Mafuta ya kokwa, mbegu matunda yana utajiri afya lishe kupindukia

By Pilly Kigome , Nipashe
Published at 07:03 AM Aug 29 2024
Twahir Nzallawahe, alipokuwa katika ziara ya kikazi katika zama akiwa Mkurugenzi wa Maendeleo ya Mazao Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi, katika Maonesho ya Nanenane Viwanja vya Ngongo, mkoani Lindi.
PICHA ZOTE: MTANDAO.
Twahir Nzallawahe, alipokuwa katika ziara ya kikazi katika zama akiwa Mkurugenzi wa Maendeleo ya Mazao Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi, katika Maonesho ya Nanenane Viwanja vya Ngongo, mkoani Lindi.

KITAALAMU inatajwa matumizi ya mafuta ya mbegu na kokwa za matunda yanaleta mabadiliko kwenye mwili wa binadamu kwa kuimarisha afya na inatibu, pasipo kutegemea dawa za kisasa za kitatibu.

Kuna utafiti mbalimbali uliofanywa na wataalamu wa afya na lishe, unaotoa majibu chanya, huku katika Chuo Kikuu cha Afya na Tiba Muhimbili (MUHAS) kukiwapo kitengo kinachojikita katika eneo hilo, kutegemea nyenzo hizo asilia. 

Nipashe ilimtafuta mtaalamu wa stadi hizo, anayejihusisha na uzalishaji, pia uuzaji wa mafuta ya mbegu na kokwa za matunda kwa matumizi ya binadamu, kupata ufafanuzi wake. 

Huyo ni Nzallawahe Twahir, mwenye shamba na kiwanda kilichoko mkoani Iringa vinavyoongezea thamani bidhaa hizo, akitetea kitaalamu faida nyingi zitokanazo na mafuta hayo. 

Twahir, ambaye ni Mkurugenzi wa Maendeleo ya Mazao Mstaafu katika Wizara ya Kilimo, sasa anaisimamia kampuni yake, anaiambia Nipashe kwamba mwanadamu anayetumia mafuta yatokanayo na matunda, kwa mapishi na vipodozi ananufaika zaidi kiafya. 

Anataja manufaa yaliyoko kwenye mafuta ya matunda na mbegu ni makubwa na bora zaidi, kuliko mafuta yaliyozoeleka kwa wengi katika matumizi ya kila siku. 

Anafafanua, awali alijihusisha na biashara ya matunda pekee, ikamkatisha tamaa kutokana na faida ndogo, ndio baadaye akahamia mauzo ya matunda. 

Mtaalamu huyo, anasimulia baadaye akapenya aliko sasa akianza na kufanya utafiti uliompatia  elimu kuhusiana na faida zinazopatikana na tunda au kokwa za matunda, akaona afanye biashara ya kusaidia kuboresha afya za Watanzania, kwa kujihusisha na kutengeneza bidhaa za mafuta yatokanayo na matunda hayo. 

Anaisimulia Nipashe kwamba, hiyo ilikuwa mwaka 2012 kwamba mbali na kuwa ekari 30 shamba la parachichi, wakati huo soko halikuwa zuri kama, akawa anajikita na kutoa faida yatokanayo na matunda anayoyafanyua kazi, akizalisha mafuta yanayouzwa ndani na nje ya nchi, ikileta tija katika afya za binadamu. 

MBEGU ZA MABOGA 

Twahir anaeleza kwamba matumizi ya mafuta anafananisha kuwa sawa na ubora wa mtu anayetumia samaki wa kawaida au dagaa, kutokana na kuwa na wingi wa viinilishe ‘magnesium’ na ‘zinki’. 

Hapo anaitambulisha kuwa mbegu pekee inayotoa madini mengi, ambayo wataalamu wengi wa afya na lishe wanashauri wajawazito wayatumie kwa nafasi ya viungo katika chakula, ikizuia watoto kuzaliwa na hali ya mtindio. 

Anafafanua kuwa, mjamzito anapotumia mafuta haya kila siku au unga utokanao na mbegu za maboga kwa, humsaidia kumkinga mtoto aliye tumboni na shida hiyo ya utindio. 

Mtaalamu huyo anataja nafasi nyingine, ni kwamba inawasaidia watu wanaokosa usingizi, wenye mawazo (stress), pia inawawezesha wazee kupata usingizi kwa usahihi. 

Lingine analieleza kwamba, watumiaji wanaongezewa ‘Vitamin A’ na viini vingi ukitofautisha, akiwa anafafanisha kwa ziada dhidi ya viinilishe kutoka mafuta ya kawaida ya kupikia. 

Twahir anataja sifa nyingine zilizopo kwenye mafuta hayo, ni kwamba hayagandi hata yanapowekwa kwenye jokofu (friji).

 Katika sura ya kijinsia, Twahir anawataja wanaume wanaotumia mafuta ya maboga au mbegu, inawafanya kuzuia tezi kutovimba, kwa sababu ya uwapo zinki kwenye mbegu hizo za maboga. 

Hiyo inatajwa kuendana na kuzuia uvimbe wa ubongo na kusaidia tezi zinazoanza kuvimba, zitanywea kutokana na kuwapo zinki nyingi kwenye mbegu au mafuta ya maboga. 

Mtaalamu huyo anatoa darasa lingine la kiafya kwamba kwa wanaotumia mafuta hayo kwenye chakula, mtiririko wake anatumia msamati ‘moja kwa moja’, akiunganisha na mfano wa dripu na sindano kwa mgonjwa, nafuu ikishuhudiwa kwa kasi na mtumiaji anaondokewa uchovu. 

MLONGE (MOLINGA)

Kwa majani ya mlonge, yanatajwa kuwa na  faida nyingi na katika mwili wa binadamu, yakiongoza kwa utoaji protini nyingi. 

Majani hayo ya mlonge kwa baadhi ya makabila nchini hutumia kama mboga, hivyo kiafya yana hadhi sawa na mboga ya maharage, kwa utajiri wake wa protini nyingi. 

Anataja ulaji mbegu za mlonge walau tatu kwa siku, anasema inasaidia kusafisha figo na kuweka sawa mifumo yake, kwa kuwa zinki an madini ya chuma kwa wingi kuliko vyanzo vingine asilia. 

Pia, mafuta ya mlonge anayapa sifa, kusaidia kuondoa sumu katika figo na maini na kufanya mzunguko wa damu kuondoa uchafu wote, ikiwamo maradhi ya UTI (mkojo mchafu), hali kadhalika kupandisha kiweango c ha kinga mwilini (CD4) kwa haraka, kwani mafuta hayo yana vitamin A na C nyingi. 

PARACHICHI, UBUYU, NYONYO

Mtaalamu Twahir, analitaja kuwa tunda lenye uwezo wa kutoa mafuta mengi kwa matumizi ya kupaka, pia ni mbadala wa mafuta ya mzaituni (Olive). 

Mafuta hayo yana virutubisho vya madini aina ya ‘potassium’ (madini ya chokaa), chuma, Vitamin A na E yenye faida kwa upande wa kuboresha afya ya moyo na kuleta unyororo wa ngozi na kuuweka uzee mbali sana.

 Pia, anasema kokwa hizo anazozalisha zinatoa mafuta yanayotumika kwa vipodozi na urembo, zikiuzwa katika masoko ndani na nje ya nchi. 

Anagusia mafuta ya nyonyo, yanasaidia kukuza nywele na kuondoa mba vichwani na inaimarisha afya ya ngozi, huku mashudu yanayopatikana baada ya kukamua mbegu za nyonyo, ikitumika kuzalisha mbolea nzuri kwa matumizi ya shambani. 

“Natamani Watanzania sasa waendane na mabadiliko ya matumizi hususani ya mafuta wanayotumia katika maisha yao ya kila siku hasa katika ulaji, watumie mafuta ya matunda kwani nibora bora kuliko,” anasisitiza Twahir.