DUMA BOKO ATIKISA; Anatisha kwa mawaziri vijana yupo mwenye miaka 26

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 08:37 AM Nov 27 2024
Rais wa Botwsana, Duma Boko
Picha: Mtandao
Rais wa Botwsana, Duma Boko

MWEZI huu wa Novemba kwa Botswana umeweka historia si kwa taifa hilo la kusini mwa Afrika pekee bali kwa bara zima.

Ni baada ya wananchi kusema ‘noo’ kwa chama tawala na kuunga mkono upinzani walioupigia kura za ushindi zikikiendea chama cha Umbrella for Democratic Change (UDC).

UDC ilipewa baraka kupitia kura za kuking’oa mamlakani chama tawala kilichodumu kwa takribani zaidi ya nusu karne kwa kupata kura za ushindi wa kishindo.

Chama tawala cha Botswana BDP, kilichokuwa kinaongozwa na rais aliyemaliza muda wake, Mokgweetsi Masisi, kilishindwa katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 30, mwaka huu.

Ushindi huo unahitimisha miaka 58 ya utawala wa chama hicho madarakani na kuongeza historia ya vyama tawala kwenye nchi zipatazo mbili barani humo kuondolewa madarakani na vijana majasiri wanaotoka vyama vya upinzani hivi karibuni.

Historia iliandikwa nchini Senegal taifa lililoko Afrika Magharibi linaloongozwa na rais kijana zaidi Bassirou Diomaye Faye (44) na sasa Botswana, inayoongozwa na Rais Duma Boko (54).

Botswana takribani asilimia 70 ya wakazi wake ambao ni milioni 2.3 ni vijana walio chini ya umri wa miaka 35, huku asilimia 70 ya idadi ya watu kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, umri wao ni chini ya miaka 30.

Kwa upande mwingine, Faye, alishinda uchaguzi wa rais wa Senegal wakati Boko naye ameapishwa kuwa rais Botswana.

Taswira za viongozi hao zinatafsiriwa kwa namna tofauti na wachambuzi wa kisiasa kwamba ni viongozi vijana wanaokuja na mbinu tofauti kwa timu wanayoambatana nayo kuongoza wakiwachagua vijana wenzao.

Rais Boko wa Botswana, baraza lake la mawaziri alilolitangaza linakadiriwa takribani asilimia 45 ya mawaziri ni vijana. 

Kati ya mawaziri 18 miongoni mwao tisa umri wao ni chini ya miaka 50, kwa mujibu wa Shirika la Habari la Uturuki (TRT).

Wachambuzi wanaeleza kwamba hatua hiyo ni kuweka msisitizo wa kuwa na sura mpya za viongozi, kuendana na naye.

Kuna waziri kijana zaidi katika Baraza la Mawaziri la Rais Boko, binti Lesego Chombo, mwenye miaka 26 ambaye ni Waziri wa Vijana na Masuala ya Jinsia.

Lesego Chombo

Chombo ni mwanasheria na mrembo akiwa Miss Botswana 2022 na pia ni ‘Miss World Afrika 2024’.

Jacob Kalebeng (35), ni Waziri wa Michezo, akiwa na shahada ya sayansi ya siasa, huku Stephen Modise (37), ni Waziri wa Afya, lakini pia ni daktari wa binadamu na ana shahada nyingine katika elimu.

Bogolo Kenewendo (37), ni Waziri wa Madini, akitazamiwa kuimarisha uchumi kupitia sekta hiyo hasa madini waliyonayo nchini humo ambayo ni almasi.

Kenewendo ana shahada ya uzamili katika uchumi wa kimataifa, kutoka chuo kikuu cha Sussex cha Uingereza na shahada ya uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Botswana.

Waziri wa Serikali za Mitaa na Masuala ya Utamaduni ni Ketlhalefile Motshegwa (40), ana shahada ya sayansi ya jamii na ya uzamili katika viwanda, ajira na uhusiano.

Kadhalika Rais Boko, amemteua Phenyo Butale (44), kuwa Waziri wa Mambo ya Nje, ambaye ana taaluma ya lugha na ana shahada ya uzamivu-PhD katika eneo hilo pia.

Kwenye Wizara ya Uchukuzi na Usafirishaji, ni Noah Salakae (47), elimu yake ni mhandisi na meneja miradi huku David Tsher ana umri usiozidi miaka 50, akiteuliwa kuwa Waziri wa Mawasiliano na Ubunifu.

Ana shahada ya sayansi na masuala ya uhandisi tiba kutoka Chuo Kikuu cha US, huko Marekani. Pia Makamu wa Rais Ndaba Gaolathe (52) ana shahada katika hisabati na nyingine ni kwenye utawala, biashara, uchumi na sheria. 

Waziri wa Sheria na Masuala ya Kubadilisha Mwenendo ana miaka 54 naye ni Nelson Ramaotwsana akiwa na shahada ya uzamili ya sheria.  

Waziri wa Ofisi ya Rais, Moeti Mohwasa (55), ana shahada na ni mhariri wa habari.

RAIS BOKO 

Rais Boko, amebobea kwenye haki za binadamu na ni wakili. Elimu yake ya uanasheria ilianzia nchini mwake, hatimaye kwenda Shule Kuu ya Sheria ya Harvard, huko Marekani.

Kwa miaka 50 wapinzani wa kisiasa nchini humo, wamekuwa wakiota ndoto, kukivua madaraka chama kikuu cha BDP, lakini ni Boko pekee ndiye aliyefanikisha hilo.

Mbinu ya ushindi wa chama chake cha Umbrella for Democratic Change ilishangaza. Yeye mwenyewe Boko, amekiri kushtushwa na idadi hiyo ya kura za ushindi.

“Ninaweza tu kuahidi (kwa watu) nitafanya kila niwezalo. Nitakaposhindwa, nitawatazama wao, waniongoze.”

Katika muda wote wa kampeni yake, mikutano ya hadhara, Boko alikuwa akiwaomba wafuasi wake kuja karibu na kuwasikiliza malalamiko ya wapigakura njia ambayo ilimfanya kuwavutia vijana.

Akizaliwa mwaka 1969, katika wilaya ya kati nchini humo, katika mji mdogo wa Mahalapye. Boko daima alikuwa na hisia ya heshima, kulingana na marafiki.

Wakati wa shule, alichaguliwa kuwa rais wa baraza la wanafunzi, wakati kwenye  taaluma ya sheria, aliibuka kuwa mmoja wa wanasheria wakuu nchini, kulingana na mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Lesole Machacha.

 Ushindi wa upinzani nchini humo ambao haukutarajiwa ni pigo kubwa la chama tawala na Masisi aliyeingia madarakani mwaka 2018.  Chama chake kimekuwa madarakani tangu Botswana ilipopata uhuru kutoka kwa Uingereza, mnamo mwaka 1966.

MITANDAO