Fahamu silaha kuu za Awamu Sita zinazoibua mapinduzi ya afya nchini

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:02 AM Oct 24 2024

Rais Samia Suluhu Hassan, alipozuru katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, jijini Dodoma mapema mwaka huu.
PICHA: MTANDAO.
Rais Samia Suluhu Hassan, alipozuru katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, jijini Dodoma mapema mwaka huu.

HADI sasa kuna uwekezaji unaoendelea kutekeleza Sera ya Afya Mwaka 2007, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika staili yake anatumia namna kuu mbili kufanikisha anayolenga, katika mradi ulioasisiwa katika Serikali ya Awamu ya Tatu, kwa jina Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM).

Rais katika ubunifu wake, ameweka mgawanyo ambao katika sura moja unagusa miundombinu inayopatikana katika namna kuu mbili; huku rasilimali watu nayo kitaalamu anaikuza kwa mgawanyiko wa aina mbili.

NGUVUKAZI AFYA

Eneo la rasilimali watu, serikali pia imewekeza katika kutanua idadi wataalamu afya na wakati huohuo, kuna uboreshaji tija kwa wakati mmoja safu yao, kukiwapo ajira mpya inayoongozwa kila mwaka kukidhi mahitaji ya nchi.

Hiyo inaendana na kasi ya uboreshaji kitaalamu uzalishaji mabingwa wa tiba kitaifa serikali ijitegemee, kupitia kinachoitwa Mpango wa Udahili wa Masomo ya Serikali, maarufu ‘Samia Health Specialization Scholarship Program’ unaopeleka masomoni wataalamu 300 kila mwaka, 2024 mwaka huu ikiwa na bajeti Sh. bilioni 14.

“Changamoto ya upungufu wa watumishi katika sekta ya afya inatokana na kukua idadi ya watu, ambayo inaongeza uhitaji wa wataalamu wa afya na walimu, lakini endapo Tanzania itakua kiuchumi changamoto hiyo itaondoka,” anasema Rais Dk. Samia.

Hapo mkuu wa nchi ameamua kutumia tafsiri ya ‘maendeleo na kujitegemea’ katika afya kwa maana nchi kukidhi mahitaji yake kwa idadi, pia ujuzi unaopunguza safari ya tiba za ugenini kama vile nchini India, Tanzania.

Utashi wa kimaendeleo hapo ni nchi kuwa na idadi ya kutosha ya wataalamu na wenye uwezo wa kuhudumia mahitaji tiba yanayojitokeza nchini, hata kwa majirani; nyenzo za kufanyia kazi zikiwapo katika namna endelevu.

Pia, Dk. Samia anafafanua kuongezeka rasilimali watu katika Sekta ya Afya ni la mustakabali mpana, yakitegemea jitihada za pamoja, ikiwamo serikali, sekta binafsi, wadau na taasisi za kidini kuwekeza katika vichocheo vya uwekezaji, kuongeza ubora wa huduma za afya nchini.

Hadi sasa Tanzania ina sheria, pia sera inayohusu ubia kati ya sekta binafsi na serikali, maarufu PPP.

Rais katika kuongeza idadi ya watumishi wa afya, anaahidi serikali itaendelea kutoa vibali vya ajira kila mwaka katika sekta ya afya, ili kupunguza uhaba wa watumishi hao, kutokana na maendeleo katika sekta hiyo.

Katika nafasi hiyo, Rais Dk. Samia anawasifu wabia, Taasisi ya Benjamin Mkapa, inayochukua hatua ya kuboresha rasilimali watu na mikataba yao inapoisha, wanaajiriwa na serikali.

Mfano wa namna ya pekee, Rais anachukua hatua hizo za kuajiri, ikishuhudiwa mapema mwaka huu mkoani Tanga, serikali iliajiri kundi la watumishi katika mgawanyiko wa madaktari wanane; wafamasia saba; wataalamu maabara 20; na wasaidizi afya 22.

Wengine wasio wataalamu afya moja kwa moja, ni wahudumu wa wateja (5); wasaidizi hesabu (8); wasaidizi ustawi jamii (4); na mtunza kumbukumbu mmoja.

Badaaye, Julai mwaka huu kukaonekana tangazo ligine la kukaribisha maombi ya watumishi afya nchini 9,483 kutumika mikoa: Arusha (9), Dar es Salaam (3), Geita (38), Iringa (26), Kagera (18) na Katavi (32). 

Manufaa yake ndio kinachoshuhudiwa kuwapo kikosi cha wataalamu wajuzi tiba kutoka Hosptali ya Taifa wanaozunguka kitaifa kusambaza ujuzi tiba na wakati huo huo, wanatoa huduma kuhusu watoto wachanga wagonjwa na hasa wenye umri chini ya siku 28.

Wajuzi hao na wenzao wengi wanaopatikana sasa, ndio wamewezesha hata kufanyika utalii tiba, wageni kuja nchi kusaka tiba na wao wakialikwa nchi jirani kutoa msaada.

MRADI MIUNDOMBINU

Sura ya pili ya uwekezaji iko katika miundombinu, dira ikijikita katika majengo, vifaa tiba, pamoja na dawa husika, kukabili shida za afya mahitaji ya tiba.

Rekodi hadi miezi saba iliyopita, inaonyesha katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wake hadi kufika mwezi Machi mwaka huu, Rais Dk. Samia, kawekeza majengo 1,061.

Hiyo inagusa kutoka majengo 8549, hadi 9,610 huku mpango MMAM kwenye miaka 16 tangu uanze kutumika, ukielekeza kila kijiji au kitongoji kuwa na zahanati, kata kuwa na kituo cha afya, wilaya inakuwa na hospitali yake.

Pia hivi karibuni kukawapo uwekezaji wa fedha shilingi trilioni 1.02 katika ukarabati wa majengo ya zamani na kuendelea na ujenzi wa jengo jipya la wagonjwa, binafsi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

UHALISI UNAOENDELEA

Kunatajwa ukamilishaji awamu za hospitali ya Kanda ya Kusini Mtwara na Hospitali ya Kanda Chato, ikiendana na upanuzi wa miundombinu kwa kujenga majengo mapya katika hospitali za rufani kanda (usimikaji mitambo ya kutibu saratani na mambo mengineyo); Kaskazini KCMC; Kanda Mbeya; Benjamin Mkapa- Dodoma na Bugando (Mwanza).

Pia hospitalini Sekou Toure (Mwanza); Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe (Dodoma), Hospitali ya Magonjwa Ambukizi Kibong’oto, Moshi.

Ni mpango unaozifikia hospitali mpya za rufani katika Mikoa ya Katavi, Njombe, Songwe, Simiyu na Geita.

Pia, kuna ya kuhamisha hospitali tano kutoka majengo yake ya zamani hadi mpya za kisasa kwenye mikoa ya Ruvuma, Shinyanga, Singida, Mara na Lindi, Rukwa, Kitete (Tabora) na Ukerewe (Mwanza).

Katika ngazi za msingi, rekodi ya Wizara ya Afya zinataja hospitali mpya za halmashauri 127 zimejengwa, kati yake 95 zimeanza kutoa huduma kwa wagonjwa tangu mwanzo wa mwaka na kuna ukarabati umefanyika kwa hospitali kongwe, kama vile Bombo ya jijini Tanga.

Ni takwimu inayofikia ujenzi wa vituo vya afya 367. Pia, hadi mapema mwaka huu, kuna maboma ya majengo ya zahanati 980 yamejengwa hata kuchangia ongezeko la vituo vya kutoa huduma za afya nchini.

Jedwali la kiserikali linafafanua kwamba, asilimia 80 ya wananchi wanapata huduma za afya ndani ya umbali wa kilometa tano ya maeneo wanakoishi, lengo kufikia asilimia 95 ifikapo mwaka 2030.

Hospitali tano nchini nazo zimehama kutoka majengo yake ya zamani, hadi mapya ambazo ni za rufani katika mikoa ya: Ruvuma, Shinyanga, Singida, Mara na Lindi.

Katika sura ya juu kuna hospitali za rufani ngazi ya mkoa, kanda, hospitali maalum kama vile za moyo na afya ya akili na MOI, juu kabisa kunakuwapo Hospitali ya Taifa ambayo ni Muhimbili (MNH).

Mgawanyo ulioko na asilimia wa uwiano kwa jumla kuu katika mabano; zahanati 7,999 (83.2%); vituo vya afya 1,170 (12.3%); hospitali wilaya 181(1.9%); hospitali rufani za mkoa 28(0.3%); hospitali zenye hadhi sawa na mkoa 36 (0.4%); hospitali za hadhi ya kanda 12 (0.1%); hospitali maalum sita (0.1%); na hospitali ya taifa iko moja (0.01%).

Ni aina ya tafsiri fulani ya matumizi ya pesa, inayotokana na jumla ya shilingi trilioni sita kuwekezwa katika Sekta ya Afya.  

HALI YA VIFAA

Ndani ya uwekezaji kiafya unaoendelea nchini, Rais Dk. Samia, amwekeza pia katika vifaa kukiwapo shilingi bilioni 14.9 zilizozinduliwa na aliyekuwa Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, kusaidia ununuzi wa vifaa tiba kwa majimbo na halmashauri 214 nchi nzima.

Mtazamo mkuu wa Rais Dk. Samia, pia unagusa kumaliza vifo vinavyosababishwa na uzazi, hiyo ikiwa sehemu ya uwekezaji katika sekta ya afya.

Pia Naibu Spika wa Bunge, Mussa Zungu, anampongeza Rais kutoa magari ya kubebea wagonjwa kwa wabunge wote 528, lengo ni kuboresha sekta ya afya nchini, hiyo ilikuwa hadi Novemba mwaka jana.

“Rais Samia ametoa magari hayo kwa wabunge kwa lengo likiwa kuhakikisha vifo vya mama na watoto vinapungua,” anatamka Naibu Spika Zungu.

Mwaka huu, Waziri wa Afya, Jenista Mhagama ameipongeza Bohari ya Dawa MSD), kuendelea kuhakikisha inanunua vifaa vinavyohitajika kusaidia kuokoa maisha ya watoto wanaozaliwa njiti.

Ni kauli yake katika hafla kukabidhi vifaa tiba maalumu vya kuwasaidia watoto wenye matatizo ya kupumua, kwa  Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk. Mohammed Mang'una kwa niaba ya waganga wakuu wote nchini.

Ni vifaa tiba 130 vyenye thamani ya Sh. 212,854,365, vilivyonunuliwa na MSD, kutekeleza agizo la Rais kusaidia kupunguza vifo vya watoto njiti, waziri akisisitiza ununuzi huo uwe endelevu.