MATOKEO ya mtihani wa kidato cha nne Zanzibar yanaashiria changamoto kubwa na ya dharura katika mfumo wa elimu, ambayo haipaswi kupuuzwa.
Hali hii inapaswa kutazamwa kama janga la kitaifa linalohitaji juhudi za pamoja kutoka kwa viongozi wa kisiasa, walimu, wazazi, walezi na jamii nzima.
Wiki iliyopita tuliangalia changamoto, mifano ya kuiga na leo tunamalizia na mapendekezo ya muhimu kuinua kiwango na kuipa Zanzibar sura mpya inayotokana na maboresho kwenye utoaji wa elimu na taaluma.
MAPENDEKEZO ZANZIBAR
Mosi ni kuimarisha walimu, ikiwa ni pamoja na kuajiri wenye sifa bora na kuwapa mafunzo ya mara kwa mara ili kuboresha mbinu za kufundishia.
Aidha, kuongeza heshima ya walimu kwa kuwapa mishahara minono na fursa za maendeleo ya pia ni muhimu kuwekeza katika teknolojia.
Kadhalika, Zanzibar inapaswa kuwekeza katika miundombinu ya teknolojia shuleni, kama vile vifaa vya kujifunzia kupitia mtandao na maabara za sayansi.
Kuanzisha mfumo wa kutambua vipaji: Ni jambo muhimu, kutengeneza programu za kutambua vipaji vya wanafunzi tangu wakiwa wadogo na kuwaelekeza kwenye fani wanazozipenda, iwe ni michezo, sanaa, au ufundi.
Kila skuli iwe na mtaalamu wa ushauri nasaha ambaye atashirikiana na wanafunzi kutambua vipaji vyao na kuboresha elimu ya ufundi na vitendo.
Kujenga vyuo vya ufundi vyenye vifaa vya kisasa na kushirikiana na sekta binafsi ili wanafunzi wapate mafunzo ya vitendo.
Aidha, kuanzisha mfumo wa elimu unaowapa wanafunzi nafasi ya kuchagua kati ya masomo ya kitaaluma na ya ufundi.
Kupunguza msisitizo wa mitihani: Hapa ni pamoja na kutumia mbinu za tathmini zinazojumuisha miradi, mawasilisho, na kazi za vitendo badala ya kutegemea mitihani ya kukariri maarifa.
Ushirikiano na nchi zenye mfumo bora. Zanzibar inapaswa kushirikiana na nchi kama Finland, Singapore na Ujerumani ili kujifunza na kubadilishana maarifa kuhusu elimu bora.
Pendekezo rasmi kuhusu uwekezaji wa Zanzibar katika elimu. Ikumbukwe elimu ni msingi wa maendeleo ya taifa lolote na ni rasilimali kuu ya Zanzibar ambayo haikubarikiwa kuwa na maliasili nyingi mfano madini. Ingawa kwa haraka haraka kutokuwapo kwa maliasili kunaweza kuonekana kama kikwazo, lakini kwa mtazamo wa muda mrefu, ni fursa ya kipekee. Hii ni kwa sababu Zanzibar inalazimika kuwekeza kwa kina katika rasilimali watu wake kama nguzo kuu ya maendeleo.
Historia ya nchi zilizofanikiwa bila kutegemea maliasili, kama Singapore na Korea Kusini, inatufundisha kuwa mafanikio makubwa yanawezekana kupitia uwekezaji madhubuti katika elimu.
Kwa mfano, Singapore, bila maliasili ya asili, imewekeza katika elimu bora, hususan masomo ya hisabati, sayansi na teknolojia na kuwa kitovu cha uchumi wa maarifa (knowledge economy). Leo ni miongoni mwa mataifa yenye nguvu ya kiuchumi duniani.
Korea Kusini: Baada ya vita vya Korea, taifa hilo lililenga kuimarisha elimu kwa kila raia wake. Wamefanikiwa kujenga uchumi wa viwanda kwa kuwa na nguvu kazi yenye ujuzi wa hali ya juu.
Finland: Japokuwa si taifa lenye maliasili nyingi, imejikita kwenye usawa wa elimu na kukuza vipaji vya wanafunzi tangu wakiwa wadogo. Mfumo wao wa elimu umetoa raia wabunifu na wenye uwezo wa kushindana kimataifa.
Ujerumani: Mfumo wa elimu ya ufundi, elimu pacha (dual education system) umewezesha Ujerumani kuwa na wataalamu wengi wa sekta ya viwanda, teknolojia, na huduma, licha ya kutotegemea sana maliasili.
Mifano hii na mafanikio yake ni funzo kwa Zanzibar, ili ipate maendeleo endelevu, yafuatayo yanapaswa kufanyika:
Elimu kama uwekezaji wa kitaifa: Serikali ichukulie elimu kama msingi wa maendeleo ya Zanzibar na iongeze matumizi ya bajeti kwa sekta ya elimu.
Kupitia mpango wa kitaifa, malengo ya muda mrefu ya elimu yawe ni kuhakikisha raia wote wanapata elimu bora.
Kuongeza uandikishaji (enrollment) na kuimarisha kiwango cha kusoma (literacy rate): Kuanzisha kampeni ya kitaifa ya uandikishaji wa wanafunzi katika skuli za msingi, sekondari, vyuo, na vyuo vya ufundi.
Pia, kuhakikisha kuwa kila mtoto wa Zanzibar anapata nafasi ya elimu ya msingi na sekondari. Jingine kuimarisha masomo ya hisabati, sayansi na Kiingereza:
Halikadhalika, Wizara ya Elimu inapaswa kuanzisha programu maalum za kukuza masomo haya kwa kiwango cha kimataifa.
Jingine ni kuandaa mashindano ya kitaifa na kimataifa ili kuchochea ushindani mzuri kwa wanafunzi, kuhakikisha wanashika nafasi za juu, na kudumisha ubora.
Kuvutia na kuimarisha wataalamu. Pia kuwashawishi Wazanzibari walioko nje na wenye vipaji vikubwa kurudi nyumbani na kushiriki katika maendeleo ya taifa.
Zanzibar iboreshe mazingira ya kazi kwa walimu na wataalamu wa elimu ili kuwapa motisha zaidi. Iboreshe ubora wa watu (quality of people).
Kuwekeza katika mafunzo ya walimu na kuboresha mitaala ya skuli kwa kuzingatia maarifa ya karne ya 21.
Kadhalika kuanzisha vyuo vya ufundi vyenye vifaa vya kisasa ili wanafunzi wawe na ujuzi wa vitendo unaokidhi mahitaji ya soko la ajira.
Kushirikiana na sekta binafsi na wadau wa elimu. Serikali ishirikiane na sekta binafsi katika kufadhili miradi ya elimu na kukuza teknolojia maskulini.
Wadau wa elimu wa ndani na nje wapewe nafasi ya kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kuboresha mfumo wa elimu.
MUHIMU
Zanzibar inaweza kufikia maendeleo makubwa kwa kuiga mifano ya nchi zilizofanikiwa kupitia uwekezaji katika elimu. Ikiwa na maono, nia njema, na mshikamano wa kitaifa, inaweza kuimarisha ustadi wa watu wetu, kuongeza ubora wa elimu na kufidia ukosefu wa maliasili kwa kujenga jamii yenye maarifa, ujuzi, na uwezo wa ushindani wa kimataifa. Elimu bora itakuwa urithi wa Zanzibar kwa vizazi vijavyo, na dira ya maendeleo endelevu ya taifa.
Singapore, Finland, Ujerumani, na Korea Kusini zimefanikiwa kielimu kwa sababu mifumo yao inalenga kukuza vipaji, kuendeleza ubunifu na kuandaa wanafunzi kwa maisha halisi.
Zanzibar inaweza kufanikisha hilo kwa kuiga mbinu hizi, kuwekeza kwenye elimu ya vitendo, na kutambua vipaji vya wanafunzi mapema. Elimu bora ndiyo njia ya uhakika ya kuijenga Zanzibar iliyo na kizazi chenye maarifa, ujuzi, na uwezo wa kuhimili ushindani wa dunia ya kisasa.
Hakuna mtoto anayefeli. Kila mtoto ana kipaji chake cha kipekee ambacho, endapo kitagunduliwa mapema, kinaweza kumpeleka katika mafanikio makubwa maishani.
Mfumo wa elimu unapaswa kubadilika ili kutambua ukweli huu. Ni lazima kuachana na mtazamo wa kupima uwezo wa watoto wote kwa njia moja ya mitihani ya kukariri. Badala yake, ni kubuni mifumo inayotambua na kukuza vipaji vyao mapema.
Hili si tu suluhisho la tatizo la wanafunzi waliofeli bali pia ni njia ya kujenga jamii yenye maendeleo endelevu na ustawi wa kila mtu. Kama alivyosema Albert Einstein, “Kila mtu ni mwerevu. Lakini kama utamhukumu samaki kwa uwezo wake wa kupanda mti, atakaa maisha yake yote akiamini kuwa yeye ni mjinga.”
Mafanikio ya taifa lolote hutegemea ubora wa elimu kwa watu wake. Matokeo ya kidato cha nne Zanzibar yanapaswa kuwa mwito wa kuamka kwa kila mdau wa elimu.
Hatua za dharura zinahitajika ili kuwekeza kwa watoto wa Zanzibar na kujenga taifa lenye maarifa, ushindani, na maendeleo. Kama alivyosema Nelson Mandela, “Elimu ni silaha yenye nguvu zaidi ambayo unaweza kuitumia kubadili dunia.”
Ni wakati sasa wa viongozi wetu, walimu, wazazi na jamii nzima kuunganisha nguvu ili kufanikisha mageuzi ya kweli katika sekta ya elimu Zanzibar. Hali hii si tu changamoto, bali pia ni fursa ya kuijenga Zanzibar bora.
Maoni: +14374316747
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED