Makipa wa4 vinara wa kuokoa penalti Ligi Kuu

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 09:12 AM Nov 18 2024
Hussein Masalanga - Tabora United
Picha: Mtandao
Hussein Masalanga - Tabora United

JUMLA ya penalti 25 zimepatikana kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara inayoendelea msimu huu wa 2024/25, hadi kufikia raundi ya 10 na baadhi ya mechi za raundi ya 11.

Kati ya penalti hizo, 19 zimewekwa ndani ya nyavu na sita zikikoswa. Penalti zilizokoswa, mbili ziliota mbawa kwa kutoka nje huku nne zikiokolewa na magolikipa.

Mbili zilizoota mbawa zilipigwa na Amza Mubarack wa Namungo, Agosti 29, mwaka huu, Uwanja wa Majaliwa uliopo Ruangwa, Lindi, timu yake ikipoteza nyumbani kwa mabao 2-0 dhidi ya Fountain Gate, na Heritier Makambo wa Tabora United ilipocheza dhidi ya Fountain Gate na kubugizwa mabao 3-1, Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora, Septemba 20, mwaka huu.

Wafuatao ni makipa waliookoa penalti nne kwenye Ligi Kuu na wachezaji ambao walipizipiga... 

1# Ley Matampi - Coastal Union

Ley Matampi wa Coastal Union, raia wa Jamhuri ya Kidemkokrasi ya Congo, aliokoa penalti ya Djuma Shaaban, katika mchezo ambao timu yake ilicheza dhidi ya Namungo, Septemba 17, mwaka huu, Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam.

Antony Mlingo alifanyiwa madhambi ndani ya eneo la hatari. Djuma alipiga kwa mguu wa kulia upande wa kushoto mwa kipa huyo. Aliruka upande huo huo na kuupangua, ukaenda kugonga mwamba wa juu.

Kwa bahati mbaya sana mabeki wa Coastal wakashinda kuuwahi na Paul Buswita akaumalizia wavuni kwa mguu wa kushoto na kuwa bao la pili kwenye mechi hiyo iliyoisha kwa Namungo kushinda mabao 2-0.

Matampi tayari alikuwa ameshafanya kazi yake ya kuokoa penalti, bao lililofungwa halikuwa la tuta badala yake lilihesabika kuwa la kawaida. 

2# Metacha Mnata - Singida Black Stars

Golikipa wa Singida Black Stars, Metacha Mnata alicheza penalti ya Hassan Dilunga wa JKT Tanzania, wakati timu zao zilipokutana, Septemba 29, mwaka huu, Uwanja wa Liti Singida na kutoka sare ya bao 1-1.

Ismail Aziz, aliangushwa ndani ya kisanduku cha hatari na mwamuzi kutoa tuta. Alipiga kwa mguu wa kulia, mpira ukaenda upande wa kushoto ambako Metacha alikuwa ameruka, akaupangua, na kuudhibiti. 

3# Ramadhani Chalamanda - Kagera Sugar 

Kipa Ramadhani Chalamanda, aliokoa penalti ya Maabad Maulid wa Coastal Union, Septemba 29, mwaka huu, katika mchezo uliopigwa, Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha, ambao timu yake ya Kagera Sugar ilipoteza kwa bao 1-0.

Alikuwa ni Omari Chibada, aliyeunawa mpira ndani ya boksi. Maabad kwa kutumia mguu wa kulia alipiga mpira upande wa kushoto kwa kipa huyo wa Kagera Sugar, akaruka, akaupangua, mmoja wa wachezaji wa Coastal Union aliuwahi kutaka kufunga, lakini akapaisha juu. 

4# Hussein Masalanga - Tabora United

Ilikuwa ni Novemba 7, mwaka huu, wakati Hussein Masalanga, alipoidaka penalti ya Stephane Aziz Ki, wakati timu yake ya Tabora United, ilipoibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Yanga, mchezo ukipigwa Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Wakati makipa wenzake wakipangua, kipa huyu ameweka rekodi yake ya kuudaka kabisa penalti hiyo na ndiye kwa kiasi kikubwa aliyesababisha kupatikana bao la pili kwa timu yake.

Pacome Zouzoua, aliangushwa ndani ya kisanduku cha hatari, ikaamriwa lipigwe tuta wakati huo Yanga ikiwa nyuma kwa bao 1-0.

Aziz Ki, alipigwa kwa mguu wa kushoto na kuupeleka kushoto kwa kipa huyo, ambaye aliruka na kuukamata. Alinyanyuka nao na kuupiga mbele kwa Yacouba Songne kwenye wingi ya kushoto, akamwacha Denis Nkane na kutoa krosi kwa Offen Chikola aliyeukwamisha wavuni.

Ikumbukwe kuwa matukio hayo yalitokea ndani ya dakika moja kutoka upigaji penalti, kipa kuudaka na kwenda kuzaa bao la pili.