu, kulinda mizigo pamoja na changamoto nyingine katika usafiri.
 
"Vilevile, tunawaelimisha abiria wasikubali basi likatishe safari hasa daladala. Tunawaelimisha ili watoe taarifa, linapotokea tatizo lolote au ajali, lakini pia tunawapa elimu ili basi linapochelewa kuondoka stendi kwa muda uliopangwa, hatua za kisheria zichukuliwe," anasema.
 
Anafafanua kwamba  ni wadau wa trafiki na LATRA na wanapopata taarifa za changamoto za aina mbalimbali kutoka kwa abiria  wanazifikisha haraka kwao ili hatua zichukuliwe.
 
 Mwenyekiti  anaongeza kuwa mambo mengine wanayoshughulikia ni kutoa elimu ili wanapoona dereva anaendesha mwendo unaohatarisha au kuyapita magari mengine bila kujali usalama wao, watoe taarifa.
 
"Pamoja na hayo, tunaelimisha abiria wasikubali kupokea tiketi ambazo si za mtandao,  wasikubali kutelekezwa njiani kwa ubovu wa basi bila kupewa usafiri mwingine," anasema.
 
Anaongeza kuwa shirika hilo pia linawaelimisha ili wanapoona dereva anaendesha huku akiongea na simu, au kuchati ama amelewa pombe na kuwatolea lugha chafu, watoe taarifa.
 
"Tunataka kupitia elimu tunayotoa, abiria wajue umuhimu wa kupaza sauti ili wasaidiwe pale wanapobaini kuwa kuna jambo haliko sawa, tuko kazini saa 24 kwa ajili ya kulinda haki zao," anasema.

KWA WANAFUNZI
 
 Katibu Mkuu wa shirika hilo, Hashim Omary anasema, mbali na kutoa elimu katika stendi na ndani ya mabasi, wanajipanga kwenda kwenye shule mbalimbali kuelimisha.
 
"Ni muhimu elimu hii ifike pia shuleni, kwa sababu wanafunzi ni abiria wanaosafiri kila siku kwa kutumia daladala au mabasi makubwa wakati wa kwenda likizo au kurudi shuleni," anasema Omary.
 
Wanafunzi nao wanatakiwa kujua haki zao ili kuondokana na manyanyaso ya makondakta na madereva yakiwamo ya kuuziwa kupata usafiri au kutozwa nauli ya mtu mzima, anaeleza.
 
"Hawatakiwi kubughudhiwa. Kwa kuwa shirika letu lina wanachama wake nchi nzima, tukiweka mipango yetu sawa wataanza kwenda shule kutoa elimu kwa kushirikiana na trafiki na LATRA, kwani hao sisi ni wadau wao wakubwa wa utoaji wa elimu kwa abiria," anasema.
 
Omary anasema lengo na matamanio ya SHIKUHA ni kuona abiria wanasafiri bila usumbufu wakiwa wamelipa nauli halali na kufika salama kule wanakokwenda.
 
"Kila mwisho wa mwaka kumekuwapo na tatizo la upandishaji wa nauli, lakini angalau mwisho wa mwaka uliopita tumejitahidi kudhibiti vitendo hivyo, hakukuwa na malalaniko mengi kama ilivyokuwa miaka ya nyuma," anasema.
 
Aidha, katibu mkuu huyo anasema wanajipanga pia kuweka mikakati ya kudhibiiti wapigadebe katika stendi za mabasi, kwa maelezo kwamba wamekuwa ni chanzo cha kupanda kwa nauli.
 
 Kiongozi huyo anasema shirika lao linaangalia uwezekano wa kuwapa elimu watafute shughuli halali za kuwaingizia kipato badala ya kushinda stendi bila kazi maalum.
 
 "Watu hawa wamekuwa ni kero kwa abiria, unaweza kukuta nauli halali ni Sh. 28,000 lakini wanaiongeza hadi 30,000 wakimbambikia abiria 2,000 zaidi. Huo ni wizi. Hivyo, tunaangalia jinsi ya kuwafikishia elimu ili waache kuishi maisha ya aina hiyo yasiyo na uhakika," anasema.