Kane vs Watkins nani anapaswa kuanza England?

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:02 AM Nov 18 2024
Kane vs Watkins nani anapaswa kuanza England?
Picha:Mtandao
Kane vs Watkins nani anapaswa kuanza England?

KULIKUWA na hisia tofauti za kutofahamika kwa Harry Kane kuwekwa benchi Alhamisi pale jijini Athens wakati England ikicheza na Ugiriki kwenye mchezo ambao ulikuwa ni lazima washinde.

Kane ni mfungaji bora wa 'Simba Watatu' hao na alishafunga mechi za kufuzu za Ligi ya Mataifa ya UEFA dhidi ya San Marino, Bulgaria na Albania.

Lakini sasa Kane amekutana na mtu wa kucheza kamari ambaye ni kocha wa muda wa England, Lee Carsley. 

Bosi huyo wa muda wa England alimwacha nahodha wake benchi Alhamisi usiku kwa mchezo ambao ulikuwa na umuhimu zaidi kushinda dhidi ya Ugiriki, na badala yake akamchagua Ollie Watkins wa Aston Villa kuanza kama mshambuliaji kiongozi.

Ni uamuzi ambao Carsley alisema kuwa Kane alikuwa nao "sawa kabisa", ingawa mshambuliaji huyo wa Bayern Munich anaweza kuwa alikuwa akiugulia moyoni wakati alipokuwa akitazama mchezo huo huku Watkins akifunga bao la kwanza kwa njia ya kuvutia katika ushindi mnono wa mabao 3-0.

Ilionekana kwamba England ingeweza kuishinda Ugiriki bila mshambuliaji wao huyo mahiri. 

Lakini uchezaji wa Watkins kule Athens ulizua swali ikiwa anafaa kuwa kiongozi wa safu ya ushambuliaji ya Simba Watatu hao wakati Thomas Tuchel atakapochukua jukumu la kuwa kocha mkuu wa kikosi cha England 2025.

Sasa, makala haya yanakuchambulia ulinganisho wa washambuliaji hao wawili, na tathmini ya nani anafaa kuanza kwa kikosi cha England. 

Kufunga mabao

Bao la Watkins, Alhamisi lilikuwa la tano kwake kuifungia timu ya taifa katika michezo 18, na lilikuwa aina ya bao ambalo tumezoea kuliona likifungwa na Kane kwa miaka mingi. 

Fowadi huyo wa Villa alijiweka sawa na kupiga mkwaju kwa urahisi akitumia vizuri asisti ya mlinzi Noni Madueke.

Watkins ana wastani wa kufunga bao kila baada ya dakika 121.2 kwa Simba Watatu hao, huku mfungaji bora wa muda wote wa England, kwa wastani, akifunga kila baada ya dakika 115.9. Hii ni rekodi ya Kane aliyofunga mabao 68 katika mechi 102 ambayo ni bora.

Kuna wachache bora kuliko Kane. Alikuwa anainyemelea rekodi ya Alan Shearer ya kufunga mabao mengi kwenye Ligi Kuu England kabla ya kuondoka kwenda Bayern Munich, ambapo alifunga mabao 36 ya Bundesliga katika kampeni yake ya kwanza. 

Watkins alifunga mabao mengi zaidi katika msimu mmoja wa mabao 19 (2023/24) na aliongoza kwa mara ya kwanza mbele ya Kane ambaye alimwongoza mara saba.

Fowadi wa Bayern ni mpiga mpira wa kutisha ambaye huwa sahihi kutoka miguu yote miwili. Yeye ni gwiji katika eneo la penalti na mmoja wa wachezaji bora kwenye yadi 12. 

Katika msimu mmoja tu kati ya misimu nane iliyopita ya ligi, Kane alifunga chini ya kiwango chake cha mabao msimu wa (2021/22), kwa mujibu wa FBref.com 

Tofauti na Watkins, ambaye amefanya vibaya katika misimu minne kati ya saba. 

Uchezaji wake wa juu zaidi ni msimu uliopita, wakati Kane amekuwa bora kwa misimu saba mfululizo.

Ingawa Watkins amefanya vema katika umaliziaji na ni mzuri sana anapopiga mpira kutoka pembeni, yeye si mfungaji bora kama Kane. 

Umiliki wa mchezo na ubunifu

Msimu wa Watkins wa mabao 19 wa Ligi Kuu England wa 2023/24 ulifanywa kuwa wa kuvutia zaidi kwake. 

Nyota huyo muhimu wa Kocha Mkuu wa Villa, Unai Emery, aliongeza pasi 13 za mabao kwenye hesabu yake ya kuhusika kwenye mabao msimu huo.

Na ndio rekodi bora zaidi kwa msimu mmoja katika maisha yake ya soka hadi sasa. 

Mara moja tu Kane ameboresha takwimu hiyo. Alirekodi asisti 14 kwenye ligi msimu wa 2020/21 wakati huo akicheza kwa upatina mzuri na Son Heung-min aliyekuwa kwenye kilele chake cha ubora.

Kane anacheza vema akiwa nyuma ya goli na bila shaka anajivunia upigaji pasi wa hali ya juu. 

Amekuwa akicheza kama namba 10 katika miaka michache iliyopita, huku mielekeo yake mikali ikielekea kwenye lango la wapinzani na alionekana kuifurahia nafasi hiyo.

Mshambuliaji huyo wa zamani wa Tottenham Hotspur pia ni gwiji wa kushinda faulo. Kwa hiyo mara nyingi anaweza kuipa timu yake ahueni kwa kupata mipira ya adhabu.

Watkins anaimarika kama mwezeshaji, kwa uwezo wake wa kujipanua pembeni na kufungua nafasi kwa wachezaji wenzake na sehemu kubwa ya uchezaji wake si wa moja kwa moja. 

Mshambuliaji huyo alisaidia kwa njia nyingi msimu uliopita, huku aina mbalimbali za onesho zikielezea mabadiliko ya Watkins. 

Nyota huyo wa Villa ni mchezaji anayeanza kuibuka kama mbunifu, lakini uthabiti wa Kane katika nyanja hizi kwa miaka mingi inamaanisha lazima atahitaji muda zaidi kujifunza. 

Maisha marefu

Enzi ya Tuchel inaelekezwa kuelekea Kombe la Dunia la 2026, na hilo ndilo tunalotazamia katika mjadala wa Kane dhidi ya Watkins.

Hadi michuano hiyo itakapoanza Juni 11, 2025, Kane atakuwa na umri wa miaka 32 na atafikisha miaka 33 baada tu ya michuano hiyo. 

Umri si jambo la kusumbua sana, huku mshambuliaji huyo akiwa na matumaini ya kufurahia kazi ndefu. 

Hata hivyo, kutokana na idadi kubwa ya michezo ambayo amecheza tangu akiwa Tottenham katika miaka yake ya mapema ya 20 na kuzorota kimwili kulikodhihirika kwenye michuano mikubwa, kuna wasiwasi kuhusu hali ya afya ya Kane kufikia Kombe la Dunia la 2026.

Kwa ujumla Kane amekuwa akisumbuliwa na jeraha katika miaka ya hivi karibuni kutokana na matatizo ya kifundo cha mguu wakati wa Kocha Mauricio Pochettino akiwa Spurs, lakini hakuna ubishi kwamba idadi ya dakika anazocheza msimu mzima huleta mchango mkubwa. 

Kwa mara ya kwanza kabisa, Gareth Southgate alikuwa tayari kumuacha Kane ili kumpa nafasi Watkins kwenye Euro 2024. 

Mshambuliaji huyo alikuwa akikabiliana na tatizo la maumivu ya mgongo kipindi cha majira ya joto.

Watkins ni mdogo kwa Kane kwa miaka mitatu, lakini atakuwa na miaka 30 mwanzoni mwa Kombe la Dunia la 2026. 

Siku hizi, huo si umri wa kuwa na wasiwasi kuhusu kudhoofika kimwili, lakini ataweza kuwa katika ufanisi kwenye kufanya kile ambacho kinatakiwa? 

Huenda ikabidi kuwe na mageuzi katika mchezo wa mshambuliaji huyo ikiwa anataka kufanya vema katika kiwango cha juu kwenye miaka yake ya 30.

Kwa washambuliaji wote wawili, usimamizi kwao utakuwa muhimu ili kuingia kwenye mashindano. 

Hakuna sababu ya kuamini kuwa Kane atadhoofika sana kimwili katika kipindi chote cha mzunguko wa Kombe la Dunia, lakini huu unaweza ukawa ndio mwisho wake kama mchezaji mkuu wa England. 

Nani anafaa zaidi kwa Tuchel?

Hili ndilo swali muhimu na gumu. Kane ni mshambuliaji bora kuliko Watkins, lakini je, yuko vizuri kimbinu kwa timu hii ya England?

Kwa mfano kwenye Euro 2024, Southgate alihangaika sana kupata usawa na ubora wa Kane akimchezesha na Jude Bellingham, lakini ilionekana kama alikosekana mtu wa kulisha mipira mbele ya nusu mstari.

Watkins anaweza kufanya vipengele vya kile Kane anafanya kwa mtazamo wa kumiliki mpira na ubunifu, na nia yake ya kunyosha uwanja kwa kufungua nafasi kwa wachezaji wa England kung'ara. 

Kwa kuzingatia mfumo wa Tuchel, Watkins ataweza kuwalisha vizuri zaidi mipira wachezaji kama Bellingham, Cole Palmer na Bukayo Saka, hivyo nyota huyo wa Vila bila shaka ni chaguo la kuvutia.

Hata hivyo, kocha anayekuja wa England pia anajua hatari ya Kane atakapopewa mkimbiaji wa kumlisha mpira mbele. 

Kama Anthony Gordon angepata nafasi zaidi kwenye michuano ya Euro, uchezaji wa Kane hakika ungeboreshwa huku kikosi cha Southgate kingekuwa na nguvu zaidi upande wa kushoto.

Tuchel tayari amefanya kazi na Kane huko Bayern. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 31, alitikisa nyavu mara 44 katika mashindano yote msimu uliopita. 

Kane anatazamia kufanya kazi tena na Mjerumani huyo, huku Tuchel akiendelea kumpigia debe fowadi huyo wakati alipokuwa Bavaria, akieleza kuwa ni 'hatari' kumfundisha Kane.

Kuzoeana huku kunamaanisha kuwa Tuchel atajaribu kumfanya Kane kuwa wa kwanza kwake kabla ya kumgeukia Watkins.