Kujua ufumbuzi wa shida kitaalamu ni mbadala wa wahubiri neno ‘wachawi’

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:04 AM Sep 11 2024
Mchungaji  Dominic Kashoix au Dibwe, aliyefungiwa kanisa kwa madai ya kukiuka maadili.
PICHA: MTANDAO
Mchungaji Dominic Kashoix au Dibwe, aliyefungiwa kanisa kwa madai ya kukiuka maadili.

WAKATI binadamu wanapokabiliwa na matatizo ulitarajiwa kuwa muda wa kuyatafakari kwa kina ili kupata ufumbuzi, lakini badala ya kusaka suluhisho, njia nyepesi zama hizi wengi ni kukimbilia kwa waganga na kwa viongozi wa dini.

Waganga hao ni wa ramli, kadhalika wahubiri ni wale wanaofundisha injili iliyoghoshiwa au kuchakachuliwa ili kukidhi wanachotomani walimu hao wa imani.

Zama hizi kumeibuka nyumba za ibada kwenye maeneo mengi hasa mijini wahubiri wakitanguliza majina na vyeo vyao, wako wanaojiita mitume hata manabii, jambo linalokua kila siku.

Ni jambo la kushangaza kwamba watu wengi wanapishana malangoni kwa wahubiri kupata ufumbuzi wa matatizo na changamoto zinazowakabili, sheria haziwazuii lakini wanatakiwa kujiongeza.

Inawezekana kuna matatizo mengine yanayozaliwa kwa wahubiri hao pasipo wenyewe kufahamu, mfano kufilisika kwa kutozwa sadaka kubwa, kulazimishwa kuacha shughuli za kiuchumi, chuki wanafamilia wakidaiwa ni wachawi na wakwamishaji.

Hivi karibuni Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango, alikemea suala hilo akisema yameibuka mafundisho ya kuwahamasisha watu kwenda kwenye nyumba za ibada kuombewa ili wapate mali ikiwamo nyumba, fedha, na kutatuliwa shida zao. 

“Tunashuhudia kuongezeka kwa wahubiri wanaojilimbikizia fedha na mali binafsi kutokana na sadaka na mauzo ya vitu mbalimbali vya hao watu wanyonge.”

Anasema: “Na wahanga wengi wa mahubiri ya aina hiyo ni watu wanyonge wanaokabiliwa na matatizo mengi kama umasikini, migogoro ya ndoa, ugumba na kukosa ajira.”

Ni muda sahihi kuamka kutoka kwenye usingizi wa pono na kijiepusha na utapeli mpya ambao unaendelea kushika kasi kupitia dini tena ukidaiwa kufanywa ndani ya nyumba za ibada. 

Inashangaza watu kujinadi kuwa wametumwa na mungu wakitamba moja kwa moja. Wanajigamba  kutatua shida na changamoto zinazowakabili wanadamu duniani hapa.

Wenye udhaifu wapokee miujiza ya uponyaji, wasio na ndoa wapate wenza na hata wale waliofiwa na ndugu na jamaa zao waweze kufufuliwa na kuishi tena.

Mafundisho haya yamewafanya wengi kuamini kuwa wanaweza kupata utatuzi na ufumbuzi wa matatizo yao mathalani kuongeza wateja katika biashara, kuboresha ndoa, kupona magonjwa, kuwa matajiri, ahueni katika migogoro ya kifamilia na ajira.

Pamoja na kwamba watu hawa huenda wakiwa na matarajio makubwa ya kupata ahueni ya matatizo yao, lakini wanaendelea kuibiwa na kutapeliwa sadaka na fedha za viingilio vya kuonana na wahubiri hao waongo.

Kuna haja ya serikali kuja na mikakati madhubuti ya kuwachunguza watu hawa hususan aina ya mafundisho wanayofundisha ndani ya nyumba za ibada.

Wengi wao wanatumia mwanya huo wa kuhubiri Neno la Mungu kama sehemu ya kuwarubuni na kuwaibia Watanzania ambao ni waamini. Hata hivyo, hukutana na masharti na maagizo magumu kutoka kwa viongozi hao wa dini. 

Kwa mfano ili kuwafanya waamini hao watoe fedha za kutosha kumewekwa hadi viingilio, kiasi cha kudhani kwamba unalipia kiingilio katika Uwanja wa Benjamini Mkapa kwenda kuzishuhudia Simba na Yanga zikichuana kumbe sivyo. 

Wakumbuke Neno la Mungu lenyewe linawaagiza wahubiri “kutoa bure” kwa kuwa karama hizo “wamezipata bure” kutoka kwa Mungu.

Waamini wanauziwa maji, mafuta, vitambaa hata na udongo na kuombewa kwa gharama kubwa hali inayosababisha hata vipato vyao kurudi nyuma tofauti na walivyodhani. 

Inawafanya wengine kuhisi kuwa ni mwisho wa dunia kama ulivyotabiriwa katika vitabu vitakatifu, kutokana na hayo yaliyonenwa na kutabiriwa hasa kupenda pesa na kumwacha Mungu.

Kwa kiasi kikubwa mafundisho ya sasa yanavuka mipaka ya kimaadili na mengine yanahamasisha chuki na uchochezi. Ikumbukwe mwishoni mwa Julai, Kanisa la Christian Life Church huko Buza jijini Dar es Salaam chini ya Nabii Dominiki Dibwa au ‘kiboko ya wachawi.’ 

Mhubiri huyo raia wa DRC anatoa mafundisho ambayo ni ya kiudhalilishaji na unyanyapaaji, madai yalitolewa hatua iliyofuatiwa na kupokea barua ya serikalini ya kumtaka asitishe shughuli zake za kidini mahali hapo kutokana na kile kilichodaiwa kuwa mafundisho yake yanakiuka maadili ya Kitanzania ikiwamo uchonganishi.

Aidha, alidaiwa kuwafundisha waamini wake kuua watu. Pia, sababu nyingine iliyotajwa kusababisha mgogoro kati ya nabii huyo na serikali ni kuwatoza waumini wake Shilingi 500,000 pale walipohitaji kuombewa, jambo ambalo ni kinyume cha maadili ya kidini. Hata hivyo, siku chache baadaye aliondoka nchini na kurejea DRC.

Ili kutoa ushuhuda na kuthibitisha kuwa Watanzania walikuwa wakiibiwa na kurubuniwa pesa zao, akiwa DRC anaonekana katika vipande kadhaa vya picha jongefu akiwakejeli Watanzania, mathalani wale waliokuwa wakimpatia fedha kwa ajili ya kuwafanyia maombi. 

Nabii Dibwe hivi sasa amevuka mipaka kiasi cha kutoa maneno machafu kwa wale waliokuwa wakitoa fedha hizo kwa ajili ya kufanyiwa maombezi kuwa ni “wendawazimu”.  Je, hii ni sawa? Na vipi kuhusu hawa manabii na mitume wengine ambao wanaendelea kutoa huduma maeneo mengine? Ni taswira gani inapatikana? Je, hakuna wengine walio na madhumuni kama ya huyu “Kiboko ya Wachawi?” 

Watanzania tumakinike na hili, tujikite katika kuchakata bongo zetu ili tujue matatizo yetu yanasababishwa na nini, na si kudhani kwamba biashara zetu zisipoenda vizuri basi tumerogwa. Ama eti mahusino yetu yakivunjika, kimbilio ni kwa nabii pekee penye suluhisho kamili. 

Mambo haya yanayoendelea hivi sasa hasa kupitia mikasa hii ya manabii, mitume na makuhani, yawe ni sehemu ya kutoa fundisho kwa watu wote wanaotumia fedha zao nyingi kwa manabii na mitume kwa lengo la kutaka kupata ufumbuzi wa matatizo yao ilihali matatizo yao yanabakia kuwa palepale. 

Watanzania waachane na kuamini uchawi na ushirikina au kutumia fedha nyingi kwa ajili ya kupata maombezi kwa viongozi hawa wa dini. Pia, mara kadhaa zimesikika shuhuda za watu waliosafiri umbali mrefu kwenda kuhudhuria ibada kubwa za manabii na mitume zilizopambwa kwa majina mazuri na makubwa kiushawishi.

 Lakini ibada hizo zilishindwa kutoa suluhisho katika matatizo yao, hata maji, mafuta, maandazi, udongo, vitambaa walivyopewa bado havikuweza kufua dafu badala yake vikawa kama sehemu ya kuongeza hasara ya upotevu wa fedha na muda kwa watu hawa. 

Je, hatuoni haja ya kutafuta vyanzo halisi vya matatizo yetu yanayotukabili na kuacha kurundikana kwa manabii, mitume na makuhani? Kwa maana sio kila tatizo lazima litatuliwe na nabii au mtume kama ambavyo watu wengi wanadhani na kufikiri.  

Umefika muda ambao Watanzania wanahitaji kupewa elimu ya kutosha ili kunusuru janga hili ambalo halijulikani lilianzia wapi, kadhalika ukomo wake bado ni kitendawili kigumu.

 Pia, ipo haja ya serikali kupitia kwa Msajili wa Jumuiya za Kiraia wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kufanya uchunguzi wa kina kuhusiana na asasi zote za kidini na kuhakikisha kuwa zile zilizomo nchini zinakuwa na vibali vinavyohitajika.

Ikumbukwe kuwa, suala la kukidhi vigezo na kuwa na vibali tu halitoshi badala yake mafundisho yote yanayotolewa kwa watu yanapaswa kuchunguzwa, kwani wengi wa manabii na mitume hao wamekuwa wakitoa mafundisho ambayo ni ya kupalilia ujanja na kujipatia mali.

Imeandikwa Na Godfrey Julius, UDSM