KIKUNDI MAARIFA KC....Kinamama wanaobadili shida zao hadi mapinduzi maendeleo

By Zanura Mollel , Nipashe
Published at 06:08 PM Apr 02 2024
Sehemu ya Ofisi ya Mtaa wa Saranga, Kimara, Dar es Salaam, kliniki ya mtoto na mjamzito inaendeshwa chini ya mti. Kikundi cha kinamama sasa kinafanyia mageuzi.
MAKTABA
Sehemu ya Ofisi ya Mtaa wa Saranga, Kimara, Dar es Salaam, kliniki ya mtoto na mjamzito inaendeshwa chini ya mti. Kikundi cha kinamama sasa kinafanyia mageuzi.

HADI sasa unatajwa, utawala bora unafanikiwa kubadili maisha ya Wakazi wa kata ya Saranga, baada ya kugeuza changamoto zao kuwa fursa kwao.

Kilichoko, wananchi wengi wamekuwa wakiamini maendeleo katika jamii yanapaswa kutekelezwa na serikali pekee, lakini wakazi wa kata hiyo sasa wanasema ‘hapana, maendeleo ni jambo la kila mmoja katika kuhakikisha taifa linapiga hatua.’

Sasa, wanatafuta njia ya kukabiliana na matatizo mbalimbali ikiwamo changamoto za miundombinu ya afya, elimu, pamoja na kujengeana uwezo kuinuana kiuchumi kama jamii. 

Maria Mwigune, Mwenyekiti wa Kituo cha Taarifa na Maarifa (KC) Kata ya Saranga Jimbo la Kibamba Wilayani Ubungo, anaisimulia Nipashe chanzo cha kituo hicho kuleta mageuzi ya kijamii na kubadili maisha ya mtu mmoja mmoja.

Anasema kuwapo changamoto ya maji katika Shule ya Msingi, Kimara ‘B’, Dar es Salaam, imewafanya wanafunzi wengi kusitisha safari ya kukosa maji na wakaugua maradhi ya UTI.

Ni hali iliyowakutanisha wazazi katika shule hiyo kujadili majibu ya kutatua tatizo hilo na kukaibuka mvutano wa wazazi kuchanga, lakini waraka wa elimu kwa wakati huo ulikataza michango kwa wanafunzi.

“Katika hili Mwalimu mkuu hakutuunga mkono kwa kuhofia kutokutii agizo la serikali,” anaeleza Mwigune na kuongeza: 

 “Nilivyoona kuna mvutano nikawaeleza wazazi wezangu anayetaka tuchange kwa ajili ya watoto wetu waweze kupata huduma katika mazingira salama wajitokeze, wakajitokeza wanawake 16.

“Tukasema kila mzazi mwenye mtoto shuleni achangie shilingi elfu moja kwa kila mtoto kwa ajili ya ukarabati wa miundobinu ya maji.”

Wazazi walijichanga wakipokea wazo na ndani ya wiki moja, wakafanikiwa kukusanya Sh. milioni 1.3, walizokarabatia kisima na kununua mota mpya, maji yakaanza kupatikana shuleni, ni kipindi kulikuwapo mlipuko wa ugonjwa UVIKO 19.

Anasimulia siku moja alipigiwa simu kutoka Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) wakimtaka kuhudhuria mafunzo na kikundi chake, wakaenda. Baada ya kupata elimu ya kubadilisha changamoto kuwa fursa, wakarejea kutoa elimu kwa makundi mengine, kutatua changamoto zao kijamii.

“TNGP walivutiwa na namna tulivyoweza kuelimisha na kushawishi jamii kutatua matatizo kwa kushirikiana, ndipo wakatuita kwenye mafunzo, tunawashukuru...” anasema Maria.

Ni kata yenye mitaa tisa, akisema wakachukua wajumbe watano wakapata mafunzo hayo kutoka TGNP, wakiweayaka kusambaza elimu hiyo kwingine, ili jamii ipate uelewea huo.

Maria anasimulia changamoto ziliibuliwa nyingi katika maeneno mbalimbali, Mtaa wa Saranga waliibua tatizo la ukosefu wa zahanati, inayowaumiza wajawazito wake, kufanyiwa vipimo katika Ofisi ya Kitongoji kipindi cha kliniki, wakiwa chini ya mti.

“Kama jamii tuliweka mpango wa haraka wa kuanza kukusanya michango kwa ajili ya ujenzi wa zahanati.

“Tulifanya hivyo kwa kuwa mazingira ya huduma ya afya yalikuwa hatarishi, kumpimia mtoto uzito kwa kumning’iniza kwenye miti...kinamama wakati wa kujifungua unapofika wanapelekwa Kituo cha afya Kimara,” anaeleza Maria.

Anasimulia kinamama walichanga fedha za ujenzi na mwaka 2022, mkakati kujenga zahanati ulianza, huku mbunge wa jimbo akiahidi kuchangiam kuunga mkono jitihada zao, ikkiwa ni zao la elimu waliopata, changamoto kuhamishiwa mtazamowa maendeleo.

“Ujenzi wa zahanati unaendelea, ila bado watoto wanapatiwa huduma ya vipimo kwa kuning’inizwa kwenye mti na wanawake bado wanafanyiwa vipimo kwa ajili ya kliniki kwenye ofisi ya mtaa” anasema.

Anataja shida nyingine inatyowakabili ni usumbufu walioupata kwa wasafirishaji (Bajaji) kukosa maegesho rasmi, hawakutambulika na kuna wakati wakatozwa fedha ambazo hazikujulikana zinakoenda.

‘Kama kituo tulibeba changamoto ile na kuwashauri njia sahihi ya kuweza kufanya shughuli zao ni kujisajili ili waweze kutambulika kisheria pamoja na kuhakikisha wanapatiwa eneo maalum.” Anasema na kuendelea;

“Walipokea ushauri wakafanya uchaguzi wa viongozi na kusajili kikundi chao na kisha walipatiwa eneo na serikali, wanaendelea na shughuli zao bila usumbufu. Ni matokeo ya kituo hiki,” anasema Mwigune.

WAKABILI UHALIFU

Hadi sasam, anasema kituo kimefanikiwa kudhibiti matukio ya kihalifu yaliyotokea katika eneo lililotambulika kwa jina maarufu “Chenji Hairudi”mtaa wa Stopover, ambayo yalihusisha biashara ya uuzaji mwili, ubakaji, wizi na uuzwaji wa pombe haramu.

Anasema kikundi chao kilimamua kuzungumza nao wakaeleza changamoto zao, hususani wafanyabiashara wakubwa, pia Mama Lishe namna ya kujikomboa kupitia mikopo sahihi na siyo ‘mikopo ya kausha damu’, hata wakajitenga na biashara ya uuzaji mwili.

Maria akasumilia: “Si lazima kuuza mwili ndio upate fedha ya kujikimu kimaisha. Tuliwafanyia vipimo vya afya na katika kukabiliana na mikopo kausha damu. tuliwajengea uwezo....

“Wamebadilika! Wana kikundi chao kinaitwa Elimika kina jumla ya watu 49, wanafanyabiashara kwa utulivu, amani wamegeuka kuwa walinzi na kuzuia biashara ya ngono.”

 Kwa mujibu wa Maria, eneo la ngono nalio limebadilika jina kutoka ‘Chenji hairudi,’ hadi sasa inaitwa Maendeleo.

MAZINGIRA

Vilevile hatua ikachukuliwa katika kumkwamua mwanamke na kijana kiuchumi, Maria anasema walipoona kata hiyo iko juu kuchafua mazingira, wao kikundi cha Taarifa na Maarifa, wakageuza hilo kuwa fursa kwa kutengeneza mbolea, inayotumika sasa kuzalisha mboga na kuotesha maua.

“Tulifanikiwa kupata mkulima wa pilipili kutoka mkoa wa Singida tulimuuzia ametupatia mrejesho kuwa mbolea hiyo inafaa pia katika kilimo hicho,” anasema.

Maria ana rai kwa serikali kuwasaidia kupata gari la kubeba taka, wapewe tenda ya kukusanya taka, pia wakihitaji kupanuliwa soko la mbolea. Lengo lao ni kuanzisha kiwanda kikubwa cha kuchakata taka kuwa mbolea.

DEREVA BAJAJI.

Longlinus Haule, ni dereva Bajaji katika kata ya Songara, anayesema walikuwa wakipitia changamoto ya usumbufu wa eneo la kupaki kwa shughuli zao, lakini baada ya kupatiwa elimu na uongozi wa kituo hicho, sasa utulivu umetawala kazi zao.

Anasema kikundi chao kina madereva 80, kimesajiliwa, kinatambulika kwa jina la Kumbajo. Awali walipatikana Mtaa wa Upendo na sasa wapo Kimara Stopover.

Akirejea zamani kipindi hawajasajiliwa, kulikuwapo kikin du kiitwacho Matembo, kikiwatoza ushuru shilingi 1000 kila siku jioni.

MWENYEKITI UWT.

Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi(UWT) Mtaa wa Stopover,  Habiba Magero,  anasema matukio ya kihalifu katika kata hiyo yamepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na jitihada zinazofanywa na kituo hicho cha kinamama.

“Hakuna mtu anayewaingilia katika utekelezaji wa majukumu yao, wanafanyakazi yao vizuri na wapo imara tunawashukuru....”anasema Habiba.

DIWANI SARANGA

Diwani wa Kata ya Saranga, Edward Laizer, anasema kata hiyo ina jumla ya wakazi zaidi ya 143,000 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi Mwaka 2022.

Anaeleza kuwa kituo cha taarifa na maarifa kilitambulishwa kwake na asasi ya TGNP, akinena: “Kituo hiki kimekuwa mkombozi katika kata hii kwa kusaidiana na serikali kutatua matatizo na kudhibiti uhalifu”.

Anasema Mtaa wa Saranga wananchi walichanga shilingi milioni 22 kujenga zahanati na mbunge wa jimbo hilo, Issa Mtemvu, kupitia mfuko wa jimbo alitoa shilingi million 10 kwa ajili ya kuongeza majengo na Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo kupitia makusanyo ya ndani kwa bajeti ya fedha mwaka uliopo, 2024/25, imetenga shilingio million 50 kusogeza ujenzi huo.

“Kata hii inawakazi wengi sana ndio sababu maendeleo yanakwenda taratibu, tumezungumza na TANROAD waweze kutupatia eneo la wazi (Road Reserve) ambalo linaonekana kuwa msitu na wahalifu hujificha humo,” anasema lazier.

Anataja lengo ni kuwekwa vibanda wafanyabiashara (machinga) na wamekubali kujenga vibanda 950 na wananchi watachangia kodi za kuvitumia.