Kwa kutumia TEHAMA bodi itawanasa wanaopiga chenga kurejesha mikopo

By Reubeni Lumbagala , Nipashe
Published at 07:58 AM Sep 24 2024
Wahitimu wakifurahia mahafali.
PICHA: MTANDAO
Wahitimu wakifurahia mahafali.

BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) inawapa mikopo wanafunzi wenye sifa na pia kukusanya fedha zilizokopeshwa kutoka kwa wanufaika hao wanapohitimu masomo.

Bodi inasisitiza kuwa  ni wajibu wa mwombaji kuzingatia kuwa fedha anazokopeshwa kugharamia masomo yake zinapaswa kurejeshwa ili ziwakopeshe wengine wenye uhitaji ili kuongeza idadi ya wasomi katika taasisi hizo na kuchagiza maendeleo.

Tangu 2004 bodi hiyo inawapa  wanafunzi wenye uhitaji hasa wanaotoka familia zenye kipato kidogo mikopo kutimiza ndoto za kufikia elimu ya juu.

Ni fedha za kugharamia ada, chakula, malazi, vitabu na mafunzo kwa vitendo kwa makubaliano ya kurejesha fedha hizo baada ya kuhitimu na kuwa na shughuli za kuwaingizia kipato iwe ajira rasmi au za kujiajiri na ujasiriamali.

Mikopo inatolewa  si tu kwa wanafunzi wa shahada bali pia wanavyuo wa  stashahada wanaosoma kozi za vipaumbele kama afya, ualimu hasa  sayansi na ufundi, usafirishaji, nishati, madini, masuala ya tiba, kilimo na mifugo.

Kazi ya kutoa mikopo kwa waombaji haina changamoto kubwa ikilinganisha jukumu la kukusanya fedha zilizotumika kusomesha.

 Maana wahenga walisema kukopa harusi, kulipa matanga. Kukusanya mikopo kutoka kwa wanufaika wake umekuwa na changamoto ikizingatiwa kuwa baadhi ya wahitimu hasa waliojiajiri kutojitokeza kulipa mikopo yao kwa hiari si jambo jepesi.

Tena baadhi ya wanufaika bado wana mtazamo kuwa wanapaswa kurejesha mikopo pale tu watakapoajiriwa kwenye sekta rasmi kama vile serikalini au ofisi binafsi, ndipo watakapoanza kulipa kupitia makato ya mishahara. 

Hivyo, wapo wanufaika wanaodhani mnufaika wa mkopo wa elimu ya juu hapaswi kulipa mkopo wake kupitia ajira yake binafsi kama vile mama na  babalishe, bodaboda, fundi uashi, seremala na mfugaji.

Huu ni mtazamo potofu. Lakini, pia wapo wachache wanaodhani pesa za umma hazina mwenyewe, wakifanya juhudi za kukwepa kulipa deni licha ya kwamba wapo ndugu zao wanaotegemea kupata fedha hizo.

HESLB wanasisitiza kuwa iIli mradi mnufaika anayo shughuli ya kumwingizia kipato iwe ni ajira rasmi yenye mshahara au shughuli binafsi za kujiajiri zinapompatia kiasi fulani cha fedha kwa siku au wiki, analo jukumu la kulipa deni.

Anatakiwa  kutenga fedha kwa ajili ya kupunguza deni lake kwa kulipa kupitia malipo ya serikali yanayofanyika kupitia ‘control number’ iliyoko kwenye taarifa ya mkopo.

Lengo ni kufanikisha kupata fedha na kuwawezesha    waombaji wengine  kupata mikopo kwa miaka mingine mingi ijayo.

Hivyo basi, kwa kutambua ugumu wa kukusanya fedha hasa kutoka kwa wanufaika waliojiajiri na wenye vipato halali, Bodi ya Mikopo imekuja na mfumo wa kisasa wenye kuhusisha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano TEHAMA.

Kwa njia hiyo waombaji wameunganishwa kwa kuwashirikisha wadau wengine muhimu kusaidiana kuwabaini wadaiwa mahali walipo na  kuongeza makusanyo.

Kwa kushirikiana na kuongeza makusanyo bodi itakuwa na  uwezo wa kukopesha waombaji wengi zaidi ikizingatiwa kuwa kuna ongezeko kubwa la waombaji wenye sifa hasa wanaomaliza kidato cha sita ambao wanahitaji mikopo kugharamia masomo yao vyuoni.

Mapema mwezi huu (Septemba 11, 2024), Bodi ya Mikopo ilibadilishana hati za makubaliano na taasisi tatu ambazo ni Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA.

Aidha, kipo chombo cha Credit Information kuongeza wigo wa kuwasaka wadaiwa na kuongeza mapato kwa ushirikiano.

Katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dk. Bill Kiwia anasema: “Katika kazi yetu ya kukusanya fedha za mikopo, tunawahitaji wadau hawa… 

Hivyo tunaomba mtufikishie ujumbe kwa wateja wetu kuwa sasa tunakwenda kufanya kazi na washirika watatu na wengine tutawatangazia siku chache zijazo. Tunalenga kuwafikia wadaiwa wote kwa kutumia mifumo.”

Ni ukweli kuwa bodi ya mikopo haiwezi kufanya kazi peke yake na wakafanikiwa bila kushirikisha wadau na kutumia mifumo ya kieletroniki hasa ikizingatiwa maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia yaliyopo sasa.

Na ndiyo maana kazi imehama kwenye utendaji wa kutumia mifumo ya kielektroniki badala ya makaratasi kwa kiwango kikubwa ili kuongeza ufanisi na ubora wa utendaji kazi.

Pamoja na hayo ni nia ya serikali kuwa ni lazima mifumo isomane ili kurahisisha kazi na kuongeza uwazi na uwajibikaji, nidhamu ya fedha na matumizi kwenye majukumu ya kuwahudumia Watanzania.

Kwa mujibu wa Dk. Kiwia, hadi sasa mikopo yenye thamani ya Shilingi bilioni 600 inapaswa kurejeshwa kutoka kwa wanufaika waliosoma katika vyuo mbalimbali.

“Mikopo ambayo imeshaiva ni Sh. trilioni 2.1 na hadi sasa zimerejeshwa Sh. trilioni 1.5, bado  bilioni 600 hazijarejeshwa, hivyo kama ilivyo kwa kampeni za urejeshwaji mikopo, tunaunganisha mifumo ili kuwafikia wanufaika wenye kipato waanze urejeshaji,” anasema Dk. Kiwia.

NIDA wanatarajiwa kusaidia kupatikana taarifa za makazi na mawasiliano ya wanufaika wa mikopo, hivyo, bodi ya mikopo itakuwa na uwezo wa kuchukua taarifa muhimu za mnufaika wa mkopo kupitia taasisi hiyo.

Ili kuongeza ufuatiliaji kutoka kwa mwanafunzi ambaye amehitimu masomo na ana kipato lakini bado hajaanza kurejesha mkopo uliotumika kumsomesha.

“NIDA jukumu lake ni kushirikiana na HESLB ili kuirahisishia kuwafikia wateja wake na kuwafikia wanufaika ambao hawajaanza kurejesha mikopo ili waanze kulipa,” anasema Deusdedit Buberwa, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NIDA.

Aidha, RITA ina jukumu la vizazi na vifo ambapo watakuwa kiungo kupitia mfumo wa kielektroniki kurahisisha wanafunzi kufanya mchakato wa mikopo kwa ufanisi.

Sanjari na hilo, Taasisi ya Credit Info Tanzania inafanya  jukumu la  kifedha la kukusanya taarifa za wakopaji wa benki na taasisi nyingine za kifedha, na hivyo mteja kabla hajaomba mkopo ni lazima apitie Credit Info.

Kwa mujibu wa Benki Kuu (BoT) inazitaka taasisi zote za fedha nchini kutafuta taarifa za mkopaji kutoka Credit Info kabla ya kumkopesha ili kujua historia ya mkopeshwaji.

Hivyo basi, Credit Info, inawajibika kufanikisha na kuwezesha mchakato wa ukopaji na urejeshaji mikopo kupitia jukumu lake la msingi la kuchakata taarifa za waombaji kupitia benki. 

Kwa mantiki hii, endapo bodi ya mikopo itapeleka taarifa za wanufaika wake ambao ni wadaiwa sugu Credit Info, kunaweza kusababisha wadaiwa wa bodi ya mikopo kukosa mikopo kwa sababu hawakopesheki kwenye taasisi mbalimbali za kifedha.

Huu utakuwa ni usumbufu kwao kukosa mikopo, kwa hiyo, ni muhimu kulipa deni la bodi ili kukopesheka kwenye taasisi nyingine za kifedha.

Vilevile, Septemba 13, 2024, Bodi ya Mikopo ilibadilishana hati za ushirikiano TRA kwa lengo la kubadilishana taarifa ili kuboresha utoaji na urejeshaji wa mikopo kutoka kwa wanufaika wake.

HESLB inafafanua kuwa kupitia TRA inaweza kutambua changamoto mbalimbali na hivyo kuboresha huduma zake. 

Mwandishi ni mwalimu wa Sekondari ya Mlali iliyoko Dodoma. 

Maoni: 0620 800 462